Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO , HABARI ZA MICHEZO - Kili Stars kufungua naRwanda chalenji

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
TIMU ya Taifa (Taifa Stars), imepangwa katika kundi linaloonekana kuwa gumu kuliko mengine kwa kukutanishwa na Ethiopia, Rwanda na Djbouti katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Chalenji, linalotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 25, mwaka huu, Dar es Salaam.
Ugumu unaonekana kuwepo katika kundi hilo ni kutokana na Taifa Stars ndio iliyotwaa ubingwa huo na kwamba haitakubali kutolewa mapema, Ethiopia ilitinga hadi nusu fainali na Rwanda ilitinga robo fainali na kutolewa na Stars katika hatua hiyo.


Pamoja na timu hizo kuonekana ndio tishio katika kundi hilo, Djibouti yenyewe inaonekana kuwa timu dhaifu lakini inaweza kuonesha maajabu kama ilivyokuwa kwa Somalia mwaka jana kwa kucheza soka safi licha ya kuishia katika hatua ya makundi.


Mbali na hilo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), imezitoa timu za Ivory Coast, Zambia na Botswana kushiriki katika michuano hiyo kutokana na katiba ya shirikisho hilo kuzibana timu hizo.


Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza makundi hayo, Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye alisema wameamua kutaja makundi hayo kwanza ambapo Jumamosi watatoa ratiba kamili.


"Kundi A litakuwa na mabingwa watetezi, Tanzania (Taifa Stars), Rwanda, Ethiopia na Djobouti, Kundi B lina timu za Uganda, Burundi, Zanzibar na Somalia na Kundi C ambalo ni la mwisho lina timu za Sudan, Kenya, Eritrea na Malawi ambayo imealikwa," alisema Musonye.


Alisema awali walipokea maombi mbalimbali kutoka kwa nchi zingine kama Nigeria, Cameroon, Ivory Coast, Botswana na Zambia na walikuwa wanaendelea kufanya nazo mazungumzo ya kuwemo katika mashindano hayo, lakini kanuni za CAF haziruhusu kwa wakati huu.


Akifafanua zaidi suala hilo, Musonye alisema kanuni ya tatu ya CAF inaeleza kwamba timu ambazo zimefuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN), haziruhusiwi kushiriki mashindano yoyote ikiwa imebaki miezi miwili kabla ya mashindano yao kuanza.


Alisema kutokana na hilo ndio maana baadhi ya timu imekuwa ngumu kuzipata na kuamua kuialika Malawi ambayo tangu awali ilionekana kuhitaji kushiriki katika mashindano hayo.


Wakati huohuo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Leodegar Tenga alisema bado wanahaha kutafuta sh. milioni 600 kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo kwani bajeti nzima ya mashindano ni sh. bilioni 1.4.


"Tuna tundu la sh. milioni 600 ili kufanikisha mashindano hayo, hivyo hatuna budi kutafuta wadau wengine kuhakikisha wanatusaidia kuzipata hizo fedha na si kuwaachia Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ambao ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo," alisema Tenga.

0 comments

Post a Comment