Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - ‘Wakuu wa shule wanachangia kushuka ufaulu’

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Prof. Hamis Dihenga (kulia) akiongea na waandishi wa habari jijini
SERIKALI imekiri kuwa sehemu ya kuporomoka kwa ufaulu wa wanafunzi katika miaka ya hivi karibuni ni baada ya kushindwa kuwawezesha walimu wakuu na shule zao kufanya vizuri.

Hata hivyo, imewarushia lawama wakuu wa shule za sekondari nchini kuwa sehemu nyingine ya kuporomoka ufaulu huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Hamis Dihenga alisema hayo jana Kibaha, mkoani Pwani alipofungua mafunzo ya siku tatu kwa walimu wakuu 50 wa shule za sekondari Tanzania Bara zilizofanya vibaya katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.

Alisema, Serikali imekuwa kikwazo kwa walimu kwa namna inavyoshughulikia changamoto zao hasa katika shule za kata lakini akasisitiza kuwa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) na ule wa msingi (MMEM), imejizatiti kushughulikia kero hizo.

Alitaja vikwazo hivyo kuwa ni pamoja na kutowezeshwa kiutendaji, miundombinu mibovu, uhaba wa wakaguzi wa elimu, vifaa vya kazi, mazingira ya kazi na uhaba wa walimu, mambo aliyosema kuwa yanachangiwa na ufinyu wa bajeti.

“Hii si semina kwa ajili yenu bali na mafunzo ya kuelimishana na kubalidishana mawazo kwa pamoja kuhusu namna ya kuboresha elimu, matokeo mabaya ya mwaka jana sababu ni sisi na ninyi lakini ni wazi kuwa Serikali imewakwaza kwa sehemu kubwa na ninyi mmeshindwa kutekeleza wajibu wenu kutokana na makwazo hayo,” alisema Profesa Dihenga.

Profesa Dihenga aliwaonya baadhi ya walimu wakuu wanaowagawa walimu kwa makundi shuleni, ili kupata wafuasi wa kuwafichia maovu ikiwemo kushinda katika vikao vya vyama vyao vya walimu na kusahau wajibu wao wa kusimamia taaluma shuleni.

Aliwataka wakuu wa shule kuacha kuleana kwa kuwakumbatia walimu wasio na uadilifu na viwango vinavyotakiwa kitaaluma kwani kufanya hivyo ni kuharibu kizazi cha Tanzania.

“Nasikia kuna watu wenye vyeti feki wanaotuharibia fani, walimu msiwalee hao ndiyo wanaotuharibia taaluma, maadili ya kazi yamepungua na huu ni wakati wa kung’oa magugu.

“Serikali inajivunia shule za kata japo wengi wanazibeza, mwaka 2009 asilimia 50.1 ya waliofaulu kuingia kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walitoka huko,” alisema Dihenga.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Jumanne Sagini alisisitiza umuhimu wa walimu wakuu kupimwa kiutendaji baada ya kuwezeshwa atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake, aondolewe na kuwajibishwa.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wenzake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mkera wilayani Ilala, Rhodina Chalila alisema Serikali haina sababu yoyote ya kuwalaumu walimu wala vyama vyao kwa kuwa haijawawezesha kufanya vizuri.

0 comments

Post a Comment