Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Makamba: Mgawo wa umeme umeliweka taifa rehani

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba amesema taifa lipo rehani kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea akisema unazorotesha uchumi wa nchi.Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Makamba alirejea kauli yake kuwa, kamati yake itakwamisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, endapo haitatoa majibu ya kuridhisha juu ya tatizo la umeme linaloendelea nchini.

“Sijawahi kuona duniani kote, eti kutokana na ukarabati, uzalishaji unasimamishwa kabisa! Ninachoelewa ni kwamba ukarabati hufanywa kwa awamu huku uzalishaji ukiendelea,” alisema Makamba na kuongeza:“Gesi ipo chini ya TPDC (Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania), lakini mwenye uamuzi wa kusema nani auziwe, kwa kiasi gani ni Songas. Wanaweza kufika mahali wakasema, wewe una ugomvi na fulani, mimi sipendi kwa hiyo nasimamisha uzalishaji.

Katika hili ni wazi kuwa nchi ipo rehani.”Alisema Songas wana mitambo minne yenye uwezo wa kuzalisha migawati 120, ambazo zinatumia mafuta ya ndege pamoja na dizeli, lakini nazo zimezimwa huku nchi ikiendelea kupata hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na mgawo unaoendelea.

Alisema Tanesco imetoa mabilioni ya shilingi ili kuikarabati mitambo hiyo iweze kufanya uzalishaji kwa kutumia mafuta hayo, lakini cha kushangaza ni kuwa wananchi wanaendelea kuumia na mgawo bila kupata maelezo ya kina juu ya kutowashwa kwa mitambo hiyo.“Kuna mashine za kuzalisha megawati 120 bila gesi kwa nini zisiwashwe? Mashine mbili zina uwezo wa kuzalisha megawati 20 kila moja na nyingine mbili megawati 40 kila moja.

Tukumbuke kuwa mafuta ya ndege yameondolewa kodi kwa hiyo hakuna mafuta yanayopatikana kwa bei rahisi kama hayo, lakini ile mitambo imezimwa tu, kwa nini isiwashwe?”

“Nadhani wenzetu (wawekezaji) hawaoni umuhimu, ndiyo maana wamezima.”Makamba alisema Februari, mwaka huu kamati yake ilipata taarifa juu ya kuharibika kwa kiasi kikubwa kwa visima vya gesi na ilitaka ufafanuzi kwa TPDC, shirika hilo la umma liliipatia kamati yake ripoti likidai kuwa havina tatizo lolote.

“Tutataka kujua kama TPDC walitudanganya, kwa sababu walisema visima vipo safi na kwamba hakuna tatizo lolote litakalotokea.”

Kutokana na hali hiyo alisema kuna kila sababu ya mkataba wa uzalishaji gesi na usambazaji baina ya Tanesco, TPDC na Songas uangaliwe upya ili kuangalia jinsi ya kuondoa ukiritimba uliopo.

Makamba ambaye pia ni Katibu wa Sekretarieti ya CCM wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa KImataifa alisema gesi hiyo ambayo ni rasilimali ya nchi, imekuwa haimnufaishi Mtanzania, bali wawekezaji.

Alisema serikali inatakiwa kumiliki miundombinu ya gesi kwa asilimia 100 au kumiliki kwa ubia, kuliko hivi sasa yote inamilikiwa na mtu mmoja.Alisema mpango wa Tanesco kukodisha mitambo ya umeme itakayozalisha megawati 260 ifikapo Juni mpaka Julai, mwaka huu kwa sasa umekwama.Alisema katika kujaribu kufanikisha suala hilo, Tanesco ilitangaza zabuni na kualika mashirika 21 na 17 tu ndiyo yaliyochukua fomu na ni manne pekee yaliyorejesha.

“Taarifa zilizopo ni kwamba, katika hayo makampuni manne ni moja tu, lililokidhi lakini mpaka sasa hakuna zabuni yoyote iliyotolewa, maana yake ni kuwa hizo megawati haziwezi kupatikana mpaka kufikia Julai na watu wamekaa kimya hawafikiri hata kuwaeleza wananchi kuwa ule mpango umefikia mahali fulani,” alisema Makamba.

Alisema kutokana na hali hiyo na jinsi watu wanavyozidi kuchukua hatua za kumaliza tatizo la umeme nchini, ni wazi kuwa Wizara ya Nishati na Madini  pamoja na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) wanafanya mzaha juu ya tatizo la umeme lililopo.“Katika mpango huu wa kukodisha hii mitambo, Tanesco walikuwa watumie zaidi ya Sh500 bilioni.

Kwa sasa tayari serikali ilikuwa imekataa kutoa fedha kwa kazi hiyo, kwa makampuni yote yaliyorejesha hizo fomu hakuna kampuni iliyokuwa ikiuza uniti moja chini ya Sh1,000 wakati Tanesco wao hawauzi hizo uniti kwa zaidi ya Sh100, kwa hiyo hapa kuna tatizo la fikra na mpango.”

Kwa jinsi hali ilivyo sasa, kwa siku za usoni tatizo la umeme litakuwa kubwa maradufu kwa sababu ukame mkubwa zaidi upo kuanzia Juni,” alisema Makamba.Alisisitiza kuwa, pamoja na kuwepo kwa mikakati mingi ya kumaliza tatizo la umeme nchini, tatizo kubwa linaloonekana ni kukosekana kwa mawasiliano baina ya serikali na wananchi.

“Hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa Waziri wa Nishati ni tatizo, lakini ukiangalia pia jinsi hali ilivyo unaweza kusema ndiyo,” alisema Makamba.Akizungumzia ratiba ya vikao vya kamati yake vitakavyoanza leo, Makamba alisema itaonana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Kesho itakutana na Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini. Katika kikao hicho kamati yake itaelezwa jinsi mapendekezo 30 ya kamati hiyo ya kupambana na tatizo la umeme yalivyofanyiwa kazi.“Tutataka watueleze wana mpango gani wa kumaliza tatizo la umeme lililopo. Kwa kweli hatutakubali kupata majibu rahisi,” alisema Makamba.

Machi mwaka huu, Makamba alisema kamati yake imetoa mapendekezo 30 ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme ikiwa ni pamoja na serikali kununua mitambo ya Dowans.Mapendekezo mengine ni serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi (Hazina) kuagiza na kununua mafuta haraka iwezekavyo na kwa wingi kwa ajili ya mitambo ya IPTL ambayo kwa sasa inachangia megawati 10 hadi 50 wakati ina uwezo wa kuzalisha hadi megawati 90 na kuzipeleka katika Gridi ya Taifa.

Alisema ikiwa serikali itaagiza mafuta kuna uwezekano wa tatizo la umeme kupungua kwa asilimia kubwa na kuwezesha wenye viwanda kuongeza uzalishaji.

Alitaka pia serikali izungumze na wawekezaji wa migodi minne ya madini yenye mitambo ya kuzalishia umeme wa megawati 125 ambayo kwa sasa haipati mgawo wa umeme kutokana na makubaliano ya serikali na wawekezaji hao.

0 comments

Post a Comment