IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI Kivuli wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), na Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Leticia Nyerere amejiuzulu wadhifa huo.Hatua ya kujiuzulu kwa mbunge huyo imekuja kipindi kisichozidi miezi minne tangu kuundwa kwa baraza hilo katika Mkutano wa Bunge la Februari.
Taarifa za kujiuzulu kwa Nyerere zilivuma kuanzia jana mchana huku Spika wa Bunge Anne Makinda, akisema anasubiri taarifa za uteuzi kutoka kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Akizungumza kwa simu jana jioni, Nyerere alithibitisha kujiuzulu akisema hatua yake ni uamuzi aliouita wa kidemokrasi kwani unalenga kutoa fursa kwa wengine kuongoza. Hata hivyo, hakutoa sababu za kuchukua hatua hiyo. Alisema Chadema kina wabunge 48 wakati nafasi za mawaziri ni 18 ukiacha manaibu, hivyo ameamua kuwapa nafasi wengine wapate uzoefu.
Mbunge huyo aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana alisema tayari amesambaza nakala ya barua hiyo hadi Ofisi ya Spika wa Bunge."Nimeamua kuachia ngazi ili kupisha wengine wapate uzoefu. Ni uamuzi wa kidemokrasi na hii ndiyo demokrasi. Demokrasi ni kuruhusu wengine waweze kuonyesha uwezo wa kuongoza," alisisitiza na kuongeza:,
"Kwa hiyo mkakati kama huu wa kutoa nafasi kwa wengine ili waongeze nadhani ni mzuri. Nimechukua uamuzi huu mchana na tayari nimeshasambaza barua kunakohusika na nakala ipo hadi kwa Spika."
Baraza kivuli la mawaziri lililotangazwa Februari mwaka huu linaundwa na wabunge wa Chadema pekee.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Waziri kivuli Chadema aachia ngazi
0 comments