WABUNGE wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, wamehoji sababu za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuingia mkataba waliouita wa ovyo na hatari na Kampuni ya Star Media ya China wakisema kuwa ni kama kitanzi kwa shirika hilo la umma.
Wakichangia katika taarifa ya hali ya TBC na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dar es Salaam jana, wabunge hao kwa pamoja walionya kuwa mkataba huo unaweza kuwa kaburi la kuzika shirika hilo siku za usoni.
Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola aliyeichambua ripoti hiyo kwa kina huku akimbana Mwenyekiti wa Bodi ya TBC, Wilfred Nyachia kuhusu kisingizio kwamba shirika hilo lilipata hati yenye shaka kutokana na mali za ubia kati yake na Star Media kutokaguliwa.
Lugola akichambua kipengele kwa kipengele, alipinga madai ya Nyachia kwamba hati hiyo ilitokana na wabia wao, Star Media na kusisitiza: "Ubia unaouzungumzia hapa ni pande mbili, sasa kama ni hati yenye mashaka na nyinyi TBC mmo. Ninyi ndiyo mliingia mkataba huu."
Mbunge huyo alisema mkataba huo hauko wazi, kitu ambacho kinaweza kufananishwa kama mazungumzo tu kati ya watu wawili wanaofahamiana.
Alisema Star Media, kwa mujibu wa mkataba huo, inao uwezo wa kuuza hisa zake asilimia 65 na kujitoa, kitu ambacho ni cha hatari endapo atakuja mbia mwingine ‘mwendawazimu.’
Alisema hata vipengele vya mkataba kumbana mbia kwa ajili ya ulipaji kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haviko wazi na kuongeza, hiyo inaweza kuwa kama mchezo wa baadhi ya kampuni kuingia kisha kubadili majina na mamlaka hiyo ya mapato kukosa mapato.
Akitolea mfano alisema Kampuni ya Celtel iliwahi kuingia nchini na kujitanua kwa kasi kwa kutumia miundombinu ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), ikitumia mgongo wa ubia kati ya kampuni hiyo ya umma na MSI/Detecon.
MSI Detecon iliwahi kununua hisa asilimia 35 za TTCL, huku ikiendesha menejimenti ya kampuni hiyo nyeti ya nchi, lakini hadi inaondoka Februari 23, 2005 baada ya kumalizika ukiritimba wa miaka minne iliacha deni la takriban Sh20 bilioni, huku Celtel sasa ikiwa imekua kwa kasi.
Luoga alisema TBC pia ilikiuka taratibu za ununuzi kwa kutumia zaidi ya Sh8 bilioni ambazo sehemu zilinunua mafuta katika Kituo cha Victoria bila mkataba wa maandishi, lakini menejimenti ikitoa sababu kwa CAG, kwamba uamuzi huo umejikita kiuchumi zaidi kwani umekwepa foleni na umbali wa kilomita kumi na moja kwenda Wakala wa Huduma na Ununuzi Serikalini (GPSA) Kurasini, ambao wana mkataba na Serikali.
Baada ya Mwenyekiti wa kikao hicho, Deo Filikunjombe kuona maswali ni mengi kuliko majibu, aliamua kusitisha kikao huku akiahidi kuwaita Makatibu Wakuu wa Hazina, Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo na Mtendaji mkuu wa TBC, ili kupata maelezo ya kina kuhusu mkataba huo.
Filikunjombe pia alihoji juhudi zinazofanywa na TBC kukusanya deni la Sh5.5 bilioni na kuonya kuwa kama hakutakuwa na jitihada za kushughulikia suala hilo, shirika hilo litakufa siku za usoni akisema lilianza vizuri lakini sasa linakwenda kwa kusuasua.
Awali, Nyachia aliahidi kuwa bodi yake itahakikisha hati chafu na zenye shaka hazipo tena na kuwa atasimamia taratibu za utawala bora katika ununuzi na kuibana Star Media iweze kwenda sawa na mkataba husika.
0 comments