Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Lowassa, Sumaye wabwatuka CCM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WALIA KUCHAFULIWA NA MAKADA WENZAO,NEC YARIDHIA GAMBA KUREJESHWA CC


MAWAZIRI Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, jana walishambulia kwa maneno makali wajumbe wawili wa Sekretarieti ya CCM kwamba wamekuwa wakikivuruga chama na kusababisha mgawanyiko uliopo.Lowassa aliyejiuzulu Uwaziri Mkuu, kutokana na kashfa ya Richmond ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo wakati wa mjadala wa hali ya siasa, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichomazika jana mjini Dodoma.


Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Lowassa alianza kubwaga moyo wake baada ya NEC kuridhia ombi la Kamati Kuu ya chama hicho (CC) kwamba suala la mageuzi ndani ya CCM maarufu kama kujivua gamba lirejeshwe katika kamati hiyo ili lifanyiwe kazi kwa taratibu za kawaida za kinidhamu baada ya wahusika kukataa kuachia nafasi zao.


“Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama wakinitukana, hivi hatukujua kwamba kuna kamati hizo za maadili,”Lowassa alinukuliwa akihoji.


Lowassa alinukuliwa akiwataja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, John Chiligati kwamba wamekuwa wakitukana watu ovyo kwa fedha wanazopewa na CCM.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lowassa alitumia dakika saba kumshambulia Nape kwamba amekuwa akifanya mambo nje ya utaratibu na kwamba mwenendo huo umekuwa ukikibomoa chama badala ya kukijenga.


Baada ya maneno ya Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Sumaye alisimama na kuhoji sababu za chama hicho kunyamazia ukiukwaji wa taratibu ambao umekuwa ukifanywa na watendaji hao.


“Mwenyekiti huyu bwana (Lowassa) amesema kwamba amechafuliwa kwa miezi saba, sasa kama leo tunasema kwamba tunarudi kwenye utaratibu wa kamati za maadili, hao waliomchafua watafanywaje?”Sumaye alinukuliwa akihoji.
Hata hivyo, taarifa za ndani ya kikao hicho zilimnukuu Kikwete akisema kwamba viongozi hao watakuchukuliwa hatua za kinidhamu kama watakuwa wamefanya hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliwasihi wajumbe kuachana na suala hilo na badala yake kuchangia maeneo mengine ya taarifa hiyo ya hali ya siasa iliyowasilishwa na Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje ya CCM, January Makamba.


Kikwete alinukuliwa akihitimisha hoja hiyo kwa kusema kwamba: “Jamani hapa tunajenga chama, watu wanasubiri kusikia tukimaliza kikao chetu kwa ugomvi, naomba tumalize kwa amani na twendeni tukajenge chama chetu”.


Richmond yatajwa
Vyanzo vyetu vilimnukuu Lowassa akizungumzia suala la Kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond kwamba yeye aliamua kuvunja mkataba baina ya kampuni hiyo, lakini Rais KIkwete alimwambia subiri baada ya kuwa amepata ushauri wa Makatibu Wakuu.


Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), alinukuliwa akisema: “Mwenyekiti utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema, lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo hii ninahukumiwa nakuitwa fisadi kwanini?”.


“Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda Serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wana CCM wenzangu na siyo wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?,”alinukuliwa akihoji Lowassa.


Kadhalika kada huyo wa CCM alinukuliwa akimkumbusha Rais Kikwete kwamba: “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina Mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina Mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo”.


Lowassa alisema kama alivyozungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa walipokutana jijini Dar es Salaam, tatizo kubwa analolifahamu la vita ya sasa ni urais wa 2015.


“Mwenyekiti nikukumbushe jambo jingine, kule Zanzibar mwaka 1997 walipoleta tuhuma za mtizamo wa umma dhidi yako, ulisema kwamba kuwa Rais ni mipango ya Mungu,”alinukuliwa Lowassa katika maelezo yake ndani ya NEC


Alisema kwa kuzingatia mazingira hayo, hii leo si sahihi hata yeye (Lowassa) kuhukumiwa kwa kuzingatia kile kinachodaiwa kuwa ni mtizamo wa umma dhidi yake unaompa sura ya ufisadi, jambo ambalo alidai kwamba siyo la kweli.
Baada ya Lowassa na Sumaye kuongoa, kada maarufu wa chama hicho, Kingunge Ngombale Mwiru alisimama akitaka kuongelea dhana ya gamba ndipo Mkapa alipomshtua Kikwete kwamba hoja hiyo ifikie mwisho.
Baadhi ya wajumbe waliiambia Mwananchi kwamba wakati Lowassa akiongea Mkapa alionekana kufurahi.


Kujivua gamba
Kufuatia uamuzi huo wa NEC hivi sasa mpango wa kujivua gamba ulioasisiwa na chama hicho, Aprili mwaka huu unarejeshwa CC ambapo watuhumiwa wote wa makosa mbalimbali watafikishwa mbele ya Kamati za maadili na kuchukuliwa hatua kwa taratibu za chama hicho.


Mpango wa kujivua gamba ulilenga kuwashinikiza watuhumiwa wa ufisadi kuachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama hicho na sasa unarejeshwa Kamati Kuu (CC) ili ichukue hatua zaidi kwa wale waliogoma kujiuzulu.


Hatua hiyo inatokana na kuwapo ukimya ambao unaashiria kutokuwapo viongozi na makada ambao wako tayari kujiuzulu nyadhifa zao kwa hiari yao kama ilivyotarajiwa.


Tangu kupitishwa kwa mpango huo maarufu kwa jina la kujivua gamba katika kikao cha NEC kilichopita cha Aprili mwaka huu, ni kada mmoja tu, Rostam Aziz aliyechukua hatua za kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Igunga na ujumbe wa NEC, lakini wengine wamekuwa kimya hadi sasa.


Katika kikao cha Aprili NEC hiyo ya CCM ilipitisha maazimio 26, lakini kubwa ni lile lililokuwa likihimiza vita dhidi ya ufisadi kuendelea na kutoa mwito kwa watu wanaotajwa na jamii kuhusika na ufisadi ambao wako ndani ya chama kujitathmini kisha kuchukua hatua za kuachia madaraka waliyonayo.


Sehemu ya mwisho ya azimio hilo inasomeka: “Wasipoachia madaraka chama kiwachukulie hatua mara moja”.


Mmoja wa wajumbe wa CC ambaye ameomba jina lake kuhifadhiwa alisema: “Tunawaomba NEC waturuhusu jambo hili tulifanyie kazi sisi (CC) na litafanyiwa kazi kupitia taratibu za kawaida za chama kwa kuzingatia kanuni na taratibu za maadili za chama hicho”.


Nec yawakaanga kina Jairo
Katika hatua nyingine, NEC imeunga mkono hatua zilizopendekezwa na Bunge dhidi ya watumishi wa umma waliotajwa katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyoanika uozo wa matumizi mabaya ya fedha za Umma ndani ya Wizara ya Nishati na Madini.


Kamati hiyo katika ripoti yake iliyowasilishwa mwishoni mwa Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma, iliwataja Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini (aliyesimamishwa), David Jairo na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kwamba wanastahili kuchukuliwa hatua.


Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, huku wabunge wakipendekeza pia kuondolewa madarakani kwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Adam Malima.

0 comments

Post a Comment