Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Magufuli awageuka wakuu wake wa kazi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KAULI ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuwa kwa vyovyote iwavyo lazima abomoe mabango yote ya biashara barabarani akisema kuwa hakuna wa kumzuia kuyaondoa kwa kuwa anatekeleza sheria za nchi, imetuma ujumbe mzito kwa wakubwa wake wa kazi.
Miongoni mwa viongozi walioguswa na kauli hiyo ya Magufuli ni Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambao kwa wakati tofauti walimkemea waziri huyo, wakimzuia kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kwa masilahi ya kisiasa.
Alipomtembelea wizarani kwake wiki chache zilizopita, Rais Kikwete alimwambia Magufuli, “acha ubabe.”
Kabla ya hapo, Pinda alimfokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Chato, linalowakilishwa na Magufuli, akimtaka asitishe bomoabomoa mara moja.

Hata juzi wakati akifungua semina elekezi mjini Dodoma, Rais Kikwete alikemea tabia ya ubabe wa mawaziri na kauli za kupingana wenyewe kwa wenyewe kupitia kwenye vyombo vya habari.
Lakini katika wiki hii pekee, Magufuli ametoa kauli zinazoonyesha hayuko tayari kusitisha ubabe wake wala bomoabomoa, kazi ambayo amekuwa akiifanya kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Hivi karibuni kituo cha televisheni cha TBC1 kilimnukuu Magufuli akisema: “Ni bora ukafukuzwa wakati unatekeleza sheria na ni bora ukafa wakati unatekeleza sheria, kwa sababu ukienda mbinguni utapewa barabara ya kutengeneza.”
Mbali na rais na waziri mkuu, msimamo wa Magufuli pia umewakera viongozi katika maeneo mengine, wakiwamo mameya wote wa manispaa tatu za Dar es Salaam.

Wanapinga kauli ya Magufuli kwa maelezo kuwa bajeti za halmashauri zao zimekuwa zikitegemea kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na mabango, ambayo Magufuli amesema atayabomoa kwa sababu yako kwenye hifadhi ya barabara.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alisema kuondolewa kwa mabango ya matangazo kutawaathiri kwa kiasi kikubwa wananchi kwani fedha inayopatikana katika mabango hayo hutumiwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Alisema mabango hayo huiwezesha manispaa yake kukusanya sh bilioni mbili kwa mwaka, ambazo hutumika kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
“Lakini ifahamike kuwa watakaoathirika ni wananchi kwa kukosa huduma za muhimu ikiwamo ujenzi wa visima vya maji na ukarabati wa miundombinu,” alisema.
Alifafanua kuwa sheria ya mwaka 2007 imeipa manispaa mamlaka ya kutoa kibali cha maeneo ili kuhakikisha wanaweza kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato.
“Manispaa zimekuwa zikijiendesha zenyewe kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya mapato, ikiwamo kodi za mabango, naona wajibu wetu ni kuboresha ulinzi katika mabango yaliyolipiwa ili kuzidi kujiongezea ukusanyaji wa mapato na kufikia malengo tuliyokusudia,” alisema.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, alisema suala hilo lilishafikishwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Bado ana matumaini kwamba atakutanishwa na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, kwa ajili ya kuzungumzia, kueleweshana na kuondoa matatizo yanayoendelea kujitokeza.
Mwenda naye alisema mabango ndicho chanzo kikuu cha mapato na kwamba kuyaondoa kunaweza kuathiri utendaji wa manispaa hiyo.
Alisema katika bajeti ya mwaka huu wanatarajia kukusanya kiasi cha sh bilioni tatu kwa ajili ya mapato ya ndani. Sh bilioni moja zinatokana na kodi za wananchi, huku sh bilioni mbili zikitokana na ushuru wa mabango.
Alisema iwapo itathibitika kwamba mabango yanasababisha ajali, watalazimika kueleweshwa ili wayapange katika mpangilio ulio mzuri na kuepusha ajali hizo, lakini si kuyabomoa.
“Tunaamini tutakaa na Magufuli ili atueleweshe tatizo ni nini? Na kama ni kusababisha ajali, basi tutalazimika kuyaweka kiufundi, nafikiri tutaelewana naye,” alieleza Mwenda.
Alisema kutokana na manispaa kutakiwa kuwa na vyanzo vya mapato kwa ajili ya kujiendesha, ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu gharama ya kuweka mabango imeongezeka.
Meya wa Manispaa ya Temeke, Maabadi Hoja, alisema manispaa ndiyo inayofahamu kiasi cha mapato kinachotokana na mabango. Alimshangaa Magufuli kwa kauli hiyo, ingawa alikiri kwamba hajaisoma wala kuisikia moja kwa moja.
“Siwezi kuongea zaidi labda acha tuone hicho kimya cha mshindo alichokisema,” alieleza.
Hata hivyo akizungumza katika kipindi hicho, Dk. Magufuli alipinga utetezi kwamba mabango hayo yanaongeza kipato kwa kukusanya kodi, kwani hakuna ushahidi wa kauli hiyo, kwa madai kuwa fedha zinazokusanywa zimekuwa zikiishia mikononi mwa watu binafsi na serikali kutonufaika kwa chochote.
“Mkakati wangu uko palepale hauwezi kubadilika, ni lazima mabango yataondolewa ili kuweka barabara salama na safi. Haiwezekani barabara zijengwe kwa mabilioni halafu mtu anakuja kuharibu na kuweka mabango,” alisema Magufuli.

0 comments

Post a Comment