IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa jana alijumuika na maaskofu wengine wa kanisa hilo kumsimika, Mchungaji Stanley Konso Hotay kuwa Askofu wa Kanisa hilo licha ya zuio la Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Sherehe za kusimikwa Askofu, Hotay zilifanyika, makao makuu ya Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, katika Kanisa la Kristo na kuhudhuriwa na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima.
Akizungumza katika sherehe hizo, Askofu Mokiwa alisema Mahakama Kuu imezuia Mchungaji Hotay asiapishwe kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro na wao wamemsimika kuwa Askofu ya Kanisa la Angilikana Tanzania hivyo hawajaingilia mahakama.
“Wanahabari tunaomba mliweke wazi hili, Askofu Hotay sasa ni Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania na kesi ikienda vizuri tutampa kiti chake cha Askofu wa Mount Kilimanjaro na mimi Jumapili ijayo nitakuwepo hapa tena,” alisema Askofu Mokiwa.
Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu ilisisitisha kusimikwa kwa Askofu Hotay baada ya waumini watatu kutoka Parishi ya Mtakatifu James ya kanisa hilo, Lothi Oilevo, Godfrey Mhone na Frank Jacob kufungua kesi wakipinga kusimikwa kwake kwa madai mbalimbali likiwamo la kugushi umri.
Jaji Kakusuro Sambo alitoa uamuzi huo akisema baada ya kusikiliza maombi ya walalamikaji kutaka kesi hiyo kusikilizwa kwa dharura na hoja zilizowasilishwa na mawakili wa pande zote Meinrad D’souza upande wa mashtaka na Arbert Msando utetezi iliona mahakama haikuwa katika mazingira bora ya kisheria ya kutoa uamuzi Ijumaa hiyohiyo na kusema kwamba atafanya hivyo leo. Alitoa amri ya kusimama kwa shughuli yoyote ambayo litaingilia shauri hilo, ikiwepo ya kusimikwa Askofu Hotay kuwa Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro.
Hata hivyo, Askofu Saimon Makundi ambaye alikuwa akiongoza dayosisi hiyo hakuhudhuria.
Akizungumza katika sherehe hizo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana la Tanzania, Dk Leonard Mtetemela aliwaonya wanaotumia vibaya mamlaka walizozazo katika jamii na kuanza kujikweza.
Alisema watu wenye mamlaka ya kutoa uamuzi wanapaswa kumwogopa Mungu: “Kuna watu wanatumia mamlaka yao vibaya, wanajiinua hadi kudai utukufu alionao Yesu Kristo jambo hili siyo zuri katika jamii.”
Wakati kesi hiyo ikisikilizwa kwa mara ya kwanza Ijumaa iliyopita, Wakili D’souza alieleza mahakama kuwa, kusimikwa kwa Askofu huyo jana, kungeathiri kesi ya msingi ya wateja wake ambao wanalalamikia taratibu mbalimbali za kanisa hilo, ikiwamo Katiba kukiukwa .
Hata hivyo, Wakili Msando alipinga hoja hiyo na kuomba mahakama kutupilia mbali shauri hilo akidai kuwa upungufu wa kisheria akitolea mfano wa walalamikaji kushindwa kutoa malalamiko yao dhidi ya ushindi wa Hotay kwa kufuata taratibu za kanisa tangu kulipofanyika uchaguzi Aprili 15, mwaka huu.
Wakili Msando pia alieleza mahakama kuwa maombi hayo ya walalamikaji yana upungufu kisheria kwani mmoja wao, Mhone hana hati ya kiapo kuthibitisha madai yake na wote hawana uwakilishi wa taasisi yoyote ya kanisa hilo au kutambuliwa kuwa ni waumini wa kanisa hilo.
“Walalamikaji kama wanajua taratibu za kanisa walipaswa kutoa malalamiko yao katika kanisa hilo tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu, mwezi April lakini wamekaa kimya hadi dakika za mwisho Askofu anataka kusimikwa ndipo wanawasilisha kesi na maombi yao, ”alisema Msando.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Askofu Anglikana asimikwa licha ya zuio la mahakama
0 comments