CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willbrod Slaa kuacha kueneza uzushi huku kikimtaka kuutoa hadharani waraka aliodai wa siri ambao umeandaliwa na chama hicho.
Akizungumza na Tanzania Daima, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema Dk. Slaa anashindwa kutofautisha kati ya waraka wa siri na ule ambao ni mahususi kwa matumizi ya umma.
Alisema Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM iliyokutana hivi karibuni ilitoa maamuzi 26 ambayo hadi sasa yanaendelea kutekelezwa hivyo ni vyema huo waraka unaodaiwa kuwa ni wa siri ukawekwa hadharani ili uweze kufahamika.
Nnauye alisema waraka huo ni batili, hautokani na maamuzi ya chama hicho kwa kuwa hadi sasa wameweza kuzunguka katika mikoa 10 kuuelezea umma yale yaliyoazimiwa na NEC.
Alisema Dk. Slaa amekuwa bingwa wa kueneza uongo hasa baada ya kuona ajenda yake ya ufisadi imeishiwa nguvu kwa kuwa CCM pamoja na serikali imezifanyia kazi.
“Inasikitisha kuona Katibu huyo anashindwa kutofautisha maamuzi yetu ya NEC na waraka anaodai wa siri…inawezekana siri iliyopo ni kwake na familia yake,” alisema Nnauye.
Alisema Dk. Slaa amekuwa kiongozi wa kuchakachua habari hivyo kutokana na kuonekana kuishiwa sera ni bora akaomba arudi akaendelee kutumikia kanisani kwake.
“Tunatarajia kuzunguka katika mikoa yote na hapa tulipo tunaelezea wananchi wa Singida kuhusu maamuzi yetu ya NEC na kuyasema yote jukwaani…sasa hiyo siri inatoka wapi?” alihoji Nnauye.
Juzi Dk. Slaa alifichua siri za waraka huo wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Sekondari Msakila mjini Sumbawanga ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya chama hicho mkoani Rukwa, baada ya kuutikisa Mkoa wa Mbeya kwa maandamano na mikutano ya hadhara kwa siku tatu mfululizo.
Dk. Slaa alieleza kuunasa waraka huo wa siri wa CCM ambao ndani yake chama hicho kimekiri waziwazi kupoteza ladha kwa umma, huku mkakati pekee wa kujinusuru ukielezwa kuwa ni kubadili sura za viongozi wa chama hicho ili kuwajengea matumaini mapya Watanzania.

0 comments