Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Sheikh Yahya afariki Dunia

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MNAJIMU Mashuhuri Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein (81), amefariki dunia.Sheikh Yahya alifariki dunia jana majira ya saa nne asubuhi muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mtakatifu Ukombozi, Kinondoni Dar es Salaam baada ya kuugua ghafla.


Mdogo wa marehemu, Nuru Hussein alisema kaka yake ambaye alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda wa miaka mitatu sasa, aliamka jana akiwa na afya njema na kuanza kuwatibu wagonjwa wake.“Alikuwa anaendelea vizuri tangu alivyoamka asubuhi. Aliwatibu hata wagonjwa wake waliokuwa na ratiba yakumwona leo (jana)," alisema na kuongeza:"Baada ya kumaliza kuwatibu, aliagiza juisi na hapo ndipo afya yake ilipobadilika.


Tulipompeleka hospitali akafariki.”Mtoto wa marehemu, Hussein Yahya alisema afya ya baba yake haikuwa mbaya alipokwenda kumjulia hali nyumbani kwake jana asubuhi lakini, ilibadilika ghafla baadaye.“Ni kweli Sheikh Yahya amefariki, ni kama majira ya saa nne na dakika kadhaa hivi asubuhi.


Tangu saa 12 alfajiri nilipofika kumsalimia alikuwa na afya njema tu, lakini ghafla hali ilibadilika na alipopelekwa hospitalini, alikata roho,” alisema Yahya na kuongeza:“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Ukombozi na utaratibu wa kuupeleka Hospitali ya (Jeshi) Lugalo unafanyika.


”Yahya alisema baba yake alikuwa anasambuliwa na maradhi ya moyo na aliwahi kupelekwa India kwa matibabu na kupata nafuu kwa kiwango kikubwa.Alisema baba yake ameacha watoto zaidi ya 20 na wajukuu wapatao 30.


“Nimekuwa mtu wa karibu sana kwa baba yangu. Nakumbuka siku tatu kabla ya kufikwa na mauti, kauli yake ya mwisho na ya msingi aliniuliza kuwa duniani kuna habari gani, nilipomweleza kuwa kiongozi wa upinzani wa Yemen Hassan Baoum ameachiwa, aliitikia sawa,”alisema.


Akizungumzia kazi ya utabiri wa nyota aliyokuwa akifanya baba yake, Yahya alisema, marehamu alikuwa anatabiri matukio mengi ambayo yalikuwa yanatokea akisema utabiri wake wa mwisho ni ule wa vifo vya wasanii wa Five Star uliotokana na ajali ya gari.


“Mzee alikuwa mtu wa kutabiri na kuacha matokeo yatokee. Tayari imethibitishwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye elimu kubwa sana ya unajimu,” alisema.Yahya alisema ataendelea kufanya shughuli zote za utabiriakisema baba yake amemfundisha kazi hiyo.


“Utabiri utaendelea kama kawaida, amenifundisha kazi na nimekuwa nikifanya baadhi ya kazi zake wakati alipokuwa mgonjwa na hata leo (jana) nilipopata taarifa za kifo chake, nilikuwa Redio Uhuru kwenye kipindi cha nyota,” alisema.


Mwenyekiti wa kamati ya msiba huo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema marehemu atazikwa leo katika makaburi ya Tambaza, Dar es Salaam.Ibada ya mazishi ya Sheikh Yahya itafanyika leo saa 7:00 mchana katika Msikiti wa Tambaza, Upanga.


“Msiba huu ni mkubwa kwetu. Marehemu alikuwa kiongozi wetu mkubwa na tulimtegemea kwa mambo mengi. Atazikwa kesho (leo) alasiri, swala itafanyika katika Msikiti wa Tambaza na atazikwa katika makaburi ya Tambaza,” alisema.“Tulimpenda sana lakini Mungu amempenda zaidi. Tunaamini kila nafsi lazima ionje umauti hivyo Sheikh Yahya ndiyo siku yake ya mwisho.”


Utabiri wa Shekhe YahyaMoja ya utabiri aliowahi kutoa Sheikh Yahya Hussein enzi za uhai wake ni ule wa mwaka 2005, aliposema kuwa ipo siku CCM na CUF wataunda serikali moja.Mwaka huo 2005 Sheikh Yahya pia alitabiri kuwa Rais Benjamin Mkapa ataongezewa muda wa kutawala zaidi ya ule wa kikatiba.


Utabiri huo ulikuja kuwa wa kweli baada ya uchaguzi mkuu kusogezwa mbele kutokana kifo na mgombea mwenza wa Chadema. Katika kipindi hicho Mkapa aliendelea kuwa madarakani kwa miezi mitatu zaidi kabla ya uchaguzi mwingine kuitishwa.


Yahya aliwaambia waandishi wa habari kuwa aliona kinyota kuwa kuna mgombea atapoteza maisha lakini, kistaarabu hukusema hivyo.


Hata uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2000 alitabiri kuwa utarudiwa na ukawa kweli.
Julai 26 mwaka 2009, Sheikh Yahya pia alitoa utabiri mwingine uliotekenya fikra za watu pale alipoeleza kuwa kuna Rais wa nchi moja ya mashariki mwa Afrika atatekwa akiwa kwenye ndege au kupinduliwa.


Alisema tukio hilo, litatokana na hali ya kupatwa kwa jua kulikotokea Julai 24, 2009 huko China na kwingineko barani Asia.Katika utabiri huo Sheikh Yahya alieleza kuwa pia kutatokea matatizo katika mambo ya ulinzi na usalama kwa viongozi wa nchi mbalimbali za Mashariki ya Afrika.




"Pia natabiri baadhi ya wabunge kadhaa kufungwa na wengine kufa ghafla," akasema. Akaongeza kuwa baadhi ya maofisa wa ngazi za juu serikalini watafukuzwa kazi wakiwa nje ya nchi zao kwa kashfa mbalimbali.Hata hivyo baadhi ya utabiri wa Sheikh Yahya haukuwahi kutokea. Moja ya utabiri wake ambao haukutokea ni ule wa Oktoba 29, 2010 alipoeleza kuwa Uchaguzi Mkuu usingefanyika.


Mwenyewe aliwahi kutetea hoja hiyo kuwa ingawa uchaguzi haukuahirishwa kitendo cha watu kujitokeza kutaka usitishwe ni sehemu ya matokeo ya nyota yake na alisisitiza kuwa jambo hilo linaashiria kwamba elimu ya nyota huwa haisemi uongo.


Lakini Sheikh Yahya alitahadharisha kuwa kwa kawaida akishatabiri kitu kinachofuata ni kusubiri na siyo kazi yake kuhakikisha kwamba kile alichotabiri kinatokea.


“Kwa kawaida mtabiri anapotabiri siyo kazi yake tena kuhakikisha kile alichokitabiri kinatokea, kwa hiyo watu wasubiri tu waone kwa sababu siku bado zipo kabla ya uchaguzi,” alisema Shekhe Yahya.


Alikuwa akisisitiza kuwa utabiri wake hautumii uchawi kama wengi wanavyofikiri, isipokuwa anatumia hesabu za kinyota na wala siyo utashi wake au wa watu anaowatabiria.


Wasifu wa SheikhYahya Hussein
Sheikh Yahya Hussein, alizaliwa mwaka 1932 wilayani Bagamoyo katika familia ya Kabila la Kimanyema lenye asili ya Mkoa wa Kigoma.


Alipata elimu yake ya awali katika Shule ya Al-Hassanain Muslim ya Dar-es-Salaam. Baadaye alijiunga na Chuo cha Muslim Academy cha Zanzibar kilichokuwa kinamilikiwa na Sheikh Abdallah Swaleh Al-Farsy ambaye alikuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar wakati huo.
Alipohitimu mafunzo yake, alikwenda Misri kuendelea na masomo ya dini katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar kilichopo Cairo.Alirejea nchini mwanzoni mwa miaka ya 1960 na kuanza kazi ya kutabiri kwa kutumia nyota

0 comments

Post a Comment