Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mkulo: Sijui mzigo wa CAG ni upi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZIRI wa Fedha, Mustafa Mkulo amesema hajui Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeelemewa kwa kiasi gani na fasheni iliyoibuka ya ukaguzi maalumu.


Mkulo alisema hayo jana alipokuwa akizungumzia kauli ya CAG, Ludovick Utouh kuhusu
tatizo hilo kuchangia kupungua kwa tija katika ukaguzi.


Mwishoni mwa wiki, Utouh alionya kuwa endapo watendaji wanaosababisha uwepo wa
ukaguzi maalumu hawatadhibitiwa mapema, ukaguzi wa hesabu hautakuwa na tija kwa taifa.


Alilalamikia kuelemewa na shughuli za ukaguzi maalumu zinazoongezeka katika ofisi yake kila kukicha.


Akifafanua suala hilo, Mkulo alisema wanatambua matatizo yaliyopo kwenye Serikali za Mitaa, ingawa hafahamu kwa sasa ni kwa kiasi gani CAG ameelemewa akimaanisha idadi ya ukaguzi maalumu alionao sasa.


“Kuna ukaguzi maalumu ambao hauwezi kuepukika kama ule wa Jairo (Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini). Sasa kwa ukaguzi maalumu kutokana na miradi kutosimamiwa vizuri katika Serikali za Mitaa bado sijajua ameelemewa kiasi gani, ingawa tunajua kuna tatizo katika ngazi hiyo,” alisema Mkulo.


Alifafanua kuwa Serikali imemteua Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Hesabu za Ndani kwa ajili ya kumsaidia CAG.


Mkulo alisema pia wamemteua Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani ya Serikali za Mitaa atakayewajibika kufanya ukaguzi wa hesabu za wakaguzi wote wa ndani katika halmashauri,
kabla ya CAG kuzifikia.


“Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za ndani katika Serikali za Mitaa ndiye atakayepaswa kupokea ripoti za wakaguzi wengine kwenye Halmashauri na kuwasilisha ripoti yake kwa Mlipaji
Mkuu wa Serikali atakayewasilisha ripoti hiyo kwa Katibu Mkuu wa Hazina,” alisema.


Alifafanua kuwa lengo la kufanya uteuzi huo ni kuimarisha mfumo wa usimamizi wa hesabu ndani ya Serikali za Mitaa kwa kubaini kasoro mbalimbali za kimahesabu kabla ya CAG kuzifikia.


“Hii ni njia moja ya hatua inayoweza kusaidia kupunguza mzigo wa kazi kwa CAG na ni fursa pia kwa Serikali za Mitaa kugundua makosa yao mapema na kuyarekebisha bila kusababisha hasara kwa Serikali.


“Ukaguzi huo utakuwa ukifanyika kila miezi mitatu ili kuondoa uwezekano wa kujificha kwa kasoro zozote kwa kuwa kutakuwa na mwanya wa kugundua tatizo kama lipo mapema na kulirekebisha,” alifafanua.


Alisema anaamini hiyo ni njia bora itakayopunguza ubadhirifu na matumizi mengine yasiyostahili ya fedha za Serikali.

0 comments

Post a Comment