Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Hoja ya kuahirisha uchaguzi na kuunda serikali ya mseto Zanzibar yawasilishwa rasmi baraza la Wawakilishi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KIONGOZI wa kambi ya upinzani kwenye Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakari jana aliwasilisha rasmi hoja binafsi ya kutaka kutenguliwa kwa vifungu vya katiba ya Zanzibar ili kumpa fursa Rais Amani Abeid Karume kukamilisha kazi ya kufungua milango ya serikali ya umoja wa kitaifa.

Zanzibar imekuwa na matumaini ya kumalizika kwa siasa za chuki tangu Rais Karume afanye mazungumzo na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Novemba 5, mazungumzo ambayo yalisababisha chama hicho kitangaze kumtambua Karume kuwa rais wa visiwa hivyo.

"Ndio nimewasilisha hoja yangu leo kwa katibu wa baraza," alisema mwakilishi huyo kutoka chama kikuu cha upinzani visiwani hapa, CUF baada ya kuwasilisha hoja yake jana asubuhi kwa katibu wa baraza.

"Nina haki ya kuwasilisha hoja hiyo na kama nilivyozungumza na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam kuwa nitawasilisha kwa hivyo nimetekeleza azma yangu."

Kwa mujibu wa kanuni ya 50 (1) ya Baraza la Wawakilishi, iwapo mjumbe anataka kuwasilisha hoja binafsi katika kikao, atatakiwa kuiwasilisha kwa spika siku mbili kabla.

"Iwapo kwa mujibu wa kanuni hizi taarifa ya hoja inatakiwa kutolewa, basi taarifa hiyo itabidi itolewe kwa maandishi, itiwe saini na mjumbe anayeitoa na ipelekwe kwa katibu ili aipokee kufuatana na masharti ya fasihi ya (1) ya kanuni hii," inaeleza kanuni hiyo.

Kanuni hiyo inaendelea kueleza kwamba muda wa chini kabisa wa kutoa taarifa ya hoja ya kutaka kufanya mabadiliko katika hoja inayotolewa ama katika Baraza la Wawakilishi au katika Kamati ya Baraza utakuwa ni siku moja kabla ya kikao kutokana na dharura.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee Ibrahim alikiri kupokea hoja hiyo kutoka kwa kiongozi wa kambi ya upinzani, hali kadhalika Spika Pandu Ameir Kificho atatoa taarifa katika kikao kinachoendelea iwapo itakuwa imekamilika.

Katibu alisema spika ameipokea hoja hiyo na hivi sasa ameanza kuifanyia kazi ili kuona kama kuna uwezekano wa hoja hiyo kuwasilishwa barazani kwa ajili ya majadiliano.

Kiongozi huyo wa upinzani aliwaambia waandishi wa habari mapema wiki hii kuwa anataka vifungu namba 39,42 na 61 vya katiba ya Zanzibar virekebishwe kuruhusu serikali ya umoja wa kitaifa.

Bakari ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CUF, alisema katika hoja yake hiyo ametaka kuwekwe utaratibu utakaowezesha kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Mjumbe huyo ambaye alishawahi kushika nyadhifa kadhaa kwenye Serikali ya Mapinduzi (SMZ), alisema lengo la hoja yake ni kuyapa nguvu maridhiano ya kitaifa yaliyotokana na mazungumzo kati ya Rais Karume na Maalimu Seif.

Alisema anapendekeza serikali hiyo ya umoja wa kitaifa, izingatie uwiano wa kura katika uchaguzi wa rais.
Tags:

0 comments

Post a Comment