IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SERIKALI YADAIWA KUZUIA UCHUNGUZI WA VIGOGO
KASHFA nyingine imeikumba Serikali ya Tanzania, kufuatia tuhuma kwamba ina mkakati maalumu kuzuia watuhumiwa wa ufisadi wa rada kufikishwa mahakamani.Taarifa za mtandao wa Wikileaks ambao umekuwa ukifichua siri za kidiplomasia na ufisadi duniani, umeibua tuhuma hizo mpya kwa Serikali na kwamba hicho ndicho kikwazo cha watuhumiwa husika kutofikishwa mahakamani.Taarifa ya mtandao huo uliyosambazwa jana imeeleza kuwa mpango huo, ndio ulioathiri jitihada za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Clare Shot kuzuia Tanzania kuuziwa rada hiyo.
Kwa mujibu wa mtandao huo, juhudi za Shot zilijumuisha kuinyima Tanzania misaada inayofikia Paundi 35 Milioni kutokana na kununua rada hiyo kwa bei ya kuruka.
"Pamoja na shinikizo hilo, juhudi za Shot zilishindwa kabisa kuzuia ununuzi wa rada hiyo ambayo thamani yake ilikuwa Paundi 28 Milioni kutoka kwa kampuni ya BAE Systems ya Uingereza," ulisema mtandao huo na kuendelea:
"Suala hilio si jipya. Gazeti la The Guardian la Uingereza liliwahi kutoa ripoti yake ya uchunguzi wake kuhusu uuzwaji wa rada hiyo ambao ulimsababishia pia Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, Tony Blair kuamuru kikosi chake cha kuchunguza makosa makubwa (SFO) kuingilia kati na kuchunguza namna BAE ilivyohusika."
Ilichobaini Wikileaks ni kwamba viongozi wa Serikali ya Tanzania ilikuwa ikifanya juhudi za kuficha kasoro zote zilizokuwa katika mpango wa ununuzi wa rada hiyo.
Hata kwa upande wake, mtu mahususi aliyetakiwa kushughulikia kashfa hiyo kwa kufanya uchunguzi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru), Dk Edward Hoseah alinukuliwa akimweleza Afisa wa Ubalozi wa Marekani nchini kwamba aliwahi kutishiwa kuuawa mara kadhaa na kukumbushwa kwa ujumbe wa maneno kila siku.
Mara kadhaa, kutokana na kashfa hiyo ya rushwa, Serikali ya Uingereza na ya Tanzania ziliingia katika mvutano.
BAE Systems ni kampuni kubwa ya uuzaji wa vifaa vya ulinzi ambayo iwapo ingefungiwa kufanya biashara yake kungekuwa na athari kubwa kwa Uingereza.
Suala la uchunguzi wa aina yoyote ambao ungemweka matatani Rais wa zamani, Benjamin Mkapa na washirika wake wa karibu (kwa mujibu wa Wikileaks) lilikuwa ni gumu kuweza kufanyika.
Ulisema baada ya kumalizika kwa kipindi cha ukimya bila kushughulikiwa kwa kashfa hiyo, suala la kutafuta ufumbuzi lilionekana kuwa muhimu kwa nchi zote mbili, lakini kasoro kubwa ni pale kila aliyehusika katika kashfa hiyo ya BAE nchini Uingereza na Tanzania kukwepa kuchunguzwa.
Hata hivyo, aliyekuwa Waziri Mkuu, Tonny Blair alifanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba SFO wanafanya uchunguzi na kama ikiwezekana BAE ifungiwe kufanya kazi katika nchi za Umoja wa Ulaya.
Kwa upande wake, Tanzania ilikuwa ikilaumiwa kwa kufanya juhudi za kutetea ununuzi huo na hata kumtisha Mkurugenzi wa Takukuru kumtaka aachane na suala hilo.
Dk Hosseah
Jana Dk Hosea hakupatikana kuzungumzia taarifa hiyo, lakini akizungumzia tuhuma za kufichua siri ya Rais Kikwete kupitia mtandao huo Desemba 20 mwaka jana, alikiri kupata vitisho vinavyohatarisha maisha yake kutokana na mapambano yake dhidi ya rushwa.
Dk Hoseah alisema hayo alipotakiwa kuzungumzia madai ya mtandao huo wa Wikileaks kuhusu kauli yake na Afisa wa Ubalozi wa Marekani kwamba kiongozi huyo wa nchi, asingependa vigogo Serikalini kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.
Mtandao huo pia ulidai kuwa mkuu huyo wa Takukuru ameshindwa kuwafikisha mahakamani vigogo waliohusika na kashfa ya rada kwa sababu anahofia usalama wake.
Mbali na hofu hiyo, mtandao huo ulieleza kuwa Dk Hoseah alipewa maelekezo maalumu na Rais Kikwete kutoshughulikia kesi za rushwa zinazowahusu vigogo katika Serikali yake na hasa marais waliomtangulia.
The Guardian lilitoa taarifa hiyo likiunukuu mtandao wa habari wa WikiLeaks uliojizolea umaarufu duniani kwa kutoa habari za kiuchunguzi hasa baada ya mwasisi wake, Julian Paul Assange, kutiwa matatani
Akijibu hoja hizo mwaka jana, Dk Hoseah alisema ni kawaida kwake kukutana na mabalozi wa nchi mbalimbali kila mwaka na kujadiliana nao mambo mengi kuhusu Tanzania, lakini hakumbuki kuzungumza naye mambo hayo.
Alisema mabalozi ni wadau wakubwa katika bajeti ya Tanzania na hivyo huwa wanakutana kila mwaka kujadili mambo mbalimbali ya kuhusu kusaidia bajeti ya Serikali.
“Mimi huwa nakutana na mabalozi wa nchi mbalimbali kwa sababu wao ni wadau katika mradi wa ‘government budget support’ (Mpango wa kusaidia bajeti ya Serikali), hivyo hilo sio tatizo,” alisema Dk Hoseah.
“Msimamo wangu ni kwamba mapambao dhidi ya ufisadi ni endelevu hadi hapo tutakapofanikiwa kumaliza tatizo hili,” alisema Dk Hosea na kukiri:
“Vitisho vipo vingi tu, kutoka kwa watu wanaotuhumiwa, lakini si hata ninyi waandishi mnamwagiwa ‘tindikali’ katika mapambano yenu, hivyo hivyo hata mimi napata vitisho.”
Alisisitiza kuwa pamoja na vitisho hivyo, hawezi kurudi nyuma katika mapambano ya rushwa na ufisadi.
“I’m a Tanzanian, I will die in Tanzania, it is my country’ (mimi ni Mtanzania, nitakufa Tanzania, ni nchi yangu), siwezi kuhama nchi kwa vitisho vya watu wachache wanaotuhumiwa kwa ufisadi na rushwa,” alisisitiza Dk Hoseah.
“Hilo la kwamba nafikiria kuhama nchi wametia chumvi si unajua magazeti? Sijafikiria kuhama nchi licha ya vitisho, mimi naona ni changamoto na jambo la kawaida katika mapambano,” aliongeza Dk Hoseah.
Kuhusu Rais Kikwete kukwamisha mapambano ya ufisadi kama alivyonukuliwa na gazeti hilo la The Guardian, Dk Hoseah alipiga chenga kulijibu badala yake akaeleza:
“Ili umpeleke mtu mahakamani si lazima umtuhumu na kumfanyia uchunguzi? Lakini pia lazima tujenge utamaduni wa kuwaheshimu viongozi wetu.”
Siku hiyo, Takukuru ilituma taarifa iliyoeleza kuwa Dk Hoseah alishangazwa na Ofisa wa Ubalozi wa Marekani kumnukuu vibaya huku akisema hajui ana lengo gani.
Katika taarifa hiyo, Dk Hoseah alikiri kukutana na ofisa huyo wa Ubalozi wa Marekani ofisini kwake Julai mwaka 2007, lakini akasema ripoti ya mazungumzo yao aliyoipeleka nchini kwake imechakachuliwa.
“Kwa mfano haikutokea katika mazungumzo yetu kusema kwamba Rais Jakaya Kikwete hakutaka kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake, kuwashitaki vigogo wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi kama ilivyodaiwa na Ubalozi wa Marekani,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na idara ya mahusiano ya Takukuru.
“Nilichosema ni kwamba Rais hayuko tayari kuruhusu kushitakiwa kwa vigogo wa Serikali au mtu mwengine yeyote kwa tuhuma za uvumi au kwa ushahidi dhaifu, kwa sababu kufanya hivyo, Serikali itakuwa hatarini kwa kulipa gharama kubwa ya fidia ikiwa mtuhumiwa huyo atashinda kesi mahakamani,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza.
Kuhusu hofu ya maisha yangu, nakumbuka niliulizwa na Ubalozi wa Marekani kwamba je, naogopea maisha yangu au la, nikiwa Mkuu wa Takukuru? Na jibu langu lilikuwa rahisi kwamba ‘bila ya shaka’ unapopambana na wakubwa na matajiri kama hao wanaotuhumiwa unapaswa kuwa makini na maisha yako.
Lakini hata siku moja sikusema kwamba napanga kuhama nchi kwa sababu maisha yangu yapo hatarini. Ni mshangao kuona kwa mara nyengine ofisa wa Ubalozi wa Marekani ananinukuu mimi vibaya au nje ya mada na sielewi kabisa lengo lao lilikuwa nini.”
Alsema rekodi yake, akiwa Mkuu wa Takukuru iko wazi kabisa wakati wowote anapokuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa yeyote wa ufisadi hawaogopi lolote isipokuwa ni kumburuza mahakamani bila ya kujali cheo chake.
Bunge la Uingereza
Taarifa ya mtandao huo imekuja siku moja tangu Bunge la Uingereza liitake Serikali ya Tanzania kuwafikisha mahakamani watu wote walioshiriki mchakato wa ununuzi wa rada na kuingiza nchi katika hasara ya mabilioni ya fedha.
Kupitia kamati yake ya Maendeleo ya Kimataifa, Bunge hilo lilisema lingependa kuona watu wote walioshiriki kwenye mchakato wa ununuzi wa rada hiyo, wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ufisadi.
Taarifa ya kamati hiyo iliyonukuliwa juzi na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), ilieleza kuwa wajumbe wake ambao ni wabunge kutoka vyama mbalimbali, watatoa ushirikiano wa dhati kwa Tanzania iwapo itaamua kuwashtaki watuhumiwa hao nchini Tanzania au Uingereza.
Wito huo wa wabunge wa Uingereza umekuja wakati tayari Kampuni ya BAE System, iliyoiuzia Tanzania rada hiyo, ikikubali kuwa kulikuwa na kasoro katika mchakato wa ununuzi wa rada hiyo na hivyo kuirudishia Tanzania Dola za Marekani 46 milioni kama fidia.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Siri zafichuka ufisadi wa rada
0 comments