Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Ofisa wanyamapori jela miaka 20

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAHAKAMA ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara imemhukumu Ofisa Wanyamapori Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Nyagabona Mayoba kwenda jela miaka 20 kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na ujangili.


Hata hivyo mahakama hiyo iliwaachia huru washtakiwa watano walioshtakiwa pamoja na Mayoba baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani.


Pamoja na hukumu hiyo, mahakama hiyo pia imeamru magari mawili yaliyohusika katika uhalifu huo aina ya Landrover Defender na Toyota Hillux mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu yataifishwe na kutumika na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kudhibiti ujangili ikieleza kuwa inaonekana mmliki wake wa awali hajui matumizi yake.


Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takribani saa mbili, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Joachim Tiganga alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka uliomtia hatiani mshtakiwa huyo huku ukikosa nguvu za kuwatia hatiani washtakiwa wengine watano.


Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Tobi, Ramadhan Mhela, Harold John, Enyamba Manyama na Stephen Ngoga ambao wameachiwa huru.


Washtakiwa hao kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuingia eneo la hifadhi bila kibali na kuua wanyama mbalimbali wenye thamani ya zaidi ya Sh5 milioni bila idhini ya mamlaka husika, kutumia magari ya Serikali katika kutekeleza uhalifu na kumiliki silaha kinyume cha sheria ambapo hakimu huyo alisema ushahidi umewaondoa washtakiwa wengine hatiani baada ya kuthibitika kuwa waliamurishwa kufanya hivyo na Mayoba.


Hakimu Mkazi Tiganga alisema kuwa mahakama hiyo imeamua kumpa adhabu hiyo mshtakiwa Mayoba aliyejitetea kuwa anasumbuliwa na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kiafya na kifamilia ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wasio waaminifu ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao kuhujumu utajiri tulionao wa wanyama pori na hivyo kulikosesha taifa mapato.


Mapema, mwendesha mashtaka wa kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya magharibi, Protas Longoma aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa akisema ameisononesha na kuiabisha Serikali na Wizara ya Maliasili na Utalii iliyompa dhamana ya kushiriki kikamilifu katika kulinda wanyamapori ambao ni rasilimali ya taifa kwa ajili ya uchumi wa taifa badala yake amegeuka jangili anayeuwa wanyama kiholela.

0 comments

Post a Comment