Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Swala La Ufutaji Posho, Bunge njia Panda. Mbowe asema watumishi hudai Posho hata kwenye Elimu dhidi ya UKIMWI

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MSIMAMO wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kutaka wabunge, watumishi na watendaji wa serikali wafutiwe posho, umeliweka njia panda Bunge.


Mbali na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuandika barua rasmi kwa Katibu wa Bunge kutaka posho zake zifutwe, msimamo huo jana uliungwa mkono na wabunge wote wa CHADEMA baada ya kikao kizito jana.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, alisema CHADEMA inataka posho za watumishi wote nchini wakiwemo wabunge, zifutwe.


Alisema posho hizo zikifutwa, serikali itaweza kukusanya sh trilioni moja ambazo zitasaidia shughuli nyingine za maendeleo.


“Sisi hatupiganii posho za wabunge tu na pia ni makosa kututaka wabunge wa CHADEMA tususie. Tunapigania matumizi mabaya ya posho kwa watumishi wote. Bajeti inasema serikali itakata posho, lakini ndani ya bajeti hiyo hiyo kuna mabilioni yametengwa kwa posho. Huu ni wizi.”


“Unamlipa mtumishi posho kwa kazi yake anayolipwa mshahara. Ofisa elimu anakwenda kukagua shule, unamlipa posho, watendaji wanakaa vikao kwenye ofisi zao, wanalipwa posho. Hatuwezi kuendelea hivi, nchi maskini hii,” alisisitiza Mbowe.


Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA, alisema watawasilisha bajeti yao mbadala Jumanne ijayo ambayo alitamba kuwa itaainisha umuhimu wa kufyeka posho na faida ambayo taifa itaipata.


Kuhusu posho za wabunge, Mbowe alisisitiza kuwa zifutwe kwani bora kupandisha mishahara yao lakini wasiendelee kulipwa posho.


“Kama tunaona mishahara ya wabunge ni midogo, bora iongezwe na hata ya watumishi wengine, lakini posho zifutwe. Posho zimewalemaza watumishi kwani kama kikao hakina posho, hawaendi, hata vikao vya kuelimishana jinsi ya kujikinga na ukimwi, watu wanataka posho. CHADEMA tunasema hapana,” alisema Mbowe.


Mwenyekiti huyo alipingana na dhana aliyoiita potovu ya kuwataka wabunge wa CHADEMA pekee wasusie posho.


“Hapa sio suala la kutaka wabunge wachache wa CHADEMA wasusie posho. Tunataka serikali ijenge mfumo wa kufuta posho kwa nchi nzima; CHADEMA wakikataa kuchukua, wengine wakiendelea kupokea haina maana na hata tukichukua, haina maana kwamba tusipige kelele kupinga ulipaji wa posho hizo,” alisema Mbowe.


Akitolea mfano wa magari ya kifahari yanayonunuliwa na serikali, Mbowe alisema hata kama serikali imemnunulia gari la aina hiyo, ataendelea kupinga utaratibu huo kwani unalizidishia taifa umaskini.


Akijibu barua ya Zitto na msimamo wa CHADEMA, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, alisema posho za wabunge haziwezi kufutwa na wala hazimo kwenye kundi la watumishi wanaopaswa kufutiwa posho.


“Zitto na wenzake ndio waliopitisha posho za wabunge. Kwa hiyo wanachofanya ni unafiki wenye lengo la kujipatia sifa,” alisema Mkullo.


Mkullo ambaye alisema anaisubiri kwa hamu kuiona na kuichambua bajeti ya upinzani, alisema hawana hoja za msingi na kuongeza kwamba wanaotaka kukataa posho, watapewa fomu maalumu za kujaza ili posho zao zielekezwe kwenye vituo vya watoto wasiojiweza.


“Nimeiona barua ya Zitto na nimesikia msimamo wa CHADEMA, tutaandaa fomu kwa wasiotaka posho ili fedha zao ziende kwa yatima na vituo vya wasiojiweza,” alisema Mkullo.


Mkullo akisema kwenye hotuba yake alisema serikali itafuta posho zisizo na tija, lakini posho za wabunge hazimo kwenye kundi hilo.


Mbali ya Mkullo, msimamo wa CHADEMA pamoja na barua ya Zitto kukataa posho, umeonekana kuwavuruga wabunge wa CCM ambao wanapinga vikali kufutwa posho zao.


Wabunge wa CCM ambao jana walikuwa na kikao chao cha kupeana msimamo wa jinsi ya kuitetea bajeti, walionekana kwenye vikundi kujadili hoja hiyo.


Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, zinasema kuwa pamoja na mambo mengine, wabunge wa chama hicho tawala wameungana kupinga kufutwa posho zao.


Kwa sasa wabunge wote wanalipwa per diem ya sh 80,000 na posho za vikao (seating allowance) ya sh 70,000, hivyo kuweka kibindoni sh 150,000 kila siku wawapo vikaoni.


Akiwasilisha bungeni juzi Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/12, Waziri Mkulo alibainisha hatua kadhaa za serikali kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima.


Aliahidi kupunguza posho zisizo na tija, safari za ndani na nje za viongozi na ukubwa wa misafara ya viongozi hao ili fedha husika ziweze kutumika kugharimia shughuli nyingine za maendeleo.


Aliahidi pia kusitisha ununuzi wa samani za ofisi, hususan zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, kupunguza malipo ya matumizi ya mafuta kwa magari ya serikali, kupunguza safari za ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa misafara na kuendelea kupunguza semina na warsha, isipokuwa pale inapobidi na kwa kibali cha Ofisi ya Waziri Mkuu.

0 comments

Post a Comment