Wachezaji 13 kati ya 26 wa timu ya kandanda ya Red Sea ya Eritrea waliosepa baada ya kushiriki kombe la Kagame Castle Cup wamejisalimisha katika Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar es salaam na kuomba hifadhi ya ukimbizi.
Msemaji wa Wizara Bw. Isaac Nantanga kaeleza sasa hivi kwamba hivi sasa wachezaji hao wanafanyiwa mahojiano na Idara ya Wakimbizi wizarani humo kabla uamuzi wa nini cha kuwafanya haujatolewa.
"Mahojiano haya ya awali yanafanywa ili kujua sababu zilizowafanya wachezaji hao kutorejea kwao na kama sababu hizo zinaweza kuwapa sifa ya kupewa hadhi ya ukimbizi kufuatana na sheria za kitaifa na kimataifa.
"Wakati wakiwa hapa nchini wechezaji hao wanahifadhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na hati zao za kusafiria zinashikiliwa na Idara ya Uhamiaji", alisema Bw. Nantanga.
Wachezaji hao waliingia mitini juzi wakati timu yao ilipokuwa inataka kuondoka kuelekea nyumbani juzi, baada ya kutolewa na Yanga katika robo fainali.
TFF waligundua kwamba jamaa wamesepa baada ya kujikuta wana hati za kusafiria 13 wakati msafara wa kwenya uwanja wa ndege ulipoanza. Ndipo wakatoa taarifa kunakohusika na msako ukaanza.
0 comments