Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Bunge: Hakuna mbunge anayetudai

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
OFISI ya Bunge imesema hakuna mbunge yeyote ambaye hajalipwa stahili zake kwa kuhudhuria Mkutano wa Tatu wa Bunge uliofanyika mwezi uliopita mjini Dodoma.

Aidha, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah amewataka wabunge wa Chadema wanaodai hawajalipwa, kupeleka idadi yao ili waangalie kwa nini hawajalipwa kwani ofisi hiyo imewalipa fedha wabunge wote na haina tatizo la fedha.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Mbeya, Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto alidai kuwa wabunge hawajalipwa posho zao ikiwa ni pamoja na posho ya kugharimu mafuta ya safari za wabunge majimboni.

Madai hayo yalipingwa na Katibu huyo wa Bunge ambaye alibainisha kuwa katika ofisi yake huwalipa wabunge kwa kipindi, hivyo fedha zao za Mkutano wa Tatu uliofanyika Aprili mwaka huu, wamelipa zote.

“Kama kuna mbunge hajalipwa fedha hizo, mbona hajafika kulalamika? Kama yupo au wapo wanachotakiwa waje ili tuangalie kwa nini hawajalipwa hadi leo, lakini tatizo si ukata katika ofisi yangu,” alisema Katibu wa Bunge.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alidai katika mkutano huo wa hadhara kwamba wabunge walikuwa hawajalipwa posho za kugharamia safari zao majimboni, kwa sababu Serikali haina fedha.

“Serikali imeshindwa kukusanya kodi inavyotakiwa, Serikali imeshindwa kusimamia vizuri kodi yenu, matokeo yake sasa imefilisika,” yalikuwa madai mazito ya Zitto katika mkutano huo kama alivyonukuliwa jana na baadhi ya magazeti yanayochapishwa nchini.

Akizungumzia madai hayo ya Serikali kufilisika ikiwamo kushindwa kulipwa watumishi wa umma, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo alisema ni madai mazito na Serikali inaandaa tamko rasmi.

Akiwa Dodoma ambako leo atahudhuria semina elekezi kwa watendaji wakuu wa Serikali wakiwemo mawaziri, Mkulo alisema Serikali itatoa tamko leo.

0 comments

Post a Comment