Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Tanzania yakataa ushirikiano ulinzi, siasa EAC

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
TANZANIA imekataa Shirikisho la Ulinzi, Siasa pamoja na Kinga za Viongozi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutaka mambo hayo kujadiliwa kwa upana zaidi kuhusu uundwaji wake ili wananchi waweze kushirikishwa kutoa maoni yao.


Hata hivyo Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki, wamekubaliana kwa pamoja kuunda Sekretarieti maalum ya Watalaam wa kufuatilia mchakato mzima wa maoni ya watu ili waweze kuyawasilisha katika mkutano ujao.


Katika mkutano huo pia kumependekezwa kuanzishwa kwa Benki Kuu Umoja wa Jumuiya ya fedha, Bunge la Jumuiya lenye uwakilishi wa Kisiasa , Mamlaka ya Uangalizi, mahakama ya Jumuiya Afrika mashariki itakayosimamia na kuhakiki mikataba .


Akizungumza na waandishi wa habari , Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki , Dk Stergomena Tax alisema Tanzania haijakubaliana na Uundwaji wa Shirikisho la kisiasa , Ulinzi na Ardhi kwa madai kuwa masuala hayo yanahitaji muda zaidi wa kujadiliwa na wadau husika wa Jumuiya.


Aliyataja mambo mengine yaliyokubaliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Baraza la Mawaziri kuwa ni pamoja na Sera ya mkakati wa uendelezaji wa viwanda, Kuimarisha Huduma ya Forodha, Itifaki ya kuzuia na kupambana Rushwa sambamba na Itifaki ya kinga na hadhi ya jumuiya zilizopo chini ya Jumuiya.


Dk .Tax Alisema suala la Ulinzi Shirikishi na siasa katika mkutano huo liliibua mjadala mzito na kuonekana kuwa changamoto inayohitaji kufikiriwa kwa makini ili kuepusha nchi husika kuingia katika migogoro baina ya nchi na nchi pale zitakapo pingana .


“Nikitolea mfano mambo ya vita katika kushirikiana na kusaidiana na nchi inayopigwa ndani ya Jumuia ya Afrika mashariki linatakiwa kujadiliwa kwa kina na kufanyiwa marekebisho ili kujua mambo gani muhimu yatakayohusika katika Ulinzi ili kuweza kujulikana na kukubaliana” alisema Dk Tax.


Katika Mkutano huo Tanzania imeteuliwa kuwa Mwenyeji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika mashariki ambaye Makao Makuu yake yatakuwa Zanzibar huku Rwanda ikichaguliwa kuongoza Kamisheni ya Sayansi naTeknolojia na Burundi ikiongoza Kamisheni ya Utafiti wa Afya.


Alisema upataji wa wenyeji huo unatokana na Tanzania kuwa mwombaji pekee sambamba na kuomba nafasi zingine za Afya na Sayansi na Teknolojia ambazo haikufanikiwa badala yake ilionekana kuwa na sifa katika Kamisheni ya Kiswahili.


Alisema kwa kupata nafasi hiyo Tanzania itanufaika kwa kiasi kikubwa katika kuinua Uchumi wake kutokana na kuwepo kwa soko huria katika sekta za biashara ,viwanda na uwekezaji katika kupunguza vikwazo vya uchumi.


Katika kongamano la Jumuia ya Afrika mashariki kuhusu Maendeleo ya Bonde la ziwa Tanganyika, Katibu huyo alisema , walijadili nchi wanachama kuvutia biashara na kuongeza uwekezaji katika nchi wanachama ili kutumia maliasili nyingi zilizopo kwaajili ya kuinua uchumi.


Dk Tax alisisitiza kuwa Tanzania haina budi kulipeleka Suala la Ardhi, Ulinzi, Siasa kwa wananchi ili walijadili zaidi kwani matokeo ya awali yalionyesha kuwa asilimia 75 ya Watanzania walikataa uharakishwaji wa uundwaji Shirikisho hilo .


Dk Tax alisema nchi wanachama zinatakiwa kupima Ardhi na kuanzisha vyombo vya msingi vinavyotoa haki ya umiliki wa ardhi kwa wananchi , Kusimamia mgawo wa faida, na gharama za mali asili kuwa sehemu ya majadiliano katika mkataba wa uundwaji wa shirikisho la kisiasa.


Kuhusu maombi ya uanachama wa Nchi za Sudan Kusini na Sudan Kaskazini , alisema majadiliano hayo yalifanyika na kwamba Sudan Kaskazini ilikosa vigezo vya kujiunga kutokana na umbali uliopo katika mipaka na nchi wanachama .


Alisema Sudan Kusini ilikidhi katika ibara ya tatu ya vigezo vya kujiunga lakini majadiliano zaidi yanaendelea ili kuhakikisha wanapata mwafaka zaidi katika kuweza kujiunga .

0 comments

Post a Comment