Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Chadema, CCM mwafaka Arusha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HATIMAYE mgogoro wa uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Arusha umepata ufumbuzi baada ya pande zinazohusika kufikia muafaka wa kupokezana madaraka.


Katika muafaka huo uliofikiwa baada ya majadiliano yaliyodumu kwa zaidi ya miezi miwili CCM kitaendelea kushikilia nafasi ya umeya huku Chadema kikipewa unaibu kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.


TLP kitachukua nafasi ya unaibu meya kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya ile minne ya Chadema kukamilika


Makubaliano mengine ni Chadema na CCM kuongoza kwa kupokezana kamati mbili za kudumu za uchumi, elimu na afya na ile ya mipango miji, mazingira na ujenzi ambapo kikao cha jana kiliwachagua John Bayo (Chadema) na Ismail Katamboi (CCM) kuongoza kamati hizo.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Manispaa kilichomchagua diwani wa Kimandolu, Estomi Mallah kuwa naibu meya, mwenyekiti wa kamati ya muafaka, Michael Kivuyo alisema uamuzi huo umejali maslahi ya umma na kuweka pembeni itikadi na maslahi ya vyama.


“Tumekubaliana kusahau yote yaliyotokea nyuma, tumeanza ukurasa mpya kwa maslahi ya wananchi ambao wanahitaji kuunganishwa na viongozi wao katika harakati za maendeleo ambayo hayajali itikadi,” alisema Kivuyo.


Kwa upande wake, Meya liyekuwa akipingwa uchaguzi wake, Gaudance Lyimo alisema “Nimeufurahia muafaka huu. Kimsingi tungeweza kuendelea na shughuli zote, lakini ingekuwa ngumu kutekeleza majukumu yetu katika hali iliyokuwepo,”


Alisema ni afya kwa maendeleo ya Manispaa ya Arusha kufanya kazi pamoja na madiwani wa vyama vyote, hasa Chadema yenye idadi kubwa kwa maendeleo ya umma uliowaamini na kuwachagua.


Meya Lyimo ambaye ni diwani wa Kata ya Olorieni aliwagiza watendaji wote wa Manispaa kuwapa ushirikiano unaostahili madiwani wote katika utekelezaji wa majukumu yao bila kubagua wala kuangalia itikadi za vyama vyao.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha aliyekuwa mmoja wa wajumbe walioshiriki vikao vya kutafuta muafaka huo alisema tatizo la uchaguzi wa meya na mauaji yaliyotokea yalikuwa ni jambo la kusikitisha ambalo katika muafaka huo wamezingatia makubaliano yatakayohakikisha hayatajirudii siku zijazo.


“Natoa wito sasa kwa madiwani wote kutekeleza wajibu wao kuwakilisha na kutetea maslahi ya wananchi bila kujali itikadi za vyama vyao kwai kiongozi akishachaguliwa anawakilisha watu wote wenye itikadi tofauti na hata wasiokuwa na vyama,” alisema Mushi.


Naibu Meya mpya kwa upande wake, aliahidi ushirikiano wa dhati kwa Meya na madiwani wote ili kuharakisha na kufanikisha maendeleo ya Manispaa ya Arusha yaliyokwama kwa kipindi kirefu kutoka na mgogoro uliokuwepo.


“Naamini sasa mstahiki Meya atapata usingizi baada ya muafaka huu kwani alikuwa akiwiwa vigumu kutekeleza majukumu yake. Wananchi wa Arusha sasa watarajie kuona na kupata maendeleo yaliyokusudiwa,” alisema Mallah.


Zaidi ya Mkuu wa Wilaya na mwenyekiti wao, Kivuyo, kamati ya kutafuta muafaka wa mgogoro huo uliosababisha vifo vya watu watatu Januari 5, mwaka huu, iliundwa na wajumbe 10, watano kutoka CCM na wengine Chadema.


Kutoka Chadema wajumbe walikuwa wa kamati hiyo iliyoanza vikao vyake tangu Aprili mwaka huu walikuwa John Bayo, Samson Mwigamba, Efatha Nanyaro na Amani Golugwa wakati CCM iliwakilishwa na Abdulrasul Tojo, Ismail Katamboi, Lilian Mmasi, Karim Moshi, Musa Sunja na Meya Lyimo.


Baada ya kikao cha muafaka na uchaguzi wa naibu meya na wenyeviti wa kamati mbili za kudumu, madiwani wote walisimama, kushikana mikono na kuimba wimbo maarufu wa kuhimiza mshikamano maarufu kwa jina la ‘solidarity forever’.


Wimbo huo uliashiria mwisho wa mgogoro na mwanzo wa ushirikiano.

0 comments

Post a Comment