Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Babu ataka apelekewe wafungwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MCHUNGAJI Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila ameomba wafungwa waliopo magerezani na watoto yatima ambao ni wagonjwa wapelekwe Samunge ili wapatiwe kikombe cha tiba.
Mwasapila ambaye anatoa tiba ya magonjwa Sugu aliliambia Mwananchi kijijini Samunge jana kuwa, Mungu amemwonyesha uhitaji wa tiba kwa watoto yatima na wafungwa.

"Nimeonyeshwa ujio wa yatima kwa wingi hapa, lakini siwaoni, naomba Serikali na wengine wanaohusika wawalete wapate dawa,"alisema Mwasapila na kuongeza kuwa wafungwa ambao ni wagonjwa, pia wana haki ya kupata tiba, hivyo kutaka wapelekwe kwake ili wapate kikombe cha tiba.

Babu akemea rushwa
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila amekemea vitendo vya rushwa na urasimu ambavyo vinadaiwa kufanywa na watu wanaoruhusu magari yanayokwenda Samunge, hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wagonjwa."Wanakuja hapa wanalalamikia kunyanyaswa katika vituo vya kupitisha magari, naomba jambo hili liachwe na wahusika,"alisema Mwasapila.

Alisema utaratibu uliowekwa na Serikali wa kuruhusu kwa mpangilio maalumu wa magari yanayokuja Samunge ni mzuri na unapaswa kutekelezwa na pande zote bila ya malalamiko.

Asisitiza kikombe ni kimoja
Kadhalika, Mchungaji Mwasapila aliendelea kusisitiza kuwa kikombe cha dawa anachopaswa kupewa mgonjwa ni kimoja tu, licha ya kuwapo kwa madai ya baadhi ya watu waliopewa dawa hiyo kutopona.
Maelezo ya Mchungaji huyo yamekuja wakati baadhi ya watu waliokunywa dawa kusema bado hawajapona vizuri, hivyo kuhitaji kikombe cha pili.

Kadhalika, tafiti za kitaalamu zilizofanywa zimekuwa zikipendekeza kuchunguzwa kwa kiwango cha dozi kinachotolewa na mchungaji huyo ili kubaini kama kinakidhi kutibu magonjwa husika kufuatia tafiti hizo kubaini uwezo mkubwa wa kitiba katika mti wa Murigariga unaotumiwa na Mchungaji Mwasapila.

Mtaalamu mmoja wa afya mkoani Arusha, aliyeomba kutotajwa jina alisema, dawa ya Mchungaji Mwasapila ina uwezo mkubwa ila kama akishauriwa kitaalamu ikaboreshwa itakuwa na manufaa makubwa.Hata hivyo, Mwasapila jana alipinga mawazo hayo na kusisitiza kuwa wagonjwa ambao wamepata kikombe na wakapata nafuu na baadaye hali zao kurejea kuumwa wanapaswa kuwasiliana naye kwa maombi na sio kunywa kikombe kingine.

Maofisa wa Kenya Samunge
Maofisa wa Serikali ya Kenya, wakiwamo wanaotoka katika ofisi ya Rais Mwai Kibaki pamoja na familia zao, jana walitinga Samunge ambapo walipata kikombe cha tiba.Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa maofisa hao, ambaye ni Chifu wa eneo la Frans Mara, Olenantea Labora alisema yeye na maofisa wenzake kutoka Kenya wamefika Samunge kupata tiba."Tumekuja kupata kikombe cha dawa na familia yangu na wenzangu, tumepata taarifa za dawa hii kutibu wengi nasi tumekuja," alisema Labora ambaye alikuwa na sare za Serikali ya Kenya.

Foleni yaongezeka Samunge
Foleni ya magari ambayo yanaingia kijiji cha Samunge, imeongezeka tena, ambapo jana ilikuwa imekwenda zaidi ya kilometa tatu kutoka nyumbani kwa Mchungaji Mwasapila.Magari mengi yaliyopo kwenye foleni hiyo, ni kutoka nchi jirani ya Kenya, mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini.

Wakati magari yakiongezeka, mvua ambazo zimeanza kunyesha zimetishia tena kuzuia watu kufika Samunge baada ya juzi usiku kunyesha mvua ambayo imesababisha magari kadhaa kukwama barabarani.Baadhi ya madereva wakizungumza na Mwananchi, waliitaka halmashauri ya Ngorongoro, kukarabati barabara ya kutokea njia panda ya Arusha na Loliondo kwenda kijiji cha Samunge ambayo magari yote yanaitumia kufika Samunge.

Jonathan Mathayo, alisema barabara hiyo ambayo ipo chini ya halmashauri ni mbaya sana na sasa imeanza kusababisha magari kukwama. "Mbona hawa halmashauri wanapokea fedha hakuna lolote, barabara  zao mbaya, hakuna huduma za afya, Samunge pachafu ....tunaomba katika fedha za ushuru tunaolipa watengeneze barabara," alisema Mathayo.

Mchungaji Mwasapila, pia jana alizungumzia tatizo hilo, la barabara na kuiomba Serikali kuifanyia ukarabati ili kuwezesha watu kufika Samunge bila tatizo. "Nimeonyeshwa maelfu ya watu wa mataifa mbalimbali kwenda Samunge sasa naomba Serikali irekebishe hii miundombinu ili wafike na kupata tiba," alisema Mwasapila.

0 comments

Post a Comment