Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Mbowe ataka JK avunje baraza la mawaziri

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amemshauri Rais Jakaya Kikwete kuangalia upya baraza lake la mawaziri kutokana na hili lililopo sasa kugawanyika.Kauli hiyo ya Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni inakuja wakati ambao Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, akiwa juzi ameonyesha msimamo hadharani kutaka Serikali iwaombe radhi Watanzania kutokana na mgawo wa umeme.


Pia, Sitta ametaka wahusika wachukuliwe hatua, msimamo ambao umetolewa katika kipindi ambacho Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akiendelea kukaangwa Bungeni kuhusu mgawo huo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema kitendo cha viongozi wa ngazi za juu Serikalini wakiwamo mawaziri kutofautiana hadharani kunaonyesha wazi kuwa Serikali imepoteza uhalali wake.
Tayari, Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe walishawahi kuingia katika mvutano wa wazi na mawaziri Ngeleja na Mathias Chikawe ( Ofisi ya Rais Utawala Bora), kuhusu uhalali wa tuzo ya Sh 94 bilioni kwa Kampuni ya Dowans.


Jana, Mbowe akirejea kauli ya Sitta aliyoitoa mkoani Mbeya juzi kuhusu matatizo ya umeme nchini, alisema, “Waziri wa Nishati na Madini (Ngeleja) anatoa kauli, mwenyekiti wa kamati ya Bunge ambaye ni Mjumbe wa Sekretarieti ya chama (CCM) anatofautiana nayo, mbaya zaidi anakuja waziri naye anatoa kauli inayoshutumu Serikali yake.Kwa mtindo huu, ni dhahiri Serikali imepoteza uhalali wake,”alisema Mbowe na kuongeza:


“Tunamtaka Rais (Kikwete) atafakari upya baraza lake la mawaziri na kisha kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuliwajibisha, kama waziri anayeingia kwenye kikao cha baraza la mawaziri anatoka nje na kutoa kauli inayotofautiana na uamuzi wa baraza zima, hiyo ni ishara tosha kuwa Serikali hiyo imegawanyika.”


Akisisitiza, Mbowe alisema mawaziri ndio wanaotegemewa kutoa taarifa juu ya mipango ya Serikali ya kushughulikia matatizo yakiwa mgawo wa umeme na kueleza kuwaa kitendo cha wao kutofautiana ni hatari kwa taifa.


Alionya kuwa kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa Serikali haina mkakati wa kutatua tatizo hilo na kuongeza kuwa, ukimya huo ni hatari na unaweza kuliingiza taifa kwenye vurugu.


Katika mkutano huo, Mbowe alisema kamati kuu ya chama hicho iliyokutana jana ilitarajiwa kujadili kwa kina suala hilo la mgawo wa umeme unaoendelea nchini kote na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua katika kukabiliana nalo.


Alionya kwamba, kama Serikali haitachukua hatua za kusudi za kuonyesha namna ya kutatua tatizo hilo, basi nchi itadhurika.Alieleza kuwa mgawo huo wa umeme umeliathiri taifa kwa kiwango kikubwa kutokana na kuendelea kuporomoka kwa uchumi.“Hivi sasa viwanda vingi nchini vinafungwa, vijana wengi wanapoteza ajira, taifa linaporomoka kiuchumi na wakati huo huo Serikali haina majibu yanayoonyesha dhamira ya kweli ya kumaliza tatizo hilo,”alieleza.


Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema chama chake kimeamua kuliwasilisha suala hilo la mgawo wa umeme pamoja na mambo mengine kwenye kamati kuu ili wazee washiriki kulijadili na kutoa msimamo wa pamoja wa hatua za kuchukua katika kupambana nalo.


“Tumewasilisha hilo kwenye kamati kuu ili wazee watupatie mwelekeo na kesho (leo), tutakwenda na tamko letu Bungeni linaloonyesha msimamo wa chama kama hawatatusikiliza tutaliwasilisha kwa wananchi,”aliongeza.


Alisema hadi sasa mgawo huo umevuruga mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano ulioandaliwa na Serikali ukielekeza kuwa uchumi ungekuwa kwa asilimia 7.2 kwa mwaka, na badala yake umeporomoka hadi asilimia 5.8.


Aliongeza kuwa tangu mgawo huo umeanza takribani Sh 1 trilioni zimepotea, hali inayoendelea kuporomosha uchumi wa taifa ambalo ni miongoni mwa nchi maskini sana za Kusini mwa jangwa la Sahara.


“Sisi (Chadema) tumeshauri hata kwenye hatuba yetu ya kambi ya upinzani kuwa iundwe task force (kikosi kazi) kitakachohusisha wabunge, wataalamu na watu wa kada mbalimbali ili kutafuta chanzo cha tatizo hilo na kuja na njia mbadala ya kutatua kero hiyo,”alisema Mbowe.


Mwanasiasa huyo aliweka bayana kwamba Tanzania ni nchi yenye rasimali nyingi na haistahili kukabiliwa na kero kama hiyo inayoendelea hivi sasa .


Katika hatua nyingine, Mbowe alieleza kuwa kamati kuu pia iliyoketi jana ilitarajiwa kumjadili Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, kutokana na kitendo chake cha kutofautiana na msimamo wa wabunge wa chama hicho Bungeni.


Akizungumza hilo, Mbowe alisema kamati hiyo itakaa kujadili hilo na kutoa maamuzi leo kwa namna itakavyoona inafaa.“Chadema ni chama kinachofuata katiba yake, kinafanya maamuzi kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria zake, ieleweke kuwa maamuzi ya kamati siyo ya Mbowe, bali ni ya chama,”alieleza na kuongoza:


“Tunaleta hoja hizo huku kwa wazee wetu ili waweze kujadili na kutoa msimamo, maamuzi siyo yangu ( Mbowe) ni ya kamati kuu. Kitu cha msingi ni kwamba chama bila nidhamu siyo chama, nasi ndani ya Chadema kuna taratibu zetu.”


Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kikao hicho pia kilikaa kujadili ripoti ya madiwani wa Arusha wanaodaiwa kukiuka taratibu za chama na kuingia mwafaka na wenzao wa CCM bila ridhaa ya chama hicho. Mwafaka huo umesababisha mtafaruku ndani ya chama hicho, kiasi cha kulazimisha kuunda kamati maalum ya uchunguzi chini ya Mabere Marando, ambayo imechunguza na kuwasilisha mapendekezo yake chamani, ambayo yalitarajiwa kujadiliwa jana.

0 comments

Post a Comment