IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SAKATA la mgogoro wa Kanisa la Anglikana mkoani hapa limechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutoa hati ya kukamatwa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini.
Mbali ya hilo pia Mahakama hiyo awali ilisimamisha shughuli zote za usimikaji wa Askofu na juzi pia kutoa hati ya kukamatwa kwa Askofu aliyesimikwa juzi, Stanley Hotay.
Kutokana na amri hiyo, iwapo Askofu Hotay atakamatwa na kutiwa hatiani kwa kosa la kukaidi amri ya Mahakama, huenda akawa amepoteza sifa za kuwania tena kiti hicho cha uaskofu kwa mujibu wa taratibu za kanisa hilo.
Kutolewa kwa hati hiyo na Jaji Kakusulo Sambo kumekuja siku moja baada ya juzi Askofu Hotay kusimikwa kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania badala ya Dayosisi ya Mount Kilimanjaro.
Juni 10, Mahakama Kuu hiyo ilitoa amri ya kuzuia kuapishwa kwa Askofu Hotay, hadi shauri la kupinga kusimikwa kwake lililofunguliwa na waumini watatu wa Kanisa la St. James jijini hapa litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Waumini waliofungua kesi hiyo ni pamoja na Godfrey Mhone ambaye ni mume wa mwanamuziki wa injili nchini, Beatrice Mhone, Lothi Oilevo na Frank Jacob, ambapo kwa pamoja wanadai kwamba uchaguzi uliomweka madarakani Askofu huyo una mpango mahsusi wa kukiuka Katiba ya Kanisa hilo.
Akitoa uamuzi wa Mahakama hiyo mara baada ya kusikiliza hoja za pande mbili katika shauri hilo, Jaji Sambo alisema ameridhika pasipo shaka kwamba amri ya Mahakama aliyoitoa Ijumaa ilipuuzwa.
Alisema katika kosa kama hilo, sheria iko wazi kushughulikia watu wanaokiuka amri za Mahakama.
Alisema kwa vile shauri hilo lilikuwa halimhusu Dk. Mokiwa, lakini katika hatua nyingine tayari amefanya jambo ambalo limesababisha amri ya Mahakama isiheshimiwe, “sasa natoa amri ya Mahakama ya kumtaka Askofu Mokiwa na Askofu Hotay wakamatwe haraka sana. Na uamuzi mdogo wa shauri hili nitautoa baadaye.
“Kwa sababu huyu tayari amekwishakuwa Askofu na mtu akishasimikwa kuwa Askofu ni kazi kweli kweli kumwondoa,” alisema Jaji Sambu.
Huku akionekana kuwa mkali, Jaji Sambu alisema pamoja na Mahakama hiyo kutoa amri hiyo, lakini kwa sasa itabidi kuangalia upya tena namna ya kuendesha shauri hilo kutokana na kuapishwa kwa Askofu huyo.
Alisema kabla ya Mahakama kusikiliza upande wa pili uliokuwa unalalamikiwa, tayari ulishamsimika Askofu Hotay ambapo kwa hatua hiyo, ni sawa na kupindisha utaratibu wa kesi.
Uamuzi wa kukamatwa kwa maaskofu hao, ulitolewa baada ya wakili wa upande wa mashitaka, Meinrad D’souza, kuwasilisha maombi maalumu mahakamani hapo ili itoe adhabu kwa Dk Mokiwa na Hotay, kutokana na kukiukwa amri ya Mahakama.
Akisoma uamuzi kwa Kiswahili kwa takriban saa moja huku akisikilizwa kwa utulivu na mamia ya waumini wa Kanisa la Anglikana waliofurika mahakamani, hapo, Jaji Sambo alisema haihitaji elimu ya chuo kikuu kuona kuwa walichokifanya maaskofu hao wa Anglikana kuwa ni kudharau amri halali ya Mahakama.
Awali wakili D’Souza alisema kitendo cha Askofu Mokiwa kumsimika Hotay kimeingilia uhuru wa Mahakama na kushusha heshma ya Mahakama Kuu, kwani ilikishatoa agizo la kusitishwa kwa shughuli zozote za kuapishwa Hotay.
D’Souza alisema alichokifanya Askofu Mokiwa juzi ni kuvuruga mwenendo mzima wa kesi hiyo, ambayo inapinga mshitakiwa wa pili, Hotay kuapishwa kwani umri wake umegushiwa, na Katiba ya Anglikana inaeleza wazi kuwa Askofu anapaswa kuwa na umri unaoanzia miaka 40 lakini Hotay ana miaka 38 na hivyo tararibu zote za uchaguzi zilikiukwa.
Hata hivyo, mawakili wa upande wa Utetezi, Joseph Thadayo na Issa Mavura, waliiomba Mahakama itupilie mbali maombi ya kuchukuliwa hatua maskofu Mokiwa na Hotay kwa maelezo kuwa hawakuingilia mwenendo wa kesi hiyo.
Thadayo alimkabidhi Jaji Sambo tamko la Askofu Mokiwa ambalo linaeleza kilichotokea, kuwa Hotay alisimikwa kama Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania si wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro.
Mara baada ya uamuzi huo, Wakili Thadayo alisema ni wa Mahakama na hivyo hawana jambo la kufanya zaidi ya kutekeleza maagizo hayo.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mahakama yaamuru Askofu Mokiwa akamatwe
0 comments