Waziri wa Elimuna Mafunzo ya Ufundi stadi Dr. Shukuru Kawambwa (katikati) |
Aidha, imesema wanafunzi 1,062 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambao jana walifanya maandamano wakitaka kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo, watalipwa Sh milioni 389.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alitangaza hayo bungeni hapa jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi).
“Hili la fedha za kujikimu, tumeongeza fedha hizo kutoka Sh 5,000 za sasa. Lakini hapa siwezi kusema tumeongeza kwa kiasi gani, isipokuwa msubiri Bajeti ya Wizara, mtafahamu hilo,” alisema Naibu Waziri Mulugo.
Katika swali lake la nyongeza, Mkosamali ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, alihoji kama Serikali itaongeza fedha za kujikimu katika bajeti ya mwaka huu kufikia Sh 10,000 na pia akahoji ni lini itatoa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vya Saut, Udom na Dar es Salaam (Udsm) ili wasiingie mtaani na kufanya maandamano.
Awali, akijibu swali la msingi la Mkosamali, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alisema Serikali imedhamiria kuboresha mfumo wa utoaji mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) pamoja na utendaji wake.
“Tume Maalumu iliyoundwa na Rais kutazama na kutoa mapendekezo juu ya kuboresha mfumo na taratibu za utoaji mikopo ikiwamo pia utendaji wa Bodi ya Mikopo, imekamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti yake serikalini,” alisema Mulugo.
“Kwa sasa, Serikali inayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuainisha maeneo yanayohitaji kuridhiwa na Baraza la Mawaziri pamoja na yale ya kiutendaji,” alifafanua Naibu Waziri.
Alizungumzia sababu za wanafunzi kuomba kuongezwa kiwango cha mkopo wa fedha za kujikimu kutoka Sh 5,000 hadi Sh 10,000 kwa siku kuwa ni kupanda kwa gharama za maisha hususan bei ya vyakula na kodi ya pango.
Alisema Serikali imepokea ombi hilo la wanafunzi na imekubali kuongeza kiwango hicho kwa mwaka wa fedha 2011/12 hasa ikizingatiwa, kwamba kiwango cha sasa kimekuwapo tangu mwaka 2007 bila marekebisho.
Kuhusu ucheleweshaji wa kuingiza fedha kwenye akaunti za wanafunzi alisema unatokana na sababu mbalimbali zikiwamo za mawasiliano hafifu kati ya vyuo, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Bodi ya Mikopo na mtiririko wa fedha kutoka Hazina. “Hata hivyo, Serikali inafuatilia kwa makini madai haya na kama ikibainika kwamba kuna ucheleweshaji wa makusudi, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema Naibu Waziri.
Akijibu swali kuhusu fedha za mafunzo kwa vitendo, Mulugo alisema kwa Udom, wanafunzi 1,062 wa programu 13 suala lao limeshughulikiwa na wametengewa Sh milioni 389.
Katika swali lake la msingi, Mkosamali alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani za haraka za kubadilisha mfumo wa mikopo kwa wanafunzi; sababu ya wanafunzi kutaka kuongezwa kiwango cha fedha za kujikimu na inachukua hatua gani za kinidhamu kwa wafanyakazi wanaochelewa kuingiza fedha za wanafunzi kwenye akaunti zao.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/12, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, alisema Serikali inapendekeza kufanyiwa marekebisho katika mgawanyo wa mapato yatokanayo na tozo za kuendeleza ufundi stadi ya asilimia sita ili asilimia nne zipelekwe Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA); lengo la hatua hiyo akisema ni kuongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.
0 comments