IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
*Wabunge walia na Lissu, wahoji usomi wake
*Waionya serikali kutochukua hatua mapema
*Mnyika: Kikao cha Kamati Kuu kukutana kesho
SIKU moja baada ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na NCCR-Mageuzi, kususia mjadala wa
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi huo unadaiwa kutokuwa na tija kwa Watanzania badala yake unalenga kuwapotosha.
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliyasema hayo Bungeni mjini Dodoma jana wakati wakichangia mjadala huo na kudai kuwa, Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tindu Lissu (CHADEMA), anatumia vibaya usomi wake kupotosha Watanzania.
Walisema maoni yaliyowasilishwa bungeni na Bw. Lissu ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Sheria na Katiba, yalilenga kupotosha Watanzania na kulichafua jina la Muasisi wa Muungano, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mbunge wa Simanjiro, mkoani Manyara, Bw. Christopher Ole Sendeka (CCM ), alisema Bw. Lissu ameshindwa kutumia vyema usomi wake kuelimisha Watanzania badala yake anajenga hoja za kuwagawa jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa.
“Kwa mara ya kwanza namsikia msomi anayejiita mwanasheria kupitia hotuba yake akimkashifu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na kudai alimomonyoa uhuru hii haiwezekani, naomba arudi tena darasani kwani usomi wake bado haujamsaidia, inakuweje anamtuhumu Baba wa Taifa na kuwapotosha Watanzania,” alisema.
Bw. Sendeka alisema elimu aliyonayo Bw. Lissu, haijamsaidia hivyo anapaswa kupatiwa mafunzo ya ziada ili yaweze kumkomboa kifikra.
“Katika hili tupo tayari kumpatia mafunzo ya ziada, tutamfundisha bure bila gharama yoyote, Watanzania mnapaswa kutambua kuwa, kinachojadiliwa hapa si uidhinishwaji wa Katiba Mpya kama wanavyopotoshwa bali ni mchakato wa kupata maoni ya kuunda tume huru ambayo itakusanya maoni ya wananchi kuunda Katiba Mpya,” alisema Bw. Sendeka.
Mbunge wa Wawi, Bw. Hamad Mohamed Rashid (CUF), alisema inasikitisha mbunge anapokula kiapo cha kuitumikia na kuiheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini anatumia nafasi hiyo kupotosha umma hali ambayo inaweza kuleta vurugu.
“Ukisoma katika muswada huu, kuanzia kipengele cha kwanza hadi hitimisho, hakuna sehemu inayoeleza kwamba nchi yetu inatawaliwa kwa misingi ya kidikteta wala ufalme, jana (juzi), Bw. Lissu wakati akiwasilisha hotuba yake, alipotosha Watanzania...hii ni hatari.
“Ukisoma ukurasa wa 20 wa hotuba ya Bw. Lissu, sisi wabunge tunaambiwa hatuna mawazo...hii ni aibu kubwa, dharau hizi hatuzitaki mimi Rashid nimekaa katika bunge hili muda mrefu, haijawahi kutokea hali kama hii,” alisema Bw. Rashid.
Aliongeza kuwa, kinachofanyika kwa sasa si kupitisha katiba mpya, bali ni mchakato wa kuunda tume ya kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kuandika katiba.
Alisema haiwezekani Tanzania igawanyike vipande kwa sababu ya ya watu fulani bali katika hatua ya kupiga kura, tume zote za uchaguzi zishiriki kuandaa vitengo vyao ili kila mwananchi aweze kushiriki kupiga kura.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Wabunge wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, amesema baada ya kutafakari, wabunge wa chama hicho kwa pamoja wamefikia uamuzi wa kuitisha Kikao cha Kamati Kuu cha dharura ambacho kitafanyika kesho na kutoa mwelekeo wao juu ya muswada huo.
“Msingi wa kikao hiki ni kutoa mwelekeo jinsi muswada huu ulivyokaa vibaya kwa wananchi kwani haujawatendea haki ya kuwasilisha maoni yao kama wanavyotaka,” alisema.
Alisema chama hicho kinatambua kuwa, muswada huo ulipowasilishwa bungeni ulitoka kwa mara ya kwanza si kwa mara ya pili kama ulivyowasilishwa na Waziri mwenye dhamana.
Katika hatua nyingine, wabunge hao walienda mbali zaidi na kuionya Serikali kuchukua hatua mapema dhidi ya vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani na uhamasishaji wananchi kushiriki vurugu kinyume na sheria za nchi kwani machafuko yaliyotokea nchi za Rwanda na Burundi yalianza kwa kauli kama zinavyotolewa na viongozi wa CHADEMA.
“Mimi naona hawa wana lao, tena nia yao ni mbaya, nchi ya Rwanda na Burundi, walianza hivi hivi, hapa lazima Serikali ichukue hatua,” alisema Mbunge wa Kibakwe, Bw. George Simbachawene.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Chadema wateka Bunge
0 comments