Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Dodoma leo, NI KETE YA MWISHO YA SITTA, LOWASSA, CHENGE, NAPE

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MATUMBO ya vigogo na wapambe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi sasa yapo moto baada ya kuvuja kwa mpango wa kuwang’oa baadhi ya makada wanaodaiwa kuvuruga amani na mshikamano ndani ya chama hicho.


Wanaowindwa katika mpango huo ni pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Katibu wa itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.


Lowassa na Chenge wanashutumiwa kwa ufisadi na kukataa kujiondoa kwenye nafasi zao baada ya kupewa muda wa kufanya hivyo; huku Sitta na Nape wanashutumiwa kwa kupalilia migawanyiko na makundi hasimu ndani ya chama na serikali.


Baadhi ya taarifa zinasema miongoni mwa hao, wapo watakaofukuzwa chama, huku wengine wakondolewa ili kupewa nyadhifa nyingine za kiserikali. Hata hivyo, taarifa za ndani zinasema Chenge na Lowassa wamejiandaa “kufa kidume” iwapo watagundua kuna mpango wa kuwatimua.


Vyanzo vya habari kutoka ndani ya CCM vinasema Lowassa na Chenge wanakaribia “kuishiwa uvumilivu,” hasa watakapogundua kuwa wenzao wana mpango mchafu dhidi yao; na kwamba iwapo wataamua kuvunja kimya na kujipigania, CCM inaweza kugawanyika vipande vipande, kwani ufisadi wanaotuhumiwa nao umeshonwa ndani ya mfumo, na unawahusu watawala na makada wengine waandamizi.


Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kitakachokutana kuanzia keshokutwa mkoani Dodoma chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete ndicho kitakachotoa uamuzi wa ama kuwang’oa madarakani viongozi hao au kuwapa onyo.


Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa kamati ya maadili ambayo ilifanya kikao chake juzi iliweka wazi kuwa chama hicho kinapaswa kuwachukulia hatua vigogo wake ili kutuliza upepo mbaya unaovuma ndani ya chama hicho katika miaka ya hivi karibuni.


Chanzo cha habari kutoka ndani ya CCM kimelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa Sitta amekuwa akiiyumbisha serikali na chama chake kwa kuwashambulia hadharani makada wenzake ambao wengine ni mawaziri.


Anadaiwa kuonyesha jeuri aliyonayo dhidi ya viongozi wa juu wa chama hicho ambao amekuwa anawatuhumu kwa kumfanyia njama za kumwengua kwenye uspika baada ya uchaguzi mkuu mwaka jana.


Tayari amesikika hadharani kwenye mahojiano na vituo kadhaa vya televisheni akilaumu waliomwengua, akisema walitumia nguvu ya mafisadi.


Inaaminika kwamba ingawa Sitta hajawahi kutamka moja kwa moja, miongoni mwa watu anaowalaumu kwa hatua hiyo ni bosi wake, Rais Kikwete na washauri wake kadhaa.


Mwaka 2005 Rais Kikwete aliasisi jitihada za kumpa Sitta nafasi ya uspika baada ya kumwondoa katika orodha ya watu aliokuwa amewafikiria na kuwaahidi kuwapa cheo cha waziri mkuu.


Utendaji wa Sitta kama spika uliongeza makali ya Bunge na kulipa “meno” yaliyoumiza serikali kwa kiwango kikubwa, hatua iliyomfanya aanze kutazamwa kwa jicho la shaka na wale waliomweka pale. Mwaka jana walimfanyia njama kama zile ambazo mwaka 2005 walimfanyia mtangulizi wake, Pius Msekwa, wakamwondoa kwa kigezo kuwa wanataka Spika mwanamke.


Katika njama za timuatimua ya sasa, mlengwa mkuu ni Lowassa, ambaye pamoja na Chenge, amegoma kujiondoa kwa shinikizo la Nape, ambaye wachunguzi wanasema amekuwa akiagizwa kimya kimya na mabosi wake.


Lowassa na Sitta wanatuhumiwa kufitiniana kwa sababu za kisiasa, ikiwa ni pamoja na njama za kuwania urais mwaka 2015. Wote wanasemekana ama kuutaka urais au kutetea watu kadhaa katika makundi yao ambao wanasemekana kuwa na tamaa ya kuwania nafasi hiyo baada ya Rais Kikwete.


Wasiomtaka Lowassa wanasema iwapo ataondolewa chama kitaimarika. Lakini wanaomuunga mkono wanasema Lowassa akiguswa, chama kitatetereka, kwa kuwa ana mizizi mirefu kwenye chama, na hoja zinazotumiwa kummaliza zinawagusa viongozi wengine wakuu katika chama hicho, kiasi kwamba anguko lake halitakiacha chama kikiwa salama.


Baadhi ya makada wa chama hicho wamekuwa wakijenga hoja kuwa Lowassa ni tishio ndani ya chama hicho, na wengine wamempikia jungu kuwa amekuwa akimhujumu Rais Jakaya Kikwete tangu apojiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya kufua umeme wa dharura ya Kampuni ya Richmond, ambayo wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema inamgusa pia Rais Kikwete.


Hata hivyo mara kadhaa Lowassa ameweka wazi kuwa hajawahi kumhujumu Kikwete bali kuna makada wanataka kuwagombanisha watu hao.


Duru za kisiasa ndani ya CCM zinabainisha kuwa makundi hasimu ya Sitta na Lowassa kila moja limekuwa likihaha huku na huko kutaka kuwanusuru vigogo hao dhidi ya uamuzi ya NEC.


Chenge, ambaye amewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, amewahi kutamka kuwa “gamba limeishia kiunoni,” na kwamba wanaotaka kuliondoa “waje na shoka.”


Haijulikani kama Rais Kikwete amelipa shoka lake makali ya kutosha kukata gamba la Chenge, mmoja wa wanasiasa wanaojiamini na wenye nguvu ndani ya CCM.


Nape anaponzwa na kauli nyingi tata ambazo zinadaiwa kutoka kwake na “wanaomtuma” bila maagizo ya vikao vya chama; na kwamba kauli hizo zimechochea moto na kuzidi kukuza makundi hasimu ndani ya CCM.


Kwa muda mrefu amekuwa akiwalenga wanasiasa watatu tu - Lowassa, Rostam Aziz na Chenge – akisema lazima wajiondoe kwenye chama, la sivyo wanafukuzwa.


Tayari Rostam Aziz amejivua vyeo vyote ndani ya CCM na kuachia ubunge wa Igunga aliokuwa ameushikilia kwa miaka 18 mfululizo.


Katika hali inayoonyesha makada wanaamini kwamba Nape amekuwa anatoa matamko kwa maagizo ya Rais Kikwete, baadhi ya makada wanasema unaandaliwa mpango wa kumteua nape kuwa balozi katika moja ya nchi za Ulaya kama zawadi kwa “kazi nzuri” aliyofanya.


Hata hivyo, si wote wanaona kazi nzuri ya Nape, kwani baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho, wamekuwa wanalalamikia asili ya mamlaka na jeuri ya Nape inayomfanya atoe matamko ambayo hata wao, kama viongozi waandamizi wenzake, hawajawahi kufanyia uamuzi.


Wanasema kauli za Nape, licha ya kukigawa chama katika makundi hasimu, yaliigawa pia sekretarieti ya chama katika vipande viwili, jambo ambalo ni hatari kwa uhai wa chama.


Wengine wanasema kwamba kutokana na jeuri hii ya Nape, hata mwenyekiti wao ni sehemu ya matatizo yanayokikabili chama hicho, vinginevyo angekuwa amemchukulia hatua kali.


Hali hii inamweka pabaya Rais Kikwete katika kufikia uamuzi, kwani anajaribu kuepuka kukiingiza chama katika mpasuko mkubwa zaidi ambao unaweza kukigawa chama na kukiathiri vibaya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


UVCCM kufumuliwa


Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) nao unatarajiwa kufumuliwa kwa madai kuwa viongozi wake wamekuwa mstari wa mbele kuendeleza siasa za makundi, huku wakidaiwa kutumiwa na wanasiasa wenye malengo ya kuwania urais.


Hata hivyo, hakuna kundi ndani ya CCM ambalo halina masilahi au malengo ya urais; kwani kila kundi lina mtu wake.


Tanzania Daima Jumapili, limehakikishiwa kuwa miongoni mwa viongozi waliohojiwa na kamati ya maadili ya CCM ni Makamu Mwenyekiti, Beno Malisa na wenyeviti wengine wa mikoa ya Mara, Arusha na Kilimanjaro.


Umoja huo unadaiwa hivi sasa umekuwa chanzo kikubwa cha kushamiri kwa makundi yanayohasimiana tangu chama hicho kikumbwe na siasa za kuchafuana, chuki na kupakana matope.


Wachambuzi wa masuala ya siasa wameweka wazi kuwa CCM hivi sasa kinakabiliwa na wakati mgumu wa kutawala, si tu kutokana na mikwaruzano iliyopo ndani ya chama hicho bali pia kwa sababu ya kushamiri kwa upinzani hapa nchini.


Waliweka bayana kuwa kutokana na changamoto hizo kunakifanya chama hicho kiwe na kazi ngumu ya kurejesha imani kwa wananchi ambao kadiri siku zinavyokwenda wamekuwa wakiviunga mkono vyama vya upinzani.


Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa pia jana jioni Rais Jakaya Kikwete alitarajia kukutana na wabunge wote wa CCM kwa lengo la kuzungumza nao mambo mbalimbali, ikiwamo mchakato wa uanzishwaji wa Katiba mpya.


Inadaiwa Rais Kikwete anataka kuwaagiza wabunge wa chama hicho kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato huo ili wapinzani wasipate fursa ya kuzungumza kile kisichotakiwa na CCM.

0 comments

Post a Comment