Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CCM kwawaka moto • UTEUZI WA DK. SHEIN WAZUA HOFU, WAJUMBE WAFURA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kiko hatarini kumeguka kwa upande wa visiwani Zanzibar baada ya baadhi ya wanachama wake kuutuhumu uongozi wa juu kukiendesha chama kwa misingi ya kufuata maslahi ya watu wachache badala ya wananchi.
Wanachama hao wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa huu ndiyo wakati wa chama hicho kudondoshwa kwenye uchaguzi mkuu, unaotarajia kufanyika Oktoba 31 mwaka huu na mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad.

Kuteuliwa kwa Makamu wa Rais Dk. Alli Mohamed Shein juzi usiku kuwa mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho, kwenye uchaguzi mkuu ndiko kumezusha mtafaruku huo ambao uliwafanya wajumbe watoleane maneno ya kashfa nje ya ukumbi makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa na baadhi ya wajumbe kutoka visiwani Zanzibar wakilaumu viongozi wa juu wa CCM, akiwemo Rais Jakaya, kwa kutumia nguvu, fedha na vitisho ili Dk. Shein apate nafasi hiyo.

Dk. Shein aliibuka mshindi kwa kupata kura 117 dhidi ya kura 54 za Dk. Mohamed Gharib Bilal na 33 za Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha.

Kura hizo, zilipigwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho walioketi juzi jioni kupitisha jina moja kati ya matatu.

Wajumbe hao, walionyesha kukerwa na rafu hizo huku wakibainisha kuwa chama kinaweza kupoteza ushindi visiwani Zanzibar, sambamba na kuibuka kwa makundi makubwa yanayosababishwa na majeraha ya mchakato wa uteuzi wa mgombea urais.

Baadhi ya makada hao mara baada ya kumalizika kwa mchakato wa kuteua jina moja la mgombea urais wa Zanzibar, waliamua kuondoka kwa hasira mkoani Dodoma huku wakijiapiza kumsubiri mgombea wa chama chao Zanzibar.

“Tumesikitishwa sana na rafu na matumizi ya fedha yaliyoratibiwa na viongozi wa juu wa chama chetu, lakini watambue fika wanapoteza misingi ya demokrasia na kuaminika,” alisema mjumbe mmoja kwa niaba ya wenzake.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kutoka Zanzibar walikuwa wanataka Dk. Bilal ateuliwe, lakini walizidiwa nguvu na wajumbe wa bara ambao inasemekana waliandaliwa kumpitisha Dk. Shein.

Wakati wajumbe hao, wakionekana kupigwa dafrao na hatua ya wenzao wa bara, chanzo kingine kimedokeza kuwa Dk. Bilal aliangushwa pia kutokana na kumchagua mmoja wa wabunge machachari kwa kukemea ufisadi kuwa msimamizi wa zoezi la kuhesabu kura zake.

Kimebainisha kuwa makada wanaopingana na msimamo wa mbunge huyo baada ya kuona kitendo hicho, walikasirika na kuamua kutompa kura Dk. Bilal kwa madai ya kushirikiana na kada anayewachafua wenzake kwenye vyombo vya habari kwa kuwaita mafisadi.

Hata hivyo, wajumbe hao wamebainisha kuwa CCM, itabidi ifanye kazi ya ziada kumpigia kampeni Dk. Shein kwa kuwa anapambana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharrif Hamad mwenye ushawishi mkubwa visiwani humo.

Wajumbe hao, waliionyesha dhana ya Uunguja na Upemba ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa ikikitafuna kisiwa hicho chenye upinzani mkali baina ya vyama vya CCM na CUF.

Moja kati ya hoja zinazojengwa kuhusu kupitishwa kwa Dk. Shein ni kuwa kiongozi huyo ni Mpemba ambaye atasaidia kwa kiasi kikubwa kuvunja ngome imara ya upinzani iliyojengwa kwa miaka mingi chini ya utawala wa Maalim Seif.

Mjumbe mmoja wa NEC, amelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa huenda leo kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho, ulioanza jana Rais Kikwete akamchagua Dk. Bilal au Nahodha kuwa mgombea mwenza ili kufukia majeraha yaliyosababishwa na uteuzi wa mgombea urais.

Amedokeza kuwa kama Dk. Bilal atateuliwa kuwa mgombea mwenza Nahodha anaweza kuendelea na wadhifa wake au kupanngiwa kazi nyingine kwa minajili ya kutuliza machangu aliyoyapata baada ya kushindwa.

Katika kile kinachoonekana kuwapoza Bilal na Nahodha, Rais Kikwete alisema viongozi hao ni muhimu kwa Zanzibar na taifa na kama hawakupata nafasi ya urais upo uwezekano wa kupata nafasi nyingine ya uongozi.

Alisema umri wa Nahodha unaruhusu na anaweza kuingia kwenye kinyang’annyiro hicho miaka inayokuja huku akimsifu Dk. Bilal kwa ukomavu na uzoefu kwenye medani ya siasa.

“Nashukuru Nahodha katuambia yuko kwenye meli yetu, si mmoja wa wale wanaotaka meli ivunjike na kuzama ili tugawane mbao, lakini ni vema tukajua kila mwenye subiri yuko pamoja na Mwenyezi Mungu ......usipopata kwa hili, utapata kwa lile, nchi ni yetu sote tushirikiane ili tupate ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Kikwete.

Hata hivyo mjumbe huyo anasema CCM, sasa imepalilia zaidi uhasama baina ya makada wake ambao kila mmoja amekuwa na kundi linalomuunga mkono huku likiamini kuna hila zimefanyika ili kumbeba Dk. Shein.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuteuliwa, Dk. Shein alisema anaamini atawaunganisha Wazanzibari kuwa kitu kimoja na yale yote yaliyojitokeza wakati wa mchakato ni sehemu ya siasa.

Naye Dk. Salim Ahmed Salim, alisema anamini kuwa Dk. Shein ni kiongozi safi na makini atakayeisaidia Zanzibar kuwa moja na kuendeleza yale mazuri yaliyofanywa na Rais Aman Abeid Karume, anayemaliza muda wake.

Awali Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, alisema chama hakiwezi kupasuka au kugawanyika kwa sababu ya urais wa Zanzibar kwa sababu wanachama wake, wanajua kuwa kila wanapokuwapo washindani zaidi ya mmoja ni lazima apatikane mshindi.

Wengine wanaotajwa kuteuliwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Seif Khatib, Zakhia Meghji, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud, na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Omar Yusuf Mzee.
Tags:

0 comments

Post a Comment