IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
BAJETI ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/12, imechukua hatua kadhaa za kupunguza makali ya maisha kwa kutangaza kupunguzwa kwa kodi katika maeneo kadhaa na kuongezwa katika maeneo mengine.
Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, aliliambia Bunge jana kuwa Serikali inapandisha bei katika vinywaji baridi, bia, sigara, mvinyo, vinywaji vikali, tumbaku, faini kwa makosa ya usalama barabarani (notification).
Mkulo alisema kwa upande wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Serikali itasamehe VAT kwenye vipuri vya zana za kilimo; chakula cha kuku; nyuzi zinazotumika kutengeneza nyavu za kuvulia samaki; kwenye vipuri vya mashine za kunyunyiza na kutifua udongo na mashine za kupanda nafaka.
Nyingine ni kuanzisha utaratibu wa marejesho ya kodi kwenye mauzo ya rejareja kwa bidhaa za ndani zinazouzwa kwa abiria ambao si raia wa Tanzania wanaosafiri nje ya nchi.
Mkulo alisema utaanzia kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam na katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kwa kuanzia kwa Sh 400,000 na zaidi na utaanza Januari mwakani.
Nyingine ni kuondoa msamaha wa VAT kwenye kuuza na kupangisha majengo ya kuishi na nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Pia Serikali itaondoa unafuu wa VAT uliokuwa ukitolewa kwa mashirika yasiyo ya Serikali. Hatua hii haitahusu taasisi za kidini, alisema Mkulo alipowasilisha hotuba yake Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/12.
Mkulo alisema pia Serikali itatoa unafuu wa VAT kwa mashirika yasiyo ya Serikali kwa vifaa vya matumizi binafsi ya kawaida kama vile chakula, mavazi, na vifaa kama sabuni ambavyo vinatolewa msaada kwenye vituo mahsusi vya kulelea watoto yatima na shule.
Mkulo alisema pia katika VAT, Serikali itasamehe kodi hiyo kwenye vipuri vya zana za kilimo kama vile fyekeo, mashine za kukausha na kukoboa mpunga, mashine za kupandia mbegu na matrekta ya kukokota kwa mkono (power tillers) vitakavyotumika kwenye kilimo cha mkataba, makundi yaliyosajiliwa na vyama vya ushirika.
Kuhusu Kodi ya Mapato, Mkulo alisema Serikali itasamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa Serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye Bajeti ya Serikali.
Kufuta kodi ya zuio kwa usafirishaji wa samaki nje ya nchi kwa kutumia ndege za nje, hatua aliyosema kuwa inalenga kuhamasisha mauzo ya samaki nje ya nchi.
Katika kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha kuwa malipo yanafanyika kupitia benki na kuanza kutumia mfumo wa kulipa kodi kwa kutumia mfumo wa M-PESA kwa malipo ya kodi yasiyozidi Sh 500,000 ili kuondoa kero ya walipa kodi kukaa kwenye mistari.
Akifafanua kuhusu ushuru wa bidhaa, Mkulo alisema inapendekezwa kufanyiwa marekebisho ya kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo kutoka Sh 80 hadi Sh 40 kwa lita, ili kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa nchini.
Kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 50 badala ya Sh 120 kwenye mifuko ya plastiki za microns 30 na zaidi; kurekebisha kwa asilimia 10 viwango vya ushuru wa bidhaa isipokuwa mafuta ya petroli.
Bidhaa hizo ni vinywaji baridi kutoka Sh 63 kwa lita hadi Sh 69 kwa lita; bia inayotengenezwa na nafaka ya nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka Sh 226 kwa lita hadi Sh 249 kwa lita.
Bia nyingine zote, kutoka Sh 382 kwa lita hadi Sh 420 kwa lita; mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka Sh 1,223 kwa lita hadi Sh 1,345 kwa lita.
Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utatozwa Sh 420 kwa lita; vinywaji vikali kutoka Sh 1,812 kwa lita hadi Sh 1,993 kwa lita.
Kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara ambavyo ni sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka Sh 6,209 hadi Sh 6,830 kwa sigara 1,000.
Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75 kutoka Sh 14,649 hadi Sh 16,114; sigara nyingine zenye sifa tofauti na hizo za awali kutoka Sh 26,604 hadi Sh 29,264 kwa sigara 1,000.
Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara kutoka Sh 13,436 hadi Sh 14,780 kwa kilo na ushuru wa siga unabaki asilimia 30. Kwa mujibu wa Mkulo, hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh milioni 99,521.5.
Aidha, Mkulo alisema inapendekezwa kufanya marekebisho katika mgawanyo wa mapato yatokanayo na tozo ya kuendeleza ufundi stadi ya asilimia sita ili asilimia nne zipelekwe kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na asilimia nne zipelekwe Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Mkulo alisema inapendekezwa pia kusamehe ushuru wa stempu wakati wa umiliki wa mali unapohamishiwa katika chombo maalumu (kampuni) cha kutekeleza na kusimamia uzalishaji kipato kwa madhumuni ya kutoa dhamana zinazotegemea mali hiyo ambayo umiliki wake umehamishwa.
Mkulo alisema inapendekezwa kusamehe ushuru wa mafuta ya petroli yanayotumika kwenye kuendeshea meli na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi.
Ili kutatua tatizo la ucheleweshaji wa marejesho ya kodi kwenye mafuta yanayonunuliwa na kampuni za madini, TRA itaanzisha utaratibu wa kuweka kiasi cha fedha kwenye akaunti maalumu ambacho kinawiana na kiwango cha mahitaji ya mafuta kwa mwezi.
Aidha, kampuni itaruhusiwa kununua mafuta kwenye matangi ya kampuni za waagizaji wa mafuta bila kulipia kodi kwa kiwango cha fedha ilichoweka kwenye akaunti.
Kodi nyingine iliyoongezwa kwa mujibu wa Mkulo ni Mamlaka za Miji (Majiji, Manispaa na Miji), inapendekezwa zitoze Sh 50,000 kwa mwaka kwa kila aina ya biashara inayostahili kupewa leseni ya biashara (isipokuwa ya vileo) inayoendeshwa katika maeneo ya mamlaka hizo.
Halmashauri za wilaya zitoze na kukusanya ada ya leseni ya biashara ya Sh 30,000 kwa mwaka kwa biashara zinazoendeshwa katika maeneo ya miji midogo na vituo vya biashara na Halmashauri za vijiji zitoze na kukusanya Sh 10,000 kwa mwaka kwa kila biashara katika eneo lao.
Kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani, Mkulo alisema ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati wa uendeshaji gari barabarani (Traffic Notification Fee), inapendekezwa faini kupanda kutoka Sh 20,000 hadi Sh 50,000.
Mkulo alieleza pia kuwa katika Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Tanzania iruhusiwe kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano.
Kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye malighafi ya kutengeneza sabuni; kutenganisha malighafi zinazotambulika ili kutoa ushuru wa forodha kwenye malighafi za kutengeneza manukato na sabuni; kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye malighafi za kutengeneza maganda ya viberiti; kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye nyaya za chuma.
Kupunguza ushuru wa forodha kwenye mifuko ya plastiki ya kuhifadhia malighafi za matunda kutoka asilimia 25 hadi 10; kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye shaba ghafi; kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa waunganishaji wa majokofu ili walipe ushuru wa forodha wa asilimia 10 badala ya 25.
Kuendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 badala ya 25 kwenye mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 25; kuendelea kutoza ushuru wa forodha kwa asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwenye magari ya mizigo yenye uwezo wa kati ya tani 5 na tani 20.
Kuendelea kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye mnagari ya mizigo yenye uwezo zaidi ya tani 20; kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 badala ya 25 kwenye mabasi yanayoingizwa kwa ajili ya mradi wa mabasi ya Jiji la Dar es Salaam, na kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye pikipiki maalumu za kubeba wagonjwa.
Kwa mujibu wa Mkulo, hatua hizo za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa kuanzia Julai mosi, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
Mkulo alisema Bajeti inaonesha kuwa jumla ya Sh bilioni 13,525.9 zinahitajika kutumika katika kipindi hicho cha mwaka 2011/12.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 8,600.3 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha Sh bilioni 3,270.3 za mishahara ya watumishi wa Serikali, taasisi na wakala wa Serikali na Sh bilioni 1,910.4 kwa ajili ya Mfuko Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mkulo alisema Sh bilioni 4,925.6 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo Sh bilioni 1,871.5 ni fedha za ndani na Sh bilioni 3,054.1 ni fedha za nje.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Ni Bajeti nafuu, vinywaji bei juu
0 comments