Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Magufuli atangaza operesheni safisha Dar

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amempa siku tano Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam awe amewaondoa katika hifadhi za barabara watu wanaoendesha shughuli zao katika maeneo hayo kinyume cha sheria.


Amri hiyo ya Dk Magufuli inaagiza kuondolewa kwenye maeneo hayo wachuuzi wa bidhaa mbalimbali pamoja na magari yanayoegeshwa sehemu hizo kiasi cha kuayafanya kuwa gereji bubu.


Agizo hilo la Dk Maguguli limekuja kipindi ambacho Jiji la Dares Salaam ambalo ni kitovu cha shughuli za kiuchumi na biashara nchini, likiwa linakabiliwa na tatizo la msongamano wa magari, ambalo pamoja na mambo mengine, linatokana na ukiukwaji wa sheria mbalimbali zikiwamo za barabarani.


Jana, akizungumza wakati wa uzinduzi wa stendi mpya ya mabasi Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema hakuna sababu ya watu hao kubaki katika hifadhi za barabara wakati sheria zipo na kusisitiza, "Hata kama mkikuta milingoti ya bendera ya CCM vunjeni."


Dk Magufuli alisema, Sheria ya Barabara ya mwaka 1987 inasema wazi kuwa mtu ambaye atakutwa anafanya biashara, kuegesha gari, kumwaga mafuta au uvamizi mwingine wa namna yoyote katika hifadhi ya barabara, adhabu yake ni faini ya Sh1 Milioni.


Alimwagiza meneja huyo kuwa Tanroads haipo kisiasa na wao wapo kusimamia sheria na sio vingine. "Mpo kusimamia sheria, acheni kupiga siasa," alisisitiza.


Huku akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria uzinduzi huo, Dk Magufuli alisema ni lazima ndani ya siku hizo tano, wachuuzi na waliovamia hifadhi za barabara kuondolewa na kusisitiza kuwa sheria haina chama, iwe Chadema, CCM ama kingine chochote.


"Mnyika (John ambaye ni Mbunge wa Ubungo) kawaambie wenzako wa CUF, UPDP na vyama vingine kuwa sheria haina mswalie mtume," alisisitiza Dk Magufuli, huku akiwaonya watendaji wa manispaa ambao wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya wanaovunja sheria.


Dk Magufuli alitoa mfano wa wafanyabiashara wa eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakikwaza ujenzi wa barabara ya Bagamoyo kutokana na kupanga bidhaa zao barabarani.


''Ukienda Tegeta watu wamepanga biashara barabarani, Mkuu wa Mkoa upo, Mbunge yupo, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) yupo, diwani yupo, mkuu wa wilaya naye pia na wote hao wanaangalia tu, ndio Tanzania hiyo?," alihoji na kusisitiza kuwa ifike sehemu sheria iachwe ifanye kazi.


Alisema kutokana na hali hiyo, biashara ya namna yoyote haitaruhusiwa katika stendi mpya ya Mbezi Mwisho na hakuna tozo yeyote kwa daladala na mabasi ya abiria ambayo yataitumia stendi hiyo.


Foleni Dar
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli alieleza kuwapo kwa miradi mitano inayotekelezwa ili kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.


Alisema Sh350 milioni zimepatikana mpaka sasa kwa ajili ya ununuzi wa kivuko ambacho kitasafirisha abiria kutoka Bagamoyo hadi jijini Dar es Salaam kwa kutumia gati saba zitakazowekwa katika maeneo tofauti hadi eneo la Feri.


"Tunakusanya pesa kwa ajili ya Kivuko hicho na hadi sasa zimepatikana Sh 350milioni na sio lazima kila ajaye mjini kutoka eneo ambako bahari inapita apande daladala," alisema Magufuli.


Dk Magufuli amelitaka jiji la Dar es Salaam pia lijipange kuangalia jinsi ya kukabiliana na msongamano wakati hatua zingine zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kutafuta wahisani ambao wanaweza kushirikiana na wadau wengine.


"Bakhresa (Said Salim) anasafirisha ngano zake kwa kutumia reli, hebu zungumzeni naye ikiwezekana mtu wa Pugu, Gongolamboto na hata Vingunguti wasilazimike kukimbilia daladala," alisema Dk Magufuli na kuongeza kuwa amepokea maombi ya barabara 27 za Dar es Salaam ambazo zinatakiwa kupandishwa hadhi.


Alisema miradi mitano ya barabara za pembezoni inatekelezwa katika jiji la Dar es Salaam, ambayo anaamini itasaidia kupunguza msongamano katikati ya Jiji hilo.


Waziri Magufuli alimtaka pia Mkurugenzi wa Tanroads kumpa majina ya wakurugenzi wa Jiji ambao hawajatumia pesa walizopewa kwa ajili ya miradi ya barabara.


"Nipe majina yao ili niyapeleke kwa Rais Jakaya Kikwete ili awafukuze kazi," alisema Magufuli na kuongeza kuwa kuna pesa ambazo zinatolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, lakini zinatumika kulipa posho za madiwani na vitu vingine vya namna hiyo.


Mipango kutatua foleni Dar
Kwa muda mrefu Serikali Kuu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji na manispaa zake za tatu, imekuwa na mikakati ya kutatua tatizo la foleni, lakini hadi leo hazifanikiwa.


Tayari Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa aliwahi kubuni mpango wa matumizi ya njia tatu za barabara, lakini baadaye mpango huo uliyeyuka na hadi sasa tatizo hilo bado lipo.


Rais Kikwete pia aliwahi kutangaza mpango wa ujenzi wa barabara za juu katika viunganishi vya barabara muhimu, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wowote.


Pia, kwa karibu muongo mmoja sasa kumekuwa na mradi wa mabasi yaendayo kasi katika jiji hilo la Dares Salaam (Dart), lakini hadi sasa hakuna dalili zozote za kukamilika.

0 comments

Post a Comment