Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - KESI YA EPA: Maranda, Farijala wafungwa miaka 5

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana iliwahukumu kifungo cha miaka mitano jela kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala Hussein baada ya kupatikana na hatia kwenye mashtaka sita kati ya manane ya kujipatia fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).Mbali ya kifungo hicho, pia wametakiwa kurudisha Sh1.8 bilioni walizochota kwenye akaunti hiyo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na endapo watashindwa kufanya hivyo, mali zao zitakamatwa na kufilisiwa.

Hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa mbili, ilisomwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilvin Mgeta kwa niaba ya jopo la mahakimu watatu waliokuwa wakiisikiliza. Mahakimu wengine ni Focus Bampikya na Saul Kinemela.

Maranda na mwenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwamo ya kula njama, kughushi, wizi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia ingizo la fedha kwa njia ya udanganyifu kwenye akaunti kiasi cha Sh1.8 bilioni, mali ya BoT wakijaribu kuonyesha kuwa Kampuni yao ya Kiloloma & Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la Kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mgeta alisema katika shtaka la pili la kughushi hati za usajili wa kampuni, Farijala atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela, katika shtaka la tatu la kughushi hati ya makubaliano, Maranda na Farijala wote watatumikia kifungo cha miaka mitano jela.Alisema katika shtaka la nne ambalo nalo pia ni la kughushi, wote watatumikia kifungo cha miaka mitano jela.


Katika shtaka la tano la kuwasilisha nyaraka za kughushi BoT, Maranda atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
Katika shtaka la sita, Hakimu Mgeta alisema wote watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kwenye shtaka la nane la kujipatia ingizo kwa njia ya udanganyifu kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Hakimu Mgeta
Baada ya kumaliza kusoma hukumu hiyo, Hakimu Mgeta alifafanua kuwa vifungo vyote vitakwenda sambamba, hivyo kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Hakimu Mgeta kwa niaba ya jopo hilo alisema wote wana kesi ya kujibu kwenye shtaka la pili, tatu, nne, tano, sita na la nane.Alisema katika shtaka la kwanza ambalo ni la kula njama ya kutenda kosa la wizi na la saba la wizi, yamefutwa kwa sababu mahakama imewaona hawana hatia baada ya mashahidi tisa wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kama ni kweli walifanya makosa hayo.

Baada ya mahakama kuwatia hatiani, Wakili Mkuu wa Serikali, Boniface Stanslaus aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa hao kwa kuzingatia kiasi cha fedha walizochukua na madhara yaliyowafika wananchi hasa ikizingatiwa kwamba hiyo ni kesi ya kwanza ya EPA kutolewa hukumu.

“Naomba mahakama itumie mamlaka yake chini ya kifungu cha Sheria cha 358 (1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kutoa amri kuwa washtakiwa hawa warudishe hela kwa mwenyewe ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Stanlaus wakati akiwasilisha maombi yake mahakamani hapo.

Wakili Magafu
Hata hivyo, Wakili wa Maranda, Majura Magafu alipinga hoja hiyo na kusema kuwa makosa yanayowakabili wateja wake hayapo chini ya kifungu hicho cha sheria, hivyo hawapaswi kurejesha fedha hizo.
“Waheshimiwa kifungu cha 358 cha Kanuni ya Uendeshaji wa Kesi za Jinai iliyorekebishwa mwaka 2009, makosa ambayo yanamtaka mtu anayedaiwa kurudisha fedha zinazodaiwa kuibwa ni yale yaliyopo kwenye sura ya 27 na 32 ya Kanuni ya Adhabu," alisema Wakili Magafu.

Magafu alisema makosa wanayowakabili wateja wake kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 61 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, ni ya kughushi na kwamba yapo kwenye sura ya 36 ambayo adhabu yake inasomwa kwenye sura ya 37 ya Kanuni ya Adhabu.

Alisema kosa la kujipatia ingizo kwa njia ya udanganyifu lipo chini ya kifungu cha sheria cha 305 na kwamba inapatikana kwenye sura ya 31 ya Kanuni ya Adhabu, hivyo kutokana na hali hiyo, aliomba ombi la upande wa mashtaka la kutaka wateja wake waamuliwe kurejesha fedha zinazodaiwa kuibwa lisiangaliwe na mahakama kwa sababu halisemwi katika  vifungu vilivyotajwa kisheria.

Wakati Magafu akiendelea kutoa hoja zake, Wakili Stanslaus aliingilia kati na kusema kuwa wao waliomba washtakiwa hao waamuliwe kulipa fedha hizo wanazodaiwa kuziiba chini ya kifungu cha sheria cha 358 (1) kwa sababu washtakiwa hao pia wanakabiliwa na shtaka la kujipatia ingizo kwa njia ya udanganyifu.

Akiendelea kuwasilisha hoja zake, Magafu alisema kuwa: "Ni rai yetu tunaomba washtakiwa wasipewe amri iliyoombwa ya kutaka warejeshe hizo fedha na kwamba kama serikali itaona wana haja ya kurudisha hizo fedha kuna njia mwafaka wanayotakiwa kufuata wapate fedha hizo."

Aliiomba mahakama iwaonee huruma kwa sababu hayo ni makosa yao ya kwanza, hawajawahi kutiwa hatiani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba wanategemewa na familia zao zenye watu wengi.

‘Waheshimiwa kama mlivyoona, hati ya makubaliano iliyopelekwa BoT ambao walithibitisha kuwapo kwa mawasiliano na hatimaye walitoa fedha hiyo inayoonyesha kuna watu walitumika kuwapotosha washtakiwa," alisema Magafu.

Aliongeza kuwa Maranda na Hussein ni wagonjwa wanaosumbuliwa na ugonjwa wa figo hivyo kutokana na hali hiyo, aliiomba mahakama kwa mamlaka iliyopewa, chini ya kifungu cha 138 cha Kanuni ya Adhabu, pamoja na kuwatia hatiani washtakiwa  bado inaweza kuwaachia huru kulingana na mazingira.Aliiomba mahakama wakati inapotoa adhabu iangalie kifungu hicho cha sheria.

Kutolewa hukumu
Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, ilipotimia saa 6:00 mchana, Hakimu Mgeta  aliwasimamisha washtakiwa na kuwaeleza kuwa Jopo la Mahakimu limesikiliza hoja zilizotolewa na wakili wao, Magafu na limezizingatia na kuziheshimu lakini kulingana na uzito wa kesi:
“Tumepima pamoja tumefikia uamuzi wa kutoa adhabu yenye kuonya, watatumikia kifungo cha miaka mitano jela, kuhusu kurudisha fedha zilizochukuliwa tumesikiliza hoja za Magafu, lakini tunatofautiana naye, hivyo washtakiwa wote wanatakiwa kurejesha kiasi hicho cha fedha na wasipofanya hivyo, mali zao zitakamatwa na kufilisiwa,” alisema Mgeta.

Hakimu huyo alisema kama upande wa utetezi haukuridhika na hukumu hiyo, haki ya kukata rufaa ipo wazi.
Mara baada ya kumaliza kutolewa kwa hukumu hiyo, washtakiwa walipelekwa gereza la Ukonga kuanza kutumikia vifungo vyao.

Washtakiwa kutakata rufaa?
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hukumu hiyo, Wakili Magafu alisema wateja wake hawajaridhika na hukumu hiyo, hivyo wataomba mwenendo mzima wa kesi hiyo ikiwamo hukumu ili waisome halafu watajua cha kufanya.
Awali, hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Aprili 29, mwaka huu lakini iliahirishwa.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya Magafu kufunga ushahidi wao mara baada ya washtakiwa hao wawili kumaliza kutoa utetezi.
Akifunga ushahidi wa utetezi, Magafu alidai kuwa wanaamini mahakama imewasikiliza mashahidi tisa wa upande wa mashtaka na wateja wake kwa umakini hivyo wanaiachia itoe uamuzi wake.

Baada ya Magafu kutoa maelezo hayo, Wakili Stanslaus alisema kuwa hata wao (Serikali) wanaiachia mahakama itoe uamuzi.
Awali, Machi 23, mwaka 2009 Stanslaus  ambaye alikuwa akisaidiana na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis walifunga ushahidi huo mara baada ya shahidi wa tisa, Steven Mwakalukwa (54), ambaye ni Mkaguzi wa Mahesabu ya Ndani katikaBoT, kumaliza kutoa ushahidi wake.

Mbali ya kesi hiyo iliyomalizika jana, Maranda anakabiliwa na kesi nyingine nne za aina hiyo katika mahakama hiyo wakati Farijala anakabiliwa na kesi tatu pia za aina hiyo ambazo zitaendelea kusikilizwa wakati wakiendelea kutumikia kifungo vyao.

0 comments

Post a Comment