Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wafiwa Tarime wafichwa, wawekewa ulinzi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WANANCHI wa Nyamongo wilayani Tarime, wamewaficha na kuwapa ulinzi mkali, ndugu wa marehemu waliouawa na polisi katika jaribio la kuvamia Mgodi wa Barrick, ili kuepuka kile kinachodaiwa kuwa ni uwezekano wa serikali kuwarubuni ili wakubali kuzika.


Mei 16 mwaka huu polisi wilayani Tarime, waliwaua kwa kuwapiga risasi, watu watano kati ya zaidi ya watu 1,000 waliovamia mgodi huo kwa lengo la kupora mchanga wa dhahabu.




Hivyo tukio hilo lililotokea katika Kijiji cha Matongo, wilayani humo limesababisha msuguano mkali kati ya polisi na wananchi wa eneo hilo ambao juzi, waligoma kuzika miili ya marehemu hao na kukataa rambirambi ya polisi.


Habari zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema uamuzi wa kufichwa ndugu wa marehemu, unalenga katika kuhakikisha kuwa hawarubuniwi na vyombo vya serikali, inayotaka miili hiyo izikwe.


Jeshi la Polisi limeonyesha nia ya kutaka kuzika miili hiyo kwa gharama zake na kutoa rambirambi kwa wafiwa, hatua ambayo wananchi wameipinga.




"Tumelazimika kuwaweka ndugu wa marehemu katika kambi maalumu na kuwapa ulinzi mkali. Tunawagharimia kila kitu ili kuvunja nguvu za ushawishi zinafanywa na vyombo vya dola kwa kuwatumia wafanya biashara maarufu wa hapa,"alisema mmoja wa wananchi hao.


"Tumefia hatua hiyo baada ya kuona serikali inataka kulifanya tukio hilo dili. Tumeanza kuona ikiwaita ndugu hao kwenye vikao vya siri juzi usiku na kuwashawishi wakubali kuzika na kupewa rambirambi ya Sh3 milioni kwa kila mfiwa," alisisitiza mwananchi huyo.


"Suala kubwa ni kwamba fedha hizo zimetoka wapi, sSerikalini ama mgodini," alihoji.Alisema kitendo hicho kinaashiria kuwa watu wengi wanaouawa na polisi na kuwahi kutangazwa kuwa walikuwa kwenye mapambano, wanauawa kimakosa.


Kauli ya mwanakijiji huyo iliungwa mkono na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, ambaye alisisitiza kuwa ndugu wa wafiwa wamefichwa.


Lema pia ni Waziri kivuli wa Mambo ya ndani aliliambia gazeti hili jana kuwa watu hao wamefichwa ili kudhibiti rushwa inayolenga katika kuwashawisihi wakubali mazishi."Haiingii akilini kuona serikali hii inaua kisha inahaha kutoa rushwa kwa wafiwa, wanaficha nini kama walitekeleza wajibu wao wa kuua
waharifu, majambazi wavamizi, hizi fedha nani katoa, je kwa kufanya hivyo inamwekea mazingira gani mwekezaji maana hilo si suluhu la
matatizo,"alisema.


Kamishina Chagonja aendelea kubanwa


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Operesheni katika Jeshi la Polisi, Paulo Chagonja jana alibanwa na ndugu wa majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Bugando wakitaka msaada.




"Mkuu sisi ndugu zetu wako Bugando wana hali mbaya sana, gharama ni kubwa hakuna msaada wowote uliotolewa, tuligharamia wenyewe kuwapeleka mbona hamuwazungumzii wanapataje hizo fedha lakini mnasema
mna ubani wa waliokufa, mpaka wafe ndipo uje utoe,"alihoji mmoja wao.


Hata hivyo Chagonja hakujibu hoja hiyo na badala yake alisema "hapa kuna majeruhi wangapi,ooh wako Bugando wako wangapi,ok sawa."


Mbunge watia neno
Mbunge wa Viti Maalumu Chadema na ambaye PIA ni Waziri kivuli wa Mambo ya Uwekezaji, Esther Matiko, alisema, mpango wa serikali wa kuunda tume hauna manufaa kwa jamii na kuwataka watoe ripoti ya watu sita wanaodaiwa kuuawa mwaka jana katika Hifadhi ya Serengeti.

0 comments

Post a Comment