DIWANI wa Kata ya Kijitonyama, Ulole Juma Athuman, amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuifungua barabara inayounganisha eneo la Sinza na Kijitonyama akitishia kwamba, asipofanya hivyo ataitisha mkutano wa hadhara wa wananchi utakaoamua kuwapo au kutokuwapo kwa njia hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, diwani huyo alisema katika suala hilo hakuna mjadala na kwamba kama unahitajika utafanyika baada ya barabara hiyo kufunguliwa na wananchi kuitumia kama ilivyokuwa awali.
Ulole alisema kuwa kitendo cha Spika Makinda kufunga barabara hiyo, ni ukiukwaji wa sheria na mamlaka zilizopo kwani hatua hiyo ilipaswa kufuata taratibu za vikao husika, kabla ya uamuzi kufikiwa na kwamba kitendo hicho hakikupaswa kufanywa na mtu wa ngazi ya Makinda.
“Sisi viongozi tunategemewa na wananchi kuwa mfano na pia ndiyo kioo cha jamii tunayoiongoza, sasa katika hali kama hii iliyojitokeza wananchi watakuwa wanajifunza nini?” alihoji diwani huyo na kudai:
"Alichofanya Spika Makinda kina nia ya kuongeza ukubwa wa eneo la kiwanja chake na si vinginevyo."
Alisema kwamba Spika Makinda alitakiwa kuwasilisha suala hilo katika ngazi ya mtaa na ama lingepitishwa katika hatua hiyo, lingepelekwa katika ngazi ya kata na kamati ya maendeleo ya kata pia ingelipitia na kutoa uamuzi kulingana na mapendekezo ya wananchi.
Katika sakata hilo, jana Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana aliwaita ofisini kwake, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kijitonyama na Ofisa Mtendaji wa Mtaa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpakani ‘B’, Balbo Kalinga kujadili suala hilo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa watendaji walioitwa na Rugumbana siyo wa mtaa ilipo barabara inayolalamikiwa kufungwa.Rugimbana alipoulizwa kuhusu suala hilo alikana kuwa na kikao na watendaji hao lakini akasema alichofanya ni kuwaita ili kusikia kutoka kwao kuhusiana na sakata hilo la kufungwa kwa barabara na kwamba hakikuwa kikao rasmi.
“Sikuitisha kikao, nimewaita kama Mkuu wa Wilaya ili kujua kitu kinachoendelea katika eneo hilo na niliowaita ndiyo ambao nimewahitaji,” alisema Rugimbana
Diwani Ulole alisema Mkuu wa Wilaya amelichukulia suala hilo kisiasa akisema licha ya kutokuwa wa eneo lenye mgogoro, aliowaita ni wanaCCM na kumwacha yeye ambaye anatoka Chadema.
Hata hivyo, Rugimbana alisema tangu kuanza kwa sakata hilo amezungumza na watu tofauti lengo likiwa kupata ukweli kuhusiana na malalamiko yalijitokeza, akisema leo atakutana na watendaji wake wa manispaa wakiwamo wa mipango miji ili kutatua tatizo hilo.
“Nitafute kesho nitakupa taarifa rasmi baada ya kukutana na watendaji wangu” alisema Rugimbana na kuongeza kuwa yeye ndiye anayejua anaongea na nani na wakati gani.Sakata la kufungwa kwa barabara hiyo liliibuka mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo kulalamika.
0 comments