Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Magufuli acharuka tena

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amezichachamalia halmashauri za wilaya akizituhumu kutumia vibaya fedha za Mfuko wa Barabara na kuibia wananchi kupitia fedha za mabango yaliyo kwenye hifadhi za barabara wakati jukumu hilo ni la Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Akifungua mkutano wa wadau wa kujadili taarifa ya utafiti ya ufuatiliaji mapato yatokanayo na tozo la mafuta mjini Dar es Salaam, Dk. Magufuli aliendelea kuzinyooshea kidole halmashauri hizo kwa kuajiri makandarasi wenye uwezo mdogo, hali inayoonesha kwamba wanafanya hivyo ili kuendeleza ‘uchakachuaji’ wa mali za umma.

“Nasema hili kwa uwazi, siogopi, je, ni kweli fedha hizi zinatumika kwa makusudi ya barabara? Zinatumika kulipa posho na hata hayo matengenezo ya barabara yanayodaiwa kufanywa, hayakidhi viwango,” alisema Magufuli.

Alisema ni vyema ikawapo orodha kwa kila halmashauri na Tanroads, zinazoonesha jinsi fedha hizo za Mfuko wa Barabara zinavyotumika, ili kudhibiti matumizi yasiyo halali.

“Mifano mingi ya matumizi mabaya ya fedha ipo, lakini baya zaidi ni hizi halmashauri kuajiri makandarasi wenye uwezo mdogo, kwani uchunguzi wa Bodi ya Makandarasi nchini umebaini asilimia 46 ya Halmashauri hazina makandarasi wenye sifa,” alibainisha Magufuli.

Akizungumzia sheria ya mabango, alisema ni kosa kwa halmashauri nchini kuchukua fedha za matangazo ya mabango yaliyowekwa kwenye hifadhi ya barabara, kwani wenye jukumu la
kuzikusanya ni Tanroads.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2007, kifungu cha 29 kinasema , kibali cha kuweka kitu chochote yakiwemo mabango ya biashara ndani ya hifadhi ya barabara kinapaswa kutolewa na Tanroads ambao ndiyo wasimamizi wa barabara husika.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu, Jiji la Dar es Salaam pekee lina jumla ya mabango 744 ndani ya hifadhi za barabara zinazosimamiwa na Tanroads na kwa kipindi cha miaka miwili ya mwaka 2008 hadi 2010, wakala huyo hakupata fedha za matangazo.

Alisema hiyo inatokana na halmashauri jijini kuingilia na kukusanya fedha hizo kinyume na sheria.

Aliwataka watendaji wa halmashauri hizo wakiwamo mameya na wenyeviti, kuwa na uelewa wa sheria, na kuacha kung’ang’ania fedha zisizowahusu.

Alisisitiza: “Watu wa manispaa wanaiba fedha za wananchi kwa kuwatoza mabango, sijui wanafuata sheria gani, tuwaeleweshe hawa, mameya wa Dar es Salaam hata wakitaka waniite nitawasaidia bure kuwaelimisha kuhusu sheria, wanahitaji elimu tu,” alibainisha Waziri Magufuli.

Alisema ikiwa fedha hizo za mabango zingetumika ipasavyo Tanroads, zingesaidia matengenezo ya barabara nyingi nchini, kwani hivi sasa Wizara ya Ujenzi inatengeneza hata barabara ambazo zilitakiwa zitengenezwe na manispaa.

Wakati huo huo, Waziri Magufuli amesema uzembe wa mamlaka zinazohusika kutoa vibali vya ujenzi wa vituo vya mafuta nchini, umechangia ongezeko la vituo vilivyojengwa holela kwenye barabara ya Morogoro.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya barabara umbali wa kituo kimoja hadi kingine cha mafuta unatakiwa kuwa kilometa 10, lakini hali ya sasa ni kilometa 1.5.

“Sasa tujiulize, hao waliotoa vibali ya ujenzi wa vituo hivyo wametumia sheria ipi? Inawezekana hata uvunjaji wa sheria kama hizi umekuwa chanzo cha msongamano jijini,”
alisema Magufuli.

Alizinyooshea kidole halmashauri kwamba hata maeneo ya hifadhi ya barabara yanafanyiwa biashara kama vile za mbao na vibanda ambazo huenda manispaa zinachukua kodi kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Magufuli alisisitiza wadau kujadili na kuweka mikakati ili kuhakikisha fedha za Mfuko wa Barabara zitokanazo na tozo kwenye mafuta ya petroli na dizeli, zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya matengenezo ya barabara nchini.

Katika hatua nyingine, Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imemkabidhi Waziri Magufuli, ripoti ya taarifa ya ukaguzi wa barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, ikionesha kuwa imejengwa chini ya kiwango na ina upungufu mwingi unaohitaji marekebisho.

Taarifa hiyo inasema barabara hiyo ina kasoro nyingine ambazo ni hatari kiusalama.

Akikabidhi ripoti hiyo katika hafla ya uzinduzi wa Leseni za Uhandisi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Profesa Ninatubu Lema, alisema upungufu huo ambao haukubainishwa unapaswa kufanyiwa kazi mapema.

Aidha, aliishauri Serikali itazame upya utaratibu wa utekelezaji wa miradi ambayo inafadhiliwa na serikali za nje kwa jicho la kina, ili zinapoonekana kasoro ziweze kurekebishwa haraka.

“Serikali itazame upya kwa jicho lake utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na serikali za nje, tena jicho lake linatakiwa liwepo hapo muda wote na watu wanaotakiwa kuisimamia wawe waadilifu … maendeleo ya kweli na endelevu yataletwa na wahandisi Watanzania na si wa nje, maana wa nje ni wafanyabiashara,” alisema.

Mapema Msajili wa Bodi hiyo, Mhandisi Steven Mlote, alisema hadi mwezi huu, jumla ya wahandisi 10,281 wamesajiliwa katika ngazi mbalimbali na kati yao 9,518 ni wazalendo na 763 ni wageni.

Alisema jumla ya wahandisi washauri ni 324 kati yao 254 ni wazalendo na 70 ni wageni ambapo pia imesajili kampuni za ushauri wa kihandisi 191 kati yao 138 zikiwa ni za kizalendo na 53 za kigeni.

Alisema Bodi imeanzisha utaratibu wa kutoa leseni kwa wahandisi kwa malengo mbalimbali ikiwamo kuthibitisha kuwa mhandisi ana sifa za kutumikia jamii kama mhandisi mtaalamu ama mshauri katika fani yake, ili kudhibiti ajira za wahandisi wa kigeni na kusimamia ufanyaji kazi wa kampuni za ushauri za kigeni.

Alisema bodi hiyo imeweka vigezo ambavyo mwombaji wa leseni atahitaji kuzikidhi ili apewe leseni, ikiwamo kuwa na elimu ya chuo kikuu kinachotambulika na Serikali na kuwa na usajili wa Bodi kama Mhandisi Mtaalamu au Mshauri.

“Napenda kuthibitisha kuwa wahandisi washauri wa kizalendo na kampuni za ushauri wa kihandisi za kizalendo zina uwezo mkubwa wa kubuni na kusimamia miradi ya ukubwa na aina yoyote ile nchini.

Ni vyema Taifa likatumia utaalamu huu wa wahandisi wazalendo ipasavyo ili kujiletea maendeleo,” alisema.

Dk. Magufuli aliiagiza bodi hiyo kuhakikisha inakagua miradi yote nchini kwa kuanzia na barabara na kuangalia wataalamu wake kama wana sifa za kuisimamia ili siku moja barabara za Watanzania ziwe na hadhi.

“Nawapa kazi mkague miradi yote nchini mkianzia na barabara, baadaye mtaendelea na mabwawa na mingine, najua kwa kazi hii mtachukiwa sana na wapenda fedha ila msikate tamaa, tekelezeni wajibu wenu, tunataka mzunguke nchi nzima na kama ni fedha tutawaongeza,” alisema.

Aidha aliitaka Tanroads kuhakikisha kila mkataba wa ujenzi wa barabara wanaoingia awepo mhandisi mzalendo na kijana kwa ajili ya kupata uzoefu.

Pia alisema wataangalia uwezekano wa kuwapa wahandisi wa ndani miradi ya barabara kuisimamia kwa asilimia 100 kwa kuanzia na kilometa 100 na baadaye watakuwa wakiongeza kulingana na ufanisi watakaoonesha.

0 comments

Post a Comment