IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Mwanza, Boniphace Magembe (32) amepandishwa kizimbani kwa mashitaka ya kujipatia fedha Sh milioni 20 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wafanyabiashara wawili wa jijini hapa.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Angelo Rumisha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mwanza, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Paskal Marungu alidai kuwa Julai 10, mwaka 2009, mshitakiwa alijipatia Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara wa jijini hapa, Edward Njau.
Marungu alidai kuwa mshitakiwa alichukua fedha hizo kwa makubaliano ya kumpangisha chumba cha biashara katika moja ya vyumba vinavyomilikiwa na CCM mkoani Mwanza wakati akijua kuwa hakuwa na mamlaka hayo.
Katika mashitaka mengine, Marungu alidai kuwa Agosti 20 mwaka 2009, mshitakiwa alijipatia fedha Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara mwingine, Iman Abdul kwa makubaliano kama hayo ya awali.
Hata hivyo mshitakiwa alikana mashitaka hayo na baadaye kuomba dhamana ambayo ilikubaliwa na hakimu kwa masharti ya kulipa fedha taslimu Sh milioni 10.
Hakimu Rumisha alisema kinyume cha hapo, wadhamini wake waweke dhamana ya mali isiyohamishika na pia mshitakiwa alitakiwa kutosafiri nje ya Mkoa wa Mwanza bila ruhusa ya Mahakama hadi kesi yake itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Wadhamini wa mshitakiwa huyo waliwasilisha mahakamani hapo hati ya mali isiyohamishika ambayo ni kiwanja chenye thamani ya Sh milioni 37.6.
Hata hivyo, Marungu alipoikagua alibaini kuwa ilikuwa na utata kwa kuwa tarehe iliyoandikwa katika hati hiyo ilikuwa inaonesha kutayarishwa Juni 4, mwaka huu wakati kesi hiyo ilisomwa Juni 3, mwaka huu.
Marungu aliiomba Mahakama impatie muda ili achunguze nyaraka hizo kama ni halali au vinginevyo.
Hakimu Rumisha alikubaliana na Marungu na kukataa hati hizo na kuongeza, "hapa mahakamani kuna kesi nyingi zinasumbua kutokana na sababu kama hizi, wadhamini na washitakiwa wamekuwa wakileta hati na baada ya washitakiwa kupewa dhamana hutoroka kwa kujua kuwa hati walizozileta ni za kughushi."
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 6, mwaka huu na mshitakiwa alirudishwa rumande hadi kesi hiyo itapotajwa tena.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mwenyekiti UVCCM Mwanza kortini kwa kutapeli
0 comments