Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Madiwani Arusha walipwa mamilioni ‘kutalii’ Kigali

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HALMASHAURI ya Jiji la Arusha limezidi kuzama katika tope la kashfa ya matumizi mabaya ya fedha baada ya madiwani wake watano kutumia mamilioni ya fedha kusafiri kwenda Kigali, nchini Rwanda, kuhudhuria tamasha la michezo ya Umoja wa Serikali za Mitaa (EACLARSA).


Tamasha hilo hufanyika kila mwaka kwa kuwakutanisha wanamichezo mbalimbali kutoka Umoja wa Serikali za Mitaa katika nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Mwaka jana, tamasha hilo lilifanyika Kigali, Rwanda kati ya Desemba nne na tisa.


Wanamichezo wanaotakiwa kushiriki ni wale ambao wako katika halmashauri hizo na michezo iiliyoainishwa ni pamoja na ile ya asili kama ngoma, kwaya, mashairi, maigizo na michezo mingine ya aina hiyo.


Kwa upande wa Tanzania ni Halmashauri ya Jiji la Arusha pekee iliyoshiriki tamasha hilo. Hata hivyo, kashfa inayojitokeza katika safari hiyo ni ukweli kwamba, waliosafirishwa ni madiwani watano na maofisa wawili wa halmashauri hiyo na si wanamichezo husika.


Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili la Raia Mwema kutoka ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha ambazo hata hivyo, bado hazijathibitishwa, zinadai kuwa ujumbe huo wa madiwani na maofisa hao wawili, ambao idadi yao inafikia saba, uliandamana na kile kinachotajwa kuwa ni timu ya wanariadha wanne.


Hata hivyo, hakuna uthibitisho kutoka kwa wahusika kwamba kulikuwa na timu ya riadha iliyokwenda Kigali na pia vigezo vilivyotumika kuwachagua wanamichezo hao walioshiriki na kiasi cha fedha walizolipwa.


Msafara wa watu hao unadaiwa kusafiri kwa njia ya barabara kutoka Arusha wakipitia Kenya, Uganda hadi Kigali, Rwanda kati ya Desemba 2, mwaka jana na kuwasili Desemba nne na kwamba, walifikia katika Hoteli ya Sky, iliyoko katikati ya Jiji la Kigali.


Habari zinadai kuwa ziara hiyo ambayo tayari imeanza kuleta ‘ufa’ miongoni mwa madiwani, ilifanywa kinyemela bila wajumbe wengine wa Baraza la Madiwani kuarifiwa, kama taratibu zinavyoelekeza.


Wamekuwa wakidai kufanya hivyo kwa sababu Meya wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo, ndiye aliyewateua madiwani hao.


Madiwani wanaotajwa kwenda katika ziara hiyo ya ‘kutalii’ na kata zao kwenye mabano ni pamoja na Julius ole Sekeyan (Terat), Issa Omari (Unga Ltd), Karim Mushi (Lemara), Paul Lotta Laizer (Baraa). Katika orodha hiyo, Julius ole Sekeyan anatajwa kuwa ndiye makamu mwenyekiti wa umoja huo.


Mwingine katika msafara huo ni diwani wa CHADEMA, kata ya Engutoto, Elibariki Marlley. Kwa upande wa watumishi wa halmashauri katika msafara huo ni Ofisa Utamaduni na Michezo, Godfrey Mollel na mwenzake, Ntegejwa Hosea, ambaye ni Ofisa Uhusiano.


Taarifa za kiuchunguzi zinabainisha kuwa hadi sasa, hakuna maelezo ya kutosha kuhusu ziara hiyo inayodaiwa kugharimu takriban Sh. milioni 20 za Halmashauri. Kitita hicho cha fedha kinatajwa kugharimia posho, nauli na malazi kwa ‘wasafiri’ hao.


Taarifa za uhakika ambazo Raia Mwema imezipata zinadai kuwa madiwani hao watano walilipwa wastani wa Sh. 3,150,000, kila moja ikiwa ni posho ya safari kwa siku moja, kwa kila mjumbe. Posho hiyo ni sawa na malipo ya Sh. 450,000, kwa siku kwa kila msafiri.


Hata hivyo, wakati madiwani wakilipwa posho hiyo nono, watumishi wawili waliohudhuria tamasha hilo wanadaiwa kulipwa posho ya Sh. milioni 1.8, ambayo ni wastani wa Sh. 200,000, kwa siku.


“Ukijumlisha fedha zote hizo ni karibu Sh. milioni 20 zilitumika katika ziara hiyo na suala hilo limeleta mtafaruku wa ndani kwa ndani miongoni mwa madiwani ambao hawakubaliani na ziara hiyo,” kilieleza chanzo chetu cha habari.


Hoja za wanaopinga ziara hiyo zinajengwa juu ya msingi kuwa ziara hiyo haikuwahi kuwepo katika kalenda ya halmashauri na fungu la fedha zilizotumika katika safari hazikuwa katika bajeti ya halmashauri na pia waliopaswa kuhudhuria tamasha hilo ni wanamichezo na si madiwani ambao si wanamichezo.


“Kama kulikuwa na nia njema na ya kweli katika ziara hiyo basi wangeongeza idadi ya wanamichezo na maofisa hao wawili na diwani moja tu, si kupeleka idadi kubwa ya madiwani ambao hawakuwa na shughuli yoyote ya muhimu katika tamasha hilo zaidi ya kwenda kutalii,” alisema diwani moja wa CCM ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.


Diwani huyo aliongeza: “Hawakuona hata aibu ya kufanya gender balance (uwiano wa kijinsia katika msafara) badala yake wamekwenda wanaume tu hii si haki na ni matumizi mabaya ya fedha za umma na madaraka”


“Tumewauliza baadhi yao wanajenga hoja kuwa walikuwa katika ziara ya kujifunza masuala mbalimbali kama mipango miji, usafi na ujenzi wa barabara, sasa sisi tunajiuliza kuwa baadhi ya madiwani wako katika nafasi hizo kwa zaidi ya miaka 10 sasa mpaka leo hawafamu wananchi wa Arusha wanahitaji nini mpaka wakajifunze?” alihoji diwani huyo wa CCM.


Wakati madiwani CCM wakitoa hisia zao chini ya “zulia” wenzao wa CHADEMA wameweka wazi nia yao kumchukulia hatua za kinidhamu diwani wao aliyeshiriki ziara hiyo bila ya kupata idhini ya chama.


Katibu wa madiwani wa chama hicho, Isaya Doita ambaye ni diwani wa Kata ya Ngarenaro, aliliambia gazeti hili kuwa tayari wamekwishamwita diwani huyo ili ajieleze kuhusu safari hiyo.


“Tumeshamwita ili ajieleze alipata wapi idhini ya kwenda katika tamasha hilo bila kuuarifu uongozi wa chama ingawa kwa sasa ni mapema kusema kuwa ana makosa kwa sababu bado hatujampa nafasi ya kumsikiliza,” alieleza Doita.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Levolosi, Ephata Nanyaro, alisema ziara za aina hiyo hazina tija kwa halmashauri kongwe kama ya Arusha na kwamba ni moja ya njia zinazotumika kutafuna fedha za wananchi.


“Ziara za aina hiyo zinabuniwa na wataalamu kama njia ya kuwalainisha madiwani ili pale wanapotaka kupitisha bajeti ya miradi waongeze fedha kwa lengo la kuzitafuna,” alisema Nanyaro.


Akizungumza Raia Mwema kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki iliyopita, kiongozi wa msafara huo, Julius ole Sekeyan, alitetea ziara hiyo akisema hakuna dosari yoyote na kuelekeza auliwe Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomih Chang’a.


“Kwani kuna nini? We unatafuta njia ya kunichafua lakini nataka nikuambie kuwa ukiniandika ‘kienyeji’ nitakuchukulia hatua za kisheria taarifa zote za ziara hiyo anazo Mkurugenzi wa Jiji, nenda kamuulize yeye,” alisema Sekeyan huku akifoka.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji (Chang’a) alithibitisha kuwapo kwa ziara hiyo na kuongeza kuwa ililenga kuhudhuria tamasha la Umoja wa Serikali za Mitaa kwa nchi za Afrika Mashariki.


“Ni Kweli wamekwenda katika ziara hiyo na tulilipia gharama za safari ila siwezi kukumbuka kiasi cha fedha walizolipwa pamoja na idadi ya wanamichezo waliokwenda, wasiliana na Ofisa Utamaduni na Michezo (Mollel), ana taarifa nzima ya ziara hiyo,” alisema Chang’a.


Chang’a hakuwa tayari kujibu maswali zaidi kwa madai kuwa alikuwa anaingia katika kikao maalumu kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi, ofisini kwake.


Hata hivyo, Raia Mwema ilipowasiliana na Mollel alidai kusafiri na timu ya wanariadha wanne ambao hata hivyo, alikuwa hakumbuki majina yao kwa wakati huo.


“Ni wanariadha wa Arusha ila siwakumbuki lakini tulishinda medali mbili za shaba katika mbio za mita 1,500 na mita 5,000 na sikuweza kwenda na wanamichezo wengi zaidi kwa kuwa halmashauri yetu haina fedha,” alidai Mollel.


Meya wa Mji wa Arusha, Gaudance Lyimo, ambaye halmashauri anayoiongoza inatuhumiwa kwa utendaji usiokidhi viwango, hakupatikana kuzungumzia ziara hiyo kwani kila mara alipopigiwa simu yake iliita bila kujibiwa.


Kwa kipindi kirefu madiwani wa Halmashauri ya Manispaa yaArusha (kabla ya kuwa jiji) wamekuwa wakinyooshewa kidole kwa baadhi yao kujihusisha na ufisadi katika sekta mbalimbali kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu.


Moja na mifano ya matukio hayo ni lile la mwaka 2006, ambalo matokeo yake ni Chama cha Mapinduzi (CCM), kumvua madaraka alyekuwa Meya wa Arusha, Paul Lotta Laizer, pamoja na madiwani wengine wawil.


Madiwani hao waliovuliwa madaraka yao pamoja na meya huyo ni Musa Mkanga na Mary Kisaka, wote wakituhumiwa kuuza uwanja wazi ulioko karibu na soko la Kilombero, kinyume cha sheria, kanuni na taratibu.

0 comments

Post a Comment