Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Ngome za urasi wa 2015 zaitikisa CCM?

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Katibu mkuu wa CCM,Wilson Mukama
MBIO za kuwania urais ndani ya CCM zinaendelea kukitikisa chama hicho, baada ya nguvu ya makundi ya watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo kuendelea kuvutana na kukipasua chama hicho.Mgogoro unaoendelea ndani ya CCM mkoani Arusha ambao unaelezwa kuwa unatokana na nguvu za makada wawili wa chama hicho wanaotaka kuwania urais mwaka 2015, sasa umeingia kwa wabunge wa chama hicho kikongwe nchini kuashiria kuwa sasa kinapitia katika wakati mgumu.


Ingawa mamlaka ya chama hicho imeonya kuwa haitawavumilia watu wanaochochea migogoro hiyo kwa maslahi yao binafsi ya kuwania urais, inaonekana moto uliowashwa na makundi hayo ni mkubwa na ni vigumu kuuzima.
Hivi karibuni ilidaiwa kuwa, wakati Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, akiwahoji watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho, alimwambia wazi mmoja wao kwamba aachane na mbio za kuwania urais, kwani anakivuruga chama.


Katika kuonyesha ukubwa wa mgogoro huo wabunge wa CCM wamemtaka Katibu Mkuu chama hicho, Wilson Mukama, kuchukua hatua za kuukomesha na ikiwezekana kwa 'kuwafukuza' watakaobainika kuchochea hali hiyo.
Mgogoro wa hivi karibuni ambao umekitikisa chama hicho tawala ulitokea mkoani Arusha ambako baadhi ya viongozi wa UVCCM, walijitokeza hadharani kumpinga Katibu wa CCM mkoani humo, Mary Chatanda.


Viongozi hao walitaka Chatanda ang'olewe katika nafasi yake ama ahamishwe mkoani Arusha kwa kile walichoeleza kuwa anaharibu chama.


Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM waliokutana katika Ukumbi wa Pius Msekwa eneo la Bunge mjini Dodoma juzi jioni, zinadai kuwa baadhi ya wabunge walimtahadharisha Mukama kuhusu vurugu zilizoko ndani ya chama na kumtaka achukue hatua za haraka badala ya kuendelea kukaa kimya.


"Kikubwa hapa kilikuwa ni mgogoro wa Arusha, ambao baadhi ya wabunge wanadai unachochewa na baadhi ya watu wanaofahamika. Wanakasirishwa sana na walihoji kazi ya Katibu Mkuu ni ipi ikiwa hali inaendelea kuwa hivyo ndani ya chama," kilidokeza chanzo chetu katika mkutano huo na kuongeza:
"Wengine walimwambia Mukama kwamba asipoangalia atakuwa Katibu Mkuu wa kutatua migogoro tu, badala ya kutekeleza shughuli za kukiimarisha chama".


Kwa mujibu wa habari kutoka katika kikao hicho, msingi wa hoja ya vurugu ulijengwa katika hali ya kisiasa mkoani Arusha, wabunge waliochangia hoja hiyo, walionyesha hofu ya migogoro kusambaa katika mikoa mingine.


Walisema hali hiyo inaweza kukiyumbisha CCM hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali.
"Migogoro hii inachochewa na baadhi ya watu na wanajulikana, sasa tukiendelea kuwalea wakafanikisha malengo yao mkoani Arusha, watahamishia vurugu hizi katika sehemu nyingine,"kilisema chanzo chetu kikimnukuu mmoja wa wabunge walihohudhuria kikao hicho.


Mukama awa Mbogo
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho cha Wabunge wa CCM, zinasema Mukama alipopewa nafasi ya kuzungumza aligeuka mbogo na kuweka wazi kwamba, hakuna mwanachama yeyote wa CCM ambaye ni maarufu kuliko chama.


"Nasema hivi, kuna watu wanadhani wako juu ya chama, hili si sahihi hata kidogo. Hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuwa maarufu zaidi ya CCM na ikibainika kwamba miongoni mwetu wamo wanaochochea vurugu basi tutawafukuza,"alinukuliwa Mukama akizungumza katika kikao hicho.


Habari zaidi zinasema Mukama alitumia fursa hiyo kuwaeleza wabunge kiini cha mabadiliko ndani ya CCM na utaratibu mzima ambao utatumika katika kutekeleza mageuzi yanayokusudiwa kukiwezesha chama hicho kujenga tena imani kwa umma.


"Tunataka Watanzania waondokane na imani kwamba chama chetu kinawakumbatia mafisadi na kuwatelekeza wanyonge. Hili lazima lifanyike na tumejipanga kutekeleza hilo," alinukuliwa Katibu Mkuu huyo wa CCM.


Uongozi wa CCM
Mwananchi iliwasiliana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuhusu yaliyojiri katika kikao hicho cha wabunge wa CCM, ambaye pamoja na kukiri, kwamba alihudhuria, hakuwa tayari kukanusha au kuthibitisha kuwapo kwa mjadala unaohusu migogoro ndani ya chama hicho.


"Jamani sawa, mimi nilikuwamo kama msikilizaji tu. Kikao kilikuwa cha wabunge wa CCM kwa hiyo watafute viongozi wao, hasa Katibu wao (Janister Mhagama) atakueleza yaliyojiri huko, vinginevyo mimi utakuwa unanionea bure ndugu yangu," alisema Nape kwa simu.
Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho mkoani Ruvuma, alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi hakupatikana baada ya simu hiyo kuita bila majibu.


Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa mbunge huyo alikuwa katika kikao cha wabunge wanawake wote chini ya uongozi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda. Hata hivyo, Mukama alikanusha suala la migogoro ndani ya CCM kuzungumziwa kwenye kikao hicho cha wabunge akisema hizo ni taarifa za uongo. "Mimi nilikuwapo kwenye kikao hicho, mbona hayo unayosema hayakuzungumzwa," alisema Mukama na kukata simu.


Alipopigiwa simu mara ya pili, Mukama alisema "......tafadhali sana msinipotezee muda kwa taarifa hizo za uongo. Mimi nilihudhuria, mambo yaliyozungumzwa ni kuhusu bajeti tu sasa hayo mnayatoa wapi?", alisema ana kukata tena simu.


Peter Saramba na Moses Mashalla wanaripoti kuwa, Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa baada ya mvutano uliyochukua muda mrefu kuhusu Millya kuvuliwa uanachama, wajumbe wa kikao cha Halmashauri ya CCM, Mkoa wa Arusha waliamua kuwa makundi yote ya vijana yaliyokuwa yakipingana yapewe onyo.


Hata hivyo, uamuzi huo kwa makundi hayo ulipokelewa kwa furaha na kambi ya Millya baada ya vijana wanaomuunga mkono kuamua kumsindikiza kwa shangwe kutoka kwenye ukumbi wa mkutano, huku wale wa Chatanda wakiondoka vichwa chini.Hatua hiyo inaonyesha wazi kwamba uamuzi huo unadhirisha kuwa mgogoro huo na kwamba haujaisha.


Awali, Millya alisema kuwa yupo tayari kwa uamuzi wowote utakaochukuliwa na chama chake, iwe kumfukuza, au kutomfukuza ndani ya chama.“Niko tayari kwa uamuzi wowote utakaotolewa na chama dhidi yangu. Mimi ni kijana na ninataka kuwa mwanasiasa ndani au nje ya CCM. Hata nikifukuzwa CCM nitaendelea kuwa mwanasiasa. Kuna njia nyingi za kuendelea kufanya siasa,” alisema.


Mwenyekiti huyo alisema akifukuzwa atakapokea kwa moyo mkunjufu uamuzi huo ingawa atasikitika kwa muda na rasilimali alizotumia kukijenga na kukiimarisha chama hicho tangu alipojiunga mwaka 2003 wakati anasoma Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa.“Iwapo hilo litatokea (kufukuzwa) nitasononeka kwa sababu sikutarajia mwisho wangu wa uongozi ndani ya chama changu kutokea kwa njia hiyo,” alisema Millya.


Alifahamisha kuwa ana wafuasi wengi ndani ya jumuiya hiyo na Kamati Kuu ya CCM, na kutoa mfano wa kura zaidi ya 5,000 alizopata wakati wa kura za maoni ya kuteuliwa kuwania Ubunge jimbo la Simanjiro mwaka jana kuwa ni kielelezo tosha.


Alionya kuwa kama uamuzi wa kumfukuza utachukuliwa na kubarikiwa na vikao vya chama, utakuwa mwanzo wa mwisho wa chama hicho kikongwe nchini, kwani itadhihirisha kuwa viongozi waliopo wanaongoza kwa kufuata maslahi na matakwa yao badala ya wanachama waliowaweka madarakani.


Hata hivyo, Millya aliyekuwa akizungumza baada ya kutolewa ndani ya ukumbi wa mkuutano uliofanyika Kituo cha Vijana (Youth Center) mjini hapa, alisema haungi wala kushawishi vijana kuhama CCM, lakini pia hawezi kuwazuia kusikiliza mioyo na hisia zao.


Akifafanua alisema kinachokiponza chama hicho kilichoadhimisha miaka 34 ya kuzaliwa Februari 5, mwaka huu ni tabia ya baadhi ya viongozi kuongoza kibabe wakijiona kuwa bora kuliko wananchi au wanachama wengine.


Millya alipinga fikra zilizojengeka kwa baadhi ya watu kuwa hakuna chama mbadala cha kuongoza taifa zaidi ya CCM akisema kwamba, vyama vingine vipo na baadhi vimeonyesha kwa vitendo kuwa vinaweza kuaminiwa na wananchi.

0 comments

Post a Comment