Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - JK akutana na Chadema, wakubaliana

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Baadhi ya viongozi wa Chadema wakiingia Ikulu jijini Dar es Salaam leo jioni.
Mhe. Rais Kiketwe akisalimiana na Mwenyekiti wa Chadema, Mhe. Freeman Mboe mara baada ya kuingia Ikulu.
Mhe. William Lukuvi akisalimiana na Mhe. Tundu Lissu.
Mhe. Mbowe akiongea na Mhe. Rais.
...safu ya viongozi wa Chadema ikiongea na Rais.
Mhe. Rais akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chadema mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu mapema leo.

RAIS Jakaya Kikwete na ujumbe wa Serikali yake, jana amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kuwahakikishia viongozi wa chama hicho kuwa yeye na Serikali yake, wana dhamira ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.


Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana jioni, katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, yamefanyika katika mazingira ya urafiki na ujumbe wa Chadema umewasilisha mapendekezo yake kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Tanzania.


Serikali imepokea mapendekezo hayo, ilieleza taarifa ya Ikulu. Hata hivyo, pande zote mbili zimekubaliana kukutana tena leo asubuhi ili kuipa nafasi Serikali iweze kutafakari mapendekezo hayo.


Kwa mujibu wa Ikulu, lakini pande hizo mbili zimekubaliana kuwa Katiba ya sasa ni Katiba nzuri iliyolilea Taifa kwa miaka 50 iliyopita kwa sababu ni Katiba ya sasa iliyoliwezesha Taifa la Tanzania kuwa na amani, utulivu na kupata maendeleo makubwa ambayo nchi yetu imepata mpaka sasa.


“Pia pande zote mbili zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kutunga Katiba mpya kama Mheshimiwa Rais Kikwete alivyoliahidi taifa wakati wa salamu zake za Mwaka Mpya Desemba 31, mwaka jana, 2010, Katiba ambayo italiongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mingine 50 ijayo,” ilieleza taarifa hiyo.


Katika mazungumzo hayo, Rais aliwahakikishia wajumbe hao wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwa ni dhamira yake na ya Serikali yake kuhakikisha kuwa Tanzania inapata Katiba mpya.


Aidha, pande zote mbili zimekubaliana kuwa ni jambo muhimu kwa mchakato mzima wa kutungwa kwa Katiba mpya kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani, utulivu na umoja wa kitaifa.


Aidha, pande zote mbili zimekubaliana kuwa mchakato huo uendeshwe kwa kuzingatia misingi ya mambo mengine muhimu kwa Taifa la Tanzania kama vile kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, kuligawa Taifa kwa misingi ya udini na ukabila ama kutugawa kwa misingi ya maeneo.


Mkutano huo umefanyika baada ya kuombwa na viongozi wa Chadema ambao Jumatatu iliyopita kupitia kwa Mbowe, walitoa maazimio ya Kamati Kuu ya Chama hicho, mojawapo likiwa ni kuunda Kamati ndogo ya kwenda kumwona Rais Kikwete kumweleza msimamo wao kuhusu mchakato wa Katiba mpya.


Mbowe alisema hatua hiyo imetokana na kutoridhika na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge, bila ushiriki wa wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi, waliosusa na kutoka nje.


Miongoni mwa madai yaliyosababisha wasusie mjadala huo ni kuwa Muswada ulikuwa na upungufu na marekebisho mengi yaliyosababisha wao kuona ni bora usomwe mara ya kwanza na kurudi kwa wadau wakiwamo wananchi ili watoe maoni kabla ya kusomwa mara ya pili.


Muswada huo uliotolewa kwa Hati ya Dharura, ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Aprili na kupelekwa kwa wadau na kufanyiwa marekebisho kadhaa ikiwemo kuuweka katika lugha ya Kiswahili na kisha kusomwa kwa mara ya pili katika Bunge lililomalizika Ijumaa ulipitishwa na
kusubiri kusainiwa na Rais ili kuwa sheria.


Wajumbe wa Kamati hiyo ya watu saba ni viongozi wa juu wa Chadema na baadhi ya wabunge wa chama hicho wakiongozwa na Mbowe (Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni), Makamu Mwenyekiti Bara na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi na Makamu Mwenyekiti Zanzibar na Said Issa Mohammed.


Wamo pia Katibu Mkuu, Dk. Slaa, Mwanasheria wa Chama na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, wajumbe wawili wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari.

0 comments

Post a Comment