Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Katibu wa CCM Dar es Salaam ‘afyekwa’

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemvua uongozi Katibu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe
Ng'enda kwa kosa la kwenda kinyume na uamuzi halali wa vikao vya Chama wakati wa uchaguzi
wa madiwani wa viti maalumu wa mkoa huo.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye alisema jana kuwa kikao cha NEC kilichokuwa kikifanyika kwa siku ya pili jana, ndicho kilichotoa uamuzi huo na Ng'enda atapangiwa kazi nyingine.


Mbali na kuvuliwa uongozi kwa Ng'enda, Nape alisema pia NEC imepanga ratiba ya ndani ya kumpata mgombea wa CCM ya Mwakilishi wa Uzini baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.


Kwa mujibu wa ratiba hiyo inayohusisha pia vikao vya chama hicho, wanachama wa CCM wataanza kuchukua na kurejesha fomu kuanzia Novemba 28 mpaka Desemba 2.


Kuanzia Desemba 3 mpaka 10, kutafanyika kampeni za wagombea wa chama hicho katika ngazi ya matawi.


Ratiba hiyo imeonesha kuwa siku ya kupiga kura kumchagua mgombea wa CCM ni Desemba 11 na baada ya hapo Kamati ya Usalama na Maadili itakaa Desemba 13.


Baada ya Kamati hiyo, itafuatiwa na kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya Desemba 14, Kamati ya Siasa ya Mkoa Desemba 17, Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya NEC Desemba 20 mwaka huu na kufuatiwa na Kamati Maalumu ya NEC, Desemba 24.


Sekretarieti ya NEC itakutana Januari 4 na 5 na Kamati Kuu ya CCM kumthibitisha mgombea huyo itakaa Januari 7 na 8.


Wachunguzi wa masuala ya siasa ndani ya CCM wanabaini kuwa uamuzi huo umejikita zaidi katika sintofahamu iliyotokea Dar es Salaam kuhusiana na uchaguzi wa wabunge wa madiwani wa viti maalumu na kuzusha lawama kutoka kwa Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan dhidi ya
Ng’enda.


Mgogoro huo ulifikia Azzan kupewa adhabu ya kufungiwa kugombea nafasi yoyote katika chama hicho na kujihusisha kwa namna moja ama nyingine katika masuala ya uongozi.


Hata hivyo baadhi ya wanachama wa CCM wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam walijitosa katika sakata hilo wakiitaka Kamati Kuu ya CCM Taifa (CC), kuingilia kati na kutengua adhabu dhidi ya Azzan.


Wanachama hao pia walimtaka Ng’enda na sekretarieti ya siasa ya mkoa huo kuwajibika kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.


Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ilala, Jumanne Kolekole, alikaririwa wakati mmoja akisema mazingira ya uendeshaji wa shughuli za CCM Dar es Salaam, yanawafanya baadhi ya wana-CCM kujiona kama wanatengwa kutokana na kushindwa kwa viongozi wa mkoa na hasa Katibu wake, kuwashirikisha katika uamuzi wenye maslahi.


“Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wamekuwa wabinafsi na wenye kuona nafasi zao ni kama mamlaka isiyohitaji kuhojiwa na mtu au mwanachama mwingine yeyote na ndiyo maana hata wakishauriwa jambo wanakuwa wakali na kuchukua hatua zikionesha chuki,” alipata kusema
Kolekole.


“Mimi nadhani CCM Mkoa wa Dar es Salaam hauna viongozi wazuri, hawa akina Kilumbe na John Guninita (Mwenyekiti wa Mkoa) ni aina ya watu walioshindwa kazi na ambao kinachowafanya kuendelea na uongozi ni siasa za mazoea, na huyu ni mwenzetu na wala hawana sifa za uongozi,” alisema mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mangundala.


Alisema wanaCCM Wilaya ya Ilala wanaunga mkono kauli ya Mbunge Azzan ya kutaka viongozi wa mkoa na kwa kuanzia katika sekretarieti ya mkoa kuwajibika na kujivua gamba.


Wilayani Temeke, wana-CCM wa kata za Yombo Makangarawe, Keko, Temeke, Kurasini alisema kilichofanywa na Kamati ya Kilumbe kilitokana na hasira ya kuelezwa ukweli ambao viongozi wengi hawataki kuusikia.


Hata hivyo, Kilumbe na Guninita walikaririwa wakijibu kwa kusema wanakiachia chama kuchukua uamuzi na ikiwa itabainika wamekosea kuchukua hatua watalazimika kuwajibika.


Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete leo atafungua semina ya watendaji wa chama hicho wa ngazi ya Taifa hadi wilaya yenye lengo la kufanikisha utendaji wa ndani ya chama.


Nape alisema semina hiyo itafanyika kwa siku tatu mpaka keshokutwa na itashirikisha wajumbe wa Sekretarieti ya NEC na Sekretarieti ya jumuiya za CCM na makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya zote nchini.


Wakati huo huo, Nape amesema taarifa rasmi kuhusiana na maamuzi mengine ya kikao hicho ambayo yanasubiriwa kwa hamu na Watanzania yatatolewa leo.

1 comments

  1. Kiongozi bora ni yule ambaye anafuata maadili na katiba cha Chama Chake.
    Kwa viongozi wote mnabidi tufuate katiba zetu zinavyosema na tuheshimiane Jamani!

Post a Comment