IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
VITA ya kufutwa posho za wabunge na watumishi wengine wa umma, imechukua sura mpya, baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kusema kwamba Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe anaweza kufukuzwa ubunge kwa kutosaini karatasi za mahudhurio.Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge baada ya kuahirisha mkutano wa asubuhi, Makinda alisema Zitto anaweza kukumbwa na adhabu hiyo iwapo hatasaini karatasi za mahudhurio ambazo ndizo zinazothibitsha uwepo wa mbunge katika mikutano na vikao vyake.
"Kwa mujibu wa kanuni zetu, asipohudhuria mara tatu anakabiliwa na adhabu tena ya kufukuzwa bunge, hizo ndivyo kanuni zinavyosema." Hata hivyo, Zitto amepuuza kauli hiyo ya Spika akisema kwamba kama ni kwa ajili ya kukataa posho, yuko tayari kufukuzwa bungeni.
"Nitafanya hivyo tuone. Kanuni inasema mikutano mitatu mfululizo na siyo vikao vitatu mfululizo. Nitatumia uzoefu wangu wa siasa za wanafunzi kukwepa mtego wake. Lakini kama anadhani ni sawa kunifukuza ubunge kwa kukataa posho, nipo tayari," alisema Zitto.
Kauli ya Makinda inafuatia msimamo wa Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), kukataa posho za vikao na kwamba kwa kuwa kinachohalalisha yeye kulipwa posho ni karatasi za mahudhurio basi hatasaini karatasi hizo.Zitto alisema juzi mjini Dodoma kuwa, tangu Juni 10, mwaka huu alijibu barua ya Spika akikataa "kushinikizwa kuchukua posho za vikao" na kwamba hatua atakayoichukua ni kutosaini karatasi za mahudhurio katika vikao vyote.
Mahudhurio hayo ndiyo hulalalisha mbunge kupewa posho hizo.
"Kuanzia kikao cha juzi cha Tume ya Mipango, sikusaini na mkitaka nendeni mkaangalie ile orodha na kesho ndani ya Bunge sitasaini ili kuondoa uhalali wa kupewa posho hizo.
Sasa hapo tutaona watanilazimisha kwa njia gani," alisema Zitto.Lakini jana, Makinda alisema mujibu wa sheria malipo yote lazima yapelekwe kwa mbunge mwenyewe na kwamba ofisi yake haitafanya vinginevyo kwa wabunge ambao wamekataa posho hizo.Kanuni 143 (1) ya Bunge inabainisha kuwa kuhudhuria vikao ndiyo wajibu wa kwanza wa kila mbunge na kwamba asipohudhuria mikutano mitatu ya Bunge bila ruhusa ya Spika atapoteza ubunge wake.
Kwa maana hiyo, Zitto anaweza kufukuzwa Bunge ikiwa hatasaini mahudhurio ya vikao vyote vya Mkutano wa Bunge la Bajeti, vikao vya mkutano ujao ambao kwa kawaida huwa wa Oktoba na mkutano wa kwanza wa mwaka 2012.
"Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria Mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake kwa mujibu wa Ibara ya 71 (1) (c) ya Katiba na Spika ataiarifu Tume ya Uchaguzi," inaeleza kanuni hiyo namba 143 (2) ambayo iko chini ya sehemu ya 10 ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007.
Kadhalika, Kanuni hiyo ya 143 (3) inakwenda mbali zaidi na kusema kuwa mbunge asipohudhuria nusu ya vikao vya mkutano mmoja bila sababu ya msingi atapewa onyo.
Fasili za kanuni hizo zinamtaka mbunge asiyehudhuria vikao vya Bunge au vile vya Kamati za Bunge kupata kibali cha Spika katika Ofisi za Bunge hilo zilizopo Zanzibar, Dar es Salaam na Dodoma.Hata hivyo, kanuni hizo haziweki utaratibu wa kudhibiti mahudhurio ya wabunge na jukumu hilo ni kama limeachwa kwa Spika ambaye kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) amepewa uwanda mpana wa kuamua mambo mengine ambayo hayakutajwa moja kwa moja na kanuni hizo.
Kauli ya SerikaliKwa upande wake, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema jana kuwa wabunge wanaokataa posho ni wanafiki wanaotafuta umaarufu kwa umma."Mtu huwezi kusema kwamba eti posho hutaki halafu unasema zipelekwe Kigoma, kama suala ni kukataa posho ili kupunguza matumizi ya Serikali basi unazikataa kabisa," alisema Mkulo katika viwanja vya Bunge.
Tayari Mkulo alikuwa amesema kuwa ikiwa wapinzani watabeba ajenda hiyo, atawaandalia fomu kwa wale wasiotaka posho ili wakajaze na fedha hizo zipelekwe kwa wahitaji wa misaada mbalimbali.
Awali, Zitto alitaka fedha zake za posho zipelekwe katika taasisi ya Kigoma Development Inititive (KDI) lakini Juni 10 mwaka huu, Spika Makinda alimwandikia barua kimweleza kuwa ofisi yake haiko tayari kufanya hivyo na kusisitiza kwamba fedha hizo za posho zitaendelea kuwekwa katika akaunti yake benki.
Wanaharakati nao watakaposho za wabunge zifutwe
WANAHARAKATI wa taasisi mbalimbali nchini wameunga mkono uamuzi wa Chadema wa kukataa posho.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wanaharakati hao kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na ule wa Jumuiko la Wadau wa Maendeleo (Ado), wametaka posho hizo zifutwe ili fedha zipelekwe katika shughuli nyingine za maendeleoMkurugenzi Mtendaji wa Ado, Ntamilyango Buberwa alisema taasisi yake imepanga kuzunguka nchi nzima kutafuta watu milioni moja wanaounga mkono hoja hiyo ili walipeleke suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete.
"Baada ya kuwapata watu hao, tutawataka wasaini fomu maalumu ambayo tutaipeleka wa Rais Jakaya Kikwete kuelezea kutoridhishwa kwetu na jambo hilo. Ado itafanya na kumaliza kampeni hiyo kabla ya kusomwa kwa Bajeti ya Wizara ya Fedha.”
Alisema ni vyema wabunge wenye nia njema na taifa na ambao wamelenga kweli kuwawakilisha wananchi, wakaunga mkono hoja ya kufutwa posho hizo.Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema siyo haki kwa serikali kuendelea kuongeza posho kwa wabunge na maofisa wa ngazi za juu serikalini na kwamba suala hilo linapaswa kuzingatia hali halisi ya nchi na watu wake ambao alisema wengi wao ni maskini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mallya alisema kumekuwa na kasumba kwa serikali kuwalipa posho kubwa maofisa wa ngazi za juu na wabunge na kuwasahau wafanya kazi wa kiwango cha chini bila kuangalia hali halisi ya maisha.
“Nchi nyingine zinaongeza kiwango cha mshahara kwa kuangalia hali ya maisha yanavyokwenda, hapa kwetu ni tofauti, ukisafiri posho kwa mfanyakazi wa juu ni kubwa kuliko ya yule wa ngazi ya chini, posho inapaswa kuwa na uwiano sawa na si kuleta tofauti baina ya mtu na mtu.”
Alikosoa kitendo cha serikali kusamahe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa baadhi ya watumishi wa serikali na wafanya kazi wa taasisi zinazopata ruzuku kutoka serikalini akidai mpango huo utawanufaisha vigogo na si wale wa ngazi za chini.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Spika: Tutamfukuza Zitto
0 comments