IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Cliton, anatarajiwa kuwasili nchini leo katika ziara inayoelezwa kuwa ya kirafiki yenye lengo la kuendeleza uhusiano mzuri kwa nchi hizo mbili.
Cliton atakuwa kiongozi wa tatu wa ngazi za juu nchini Marekani kutembelea Tanzania, wa kwanza akiwa Rais wa zamani Bill Clinton, mwaka 2000 na Rais George Bush aliyetembelea mwaka 2008.
Mbali na viongozi hao wakuu kutembelea hapa nchini, kitendo cha Rais Kikwete kuwa Rais wa kwanza wa Afrika kukutana na Rais wa nchi hiyo, Barack Obama, miezi michache baada ya kuchaguliwa kuliongoza taifa hilo kubwa kinaonyesha jinsi Tanzania ilivyo karibu na taifa hilo ambalo limejizolea maadui wengi kutokana na sera yake ya kupinga ugaidi.
Ujio wa waziri huyo, unaweza kusababisha baadhi ya shughuli kusimama kwenye maeneo ya jiji atakakopita na kutembelea.
Usalama katika jji la Dar es Salaam unategemewa kuimarishwa zaidi kama ilivyokuwa wakati wa ziara ya Rais Bush takriban miaka mitatu iliyopita.
Inaelezwa Clinton atakapokuwa nchini, ziara yake itaanza kwa kukutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Naibu Waziri Mkuu wa Ireland, kuzungumzia mradi wa siku 1000 za lishe nchini.
Vivyo hivyo kesho atakuwa na ratiba kali ambapo ataongozana na Pinda kutembelea chama cha ushirika cha wakulima kilichoko Mlandizi, Kibaha, mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ubalozi wa Marekani, Waziri Cliton siku hiyohiyo atapata fursa ya kutembelea mitambo ya kufua na kuzalisha umeme ya Symbion iliyoinunua toka katika kampuni iliyokuwa ikipigiwa kelele ya Dowans.
Kutembelea mitambo hiyo kunatokana na kampuni hiyo ya Symbion kutoka nchini Marekani, nchi ambayo pia msaada katika Mradi wa Changamoto za Milenia (MCC) unatokea.
Akiwa katika mitambo hiyo, Hillary Cliton atakutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Symbion Power LLC, Paul Hinks, na Ofisa Mkuu Mtendaji wa MCC, Daniel Yohannes.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kiongozi huyo kesho hiyo hiyo atapata fursa ya kutembelea kituo cha afya cha wanawake kilichoko Buguruni, ambacho kinahusika na masuala ya virusi vya ukimwi na uzazi.
Waziri huyo atamaliza ziara yake ya siku hiyo kwa kukutana na Rais Jakaya Kikwete na kufanya naye mazungumzo ambapo pia watakuwa na mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Hillary Clinton kutua nchini Leo
0 comments