IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
• Mapambano dhidi ya ufisadi
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kamwe hamwogopi mtu katika suala zima la kupigania maendeleo ya nchi, bali anamtegemea zaidi Mungu amlinde katika mapambano dhidi ya ufisadi.
Sitta aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa albamu ya ‘Baba Mwenye Uweza’ iliyofanyika jana katika Parokia ya Kanisa Katoliki Chang’ombe Dar es Salaam.
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, alisema katika suala zima la utekelezaji wa majukumu ya kikazi amekuwa akikumbana na misukosuko mingi hasa wakati wa kuendesha vikao vya Bunge.
“Nimekuwa nikikutana na misukosuko mingi mno katika masuala ya kazi ninazozifanya hasa pale Bunge… lakini nimekuwa na kazi moja tu ya kumtanguliza Mungu mbele; ndiyo sababu nimefanikiwa hadi sasa kwa maana hiyo sitishiki na mtu,” alisema Sitta.
Alisema kutokana na hali hiyo, watu wengi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi juu ya kujiamini kwake bila kupata majibu huku akisisitiza kuwa Mungu ndiye muweza na wengine ni sawa na visisimizi.
“Watu wamekuwa wakiniuliza, eti ‘mbona unajiamini, unajiamini kitu gani?’… huwa nawajibu mara nyingi kuwa mimi ni msikilizaji mzuri wa nyimbo za Injili, lakini pia niko karibu na Nyumba ya Mungu kama hii, hivyo sitishiki!” alisema Sitta.
Alisema kitendo cha viongozi kualikwa katika sehemu za Nyumba ya Mungu na kugoma kuhudhuria ndiyo sababu kubwa ya kuwafanya kuwa na kiburi hadi kufikia hatua ya kuongoza kwa kiburi.
Aliwataka viongozi wa dini kutoogopa kuwaalika katika nyumba za Mungu kwa kuwa yeye anaamini kufanya hivyo kutasaidia viongozi kuongaza taifa kwa amani na utulivu.
“Sisi Wakristo siku zote kusogelea Nyumba ya Mungu kunapunguza kiburi na pia kunasaidia kuongoza kwa moyo… nawaambieni juu ya Mungu sisi ni sawa na sisimizi tu,” alisema Sitta.
Sitta alisema kutokana na mwenendo wa kisiasa amekuwa mstari wa mbele kupinga mambo yanayoendeshwa hovyo hovyo ikiwa ni pamoja na ufisadi.
Aidha, alitoa wito kwa vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi bila kuogopa; zikiwemo za bungeni kwa vile yeye ameingia bungeni akiwa na umri wa miaka 32.
Naye Paroko wa Kanisa hilo, Joseph Mosha, alimpongeza Sitta na kumtaka asikate tamaa dhidi ya changamoto mbalimbali zinazomkabili.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo Temeke, Abass Mtemvu, alitumia muda mwingi kuelezea mambo mbalimbali ambayo ameyafanya tangu alipochaguliwa mwaka 2005.
Katika hafla hiyo Spika Sitta alichangia sh milioni moja wakati Mtemvu alichangia sh 600,000.
You Are Here: Home - - Sitta: Simwogopi mtu. Namtegemea Mungu
0 comments