Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - TRA 'wambana' Dk Slaa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), 'imemkaba kooni' Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) Dk. Willibrod Slaa, kufuatia tuhuma alizozitoa dhidi ya ofisa wa mamlaka hiyo kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha.

Hivi karibu, gazeti moja lilimkariri Dk. Slaa akitaja majina ya watu mbalimbali wanaotuhumiwa kuwa ni mafisadi.Pia wakati akihutubia katika mkutano wake wa hadhara mkoani Tabora, alitaja orodha ya watuhumiwa hao akiwamo oafisa wa TRA, Placidus Luoga.Gazeti hilo lilimkariri Dk. Slaa akidai kuwa Luoga aliingizia serikali hasara ya Sh800 bilioni kwa  kuzuia  magari ya Kampuni ya Tango, Transport ya jijini Dar es Salaam kwa miaka 10 kwa kisingizio cha kutolipa kodi.

Alidai kuwa kitendo hicho, kiliilazimisha kampuni hiyo, kufungua kesi mahakamani ambako ilishinda na serikali kuamriwa kuilipa kiasi hicho cha fedha.Gazeti hilo lilimkariri kiongozi huyo wa Chadema akidai kuwa tayari serikali imeshailipa kampuni hiyo Sh500 milioni.

Hata hivyo jana TRA kupitia taarifa yake iliyotolewa na Idara ya Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi, imekanusha madai hayo na kuyaita kuwa uzushi tu wa Dk Slaa na kumtaka atoe uthibitisho wa madai yake hadharani.

"Huu ni uzushi unaopaswa kulaaniwa  vikali kwa sababu unapotosha wananchi na hasa wasomaji wa magazeti.  Dk. Slaa atoe nakala ya hukumu hiyo ili wananchi wamwamini.  Bila kufanya hivyo kutaonyesha kuwa ametoa habari za uongo kwa kusingizia mahakama," ilisema taarifa.

Taarifa hiyo ilimtaka Dk. Slaa kutoa vielelezo vya maelezo yake hadharani na kwenye mkutano ili awathibitishie wananchi kuwa alichosema ni cha kweli.

TRA ilisema kama Dk. Slaa atashindwa kufanya hivyo, ni dhahiri kuwa yeye si mtu makini na ni mtu mwenye nia ya kupotosha umma wa Watanzania na kuchafua heshima ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.

"Kudanganya watu kwa siri au hadharani ni aina mojawapo ya aina nyingi za kutokuwajibika. Kutokuwajibika kuna sura nyingi na uongo ni mojawapo. Dk. Slaa lazima ajisafishe na hili," ilisisitiza taarifa ya TRA. Taarifa hiyo ya TRA ilisema  Luoga hajawahi kuzuia wala kukamata magari yanayodaiwa na Dk. Slaa.

"Hakuna ofisa wa TRA mwenye akili timamu anayeweza kukaa na mali ya mtu anayedaiwa kodi kwa miaka 10 huku akijua kuwa anatakiwa kukomboa kodi hiyo. Anatakiwa kuuza mali hiyo ili serikali ipate kodi;  Kwa afisa yoyote aliye kwenda shule hawezi kufanya hivyo akishuhudia mlipa kodi anapeleka kesi Mahakamani ambako atapata fidia ya sh.800 bilioni," ilisema sehemu ya taarifa.


Ilisema hata kama ofisa huyu hajaenda shule, lakini hawezi kuhusika na mpango kama huo.
Ilisemwa mujibu wa maelezo ya Dk. Slaa,mahakama iliona kuwa Tango Trasport ya Dar es Salaam ilipata hasara ya wastani wa Sh80 bilioni kwa mwaka."Kwa biashara ya kawaida Tanzania, mahesabu kama haya hayawezi kuingia vyema kichwani kwa yeyote mwenye busara," imesisitiza TRA.

Hata hivyo TRA katika taarifa yake ilisisitiza kuwa  Luoga haifahamu Kampuni ya Tango Transport ya jijini Dar es Salaam ambayo magari yake  yamewahi kuzuiwa kwa muda wa miaka 10.

Imefafanua kuwa kumbukumbu zilizoko TRA zinaonyesha kuwa kampuni ya  Tango Transport ni ya Arusha na kusisitiza kwamba hakuna taarifa zinazoeleza kuwa TRA imewahi kukamata magari ya kampuni hiyo kwa miaka 10.
Juhudi za gazeti hili kumpata Dk. Slaa kuzungumzia taarifa ya TRA hazikufanikiwa kwa kuwa simu yake ya mkononi haikuwa hewani.

0 comments

Post a Comment