Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Slaa awasilisha ushahidi kumbana Chenge

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ameendelea kumkalia kooni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na sasa amewasilisha serikalini uchambuzi wa ushahidi utakaosaidia kumtia hatiani mwanasiasa huyo, dhidi ya tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa rada.


Dk Slaa aliwasilisha waraka wa uchambuzi wa kisheria kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Nchini (DPP), Eliezar Feleshi, akiweka wazi kwamba Serikali ya Tanzania ina mamlaka ya kufanya uchunguzi dhidi ya uhalifu kwa watuhumiwa ambao ni raia wa Tanzania.


Katika waraka huo ambao Mwananchi umeuona, Dk Slaa ameweka wazi kuwa kazi iliyofanywa na Ofisi ya Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) ililenga kubaini makosa ya kuvunja sheria nchini Uingereza na kwamba Tanzania ilipaswa kufanya uchunguzi wake katika jambo hilo.


“Kimsingi SFO ilikuwa inafanya upelelezi kuhusiana na uvunjifu wa sheria chini ya mamlaka yao yaani Uingereza, Wales na Ireland ya Kaskazini. Makosa ya ufisadi wa rada yaliyofanywa na Watanzania (na mawakala wao) ni makosa dhidi ya Sheria za Tanzania,” inaeleza sehemu ya waraka huo na kuongeza:“Ni kwa msingi huo mimi niko “on record” ndani ya Bunge na nje ya Bunge kuitaka Serikali ya Tanzania nayo kuanzisha upelelezi wa kwake kwa mujibu wa Sheria za Tanzania kwani walioibiwa ni Watanzania na fedha zilizoibiwa ni za Watanzania”.


Dk Slaa alisema hakuna mantiki ya upelelezi wa ufisadi uliofanyika Tanzania kuachiwa mamlaka nyingine.
Aliliambia Mwananchi jana kuwa tayari amekamilisha uchambuzi huo na kwamba waraka husika ulikuwa katika mchakato wa kupelekwa kwa Feleshi.


Hatua hiyo ya Dk Slaa ni kuitika wito wa DPP ambaye juzi, alimtaka kuwasilisha nyaraka zenye ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa rada serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi, akieleza kuwa ushahidi alionao hautoshi kumtia Chenge hatiani kama atafikishwa mahakamani.


Msimamo wa Feleshi unaungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema, ambaye pia alimtaka Dk Slaa asaidie kupelekea ushahidi kwa kuwa sheria inaruhusu.Kadhalika, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah pia alishaweka bayana kwamba taratibu za kuwasilisha ushahidi ofisini kwake ziko wazi, hivyo kumtaka Dk Slaa kutumia njia hizo ili ushahidi huo akaufanyie kazi.


"Kama Chadema wanao (ushahidi), kama alivyoeleza Dk Slaa, walete tutaulinganisha na ushahidi tulionao ili tuone kama unatosha kuitetea kesi hiyo mahakamani," alisema Dk Hoseah


Ambana Chikawe
Katika waraka huo, Dk Slaa alisema kwamba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe alilidanganya Bunge pale aliposema kwamba Serikali haina ushahidi wa kumfikisha Chenge mahakamani.Alisema Serikali kupitia kwa AG iliandikiwa barua na SFO yenye Kumb.


Na SPCO1/D/MC ya Machi 21, 2008, iliyosainiwa na msimamizi wa kesi hiyo, Mathew Cowie kuhusu suala la rada.“Attorney General (Mwansheria Mkuu wa Serikali), ndiye Mshauri Mkuu wa Serikali kwa masuala ya kisheria, na hivyo ni dhahiri barua hiyo Serikali inaifahamu. Kutokana na barua hiyo, ni dhahiri Chikawe alipotosha Bunge na Taifa kwa kusema kuwa Serikali haina ushahidi,” unasema waraka huo.


Alisema barua ya SFO inawataja wahusika wote kwa upande wa Tanzania na kwamba miongoni mwao ni Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati mkataba huo uliposainiwa.“SFO wanaeleza fika kuwa nyaraka za mkataba zilikuwa moja kwa moja chini ya usimamizi na maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali”.


Barua/Fax ya Mark Simpkins wa SPS ya tarehe 30 Agosti, 1997 ni ushahidi dhahiri wa ushiriki wa Andrew Chenge,”anaeleza DK Slaa katika barua yake na kuongeza:“DPP anao mkataba wenyewe wenye kuonyesha dhahiri “Financial Arrangement” na kama hana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inao.




Dk Slaa aliweka bayana kuwa nyaraka zote husika ziko serikalini na kwamba wajibu wa raia mwema ni kutoa taarifa ya uhalifu kwa mujibu sheria zetu mbalimbali.“Isitoshe hisia za ufisadi huu hazikuanzia kwa raia tu bali hasa kwa chombo chenye wajibu wa kuisimamia Serikali yaani Bunge kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 63(2),(3),” unasema waraka huo na kuongeza:“Raia na wabunge hatuna vyombo vya dola. Kazi yetu ni kutoa mashaka (criminal suspicion na msingi wa suspicion hiyo). Kazi ya kupeleleza ni ya DPP na Dola”.




Kwa mujibu wa Feleshi kuna uwezekano wa nyaraka alizonazo Dk Slaa kuwa na ushahidi unaotofautiana na ushahidi uliopo serikalini hivyo kuwasilisha nyaraka hizo, kutasaidia kufanikisha jambo hilo.“Sheria zetu zina utaratibu mzuri wa kupokea ushahidi. Sheria ya Mwenendo wa Kesi na Makosa ya Jinai, kifungu cha Saba na ile ya kupambana na rushwa, kifungu cha 39, zinaeleza bayana kuwa mtu mwenye ushahidi anaweza kuuwasilisha kwenye vyombo vinavyohusika,” alisema Feleshi.


Feleshi alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa na gazeti hili azungumzie kauli ya Dk Slaa aliyoitoa Jumatano wiki hii kuwa Serikali ina ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wa rada ila imeamua kuwalinda.


Sakata la Rada


Jumatano wiki hii Dk Slaa alisambaza ripoti ya SFO yenye kurasa 11 na kusisitiza kuwa ushahidi huo unatosha kumtia Chenge hatiani.Dk Slaa alisambaraza ripoti hiyo kufuatia kauli ya Chikawe aliyedai Serikali haina ushahidi wa kuwafikisha watuhumiwa wa kashifa ya rada mahakamani.


Kitendo cha Dk Slaa kukubali ombi hilo la Serikali kinabadili sura na msimamo waliokuwa nao yeye pamoja na chama chake wa kutowasilisha ushahidi na badala yake kufanya maandamano nchi nzima kuueleza umma kuhusu tuhuma hizo za rada.


Dk Slaa alisema amefikia hatua ya kukubali kuandaa na kuwasilisha ushahidi huo kufuatia kauli ya DPP iliyotaka afanye hivyo kwa maelezo kuwa unaweza ukawa una tofauti na ule ambao Serikali inao.

0 comments

Post a Comment