Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - UDOM watawanywa kwa mabomu bungeni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
ASKARI wa Kikosi cha Kuzia Fujo (FFU) jana, walilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi kuwatawanya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na
wanaharakati wengine baada ya kufunga barabara kuu ya kutoka Morogoro ili kulishinikiza waruhusiwe kuingia kwenye eneo la kushiriki mjadala Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Wakizungumza katika lango kuu la  Ofisi za Bunge majini Dodoma  jana kwa nyakati tofauti wanafunzi hao walisema kuwa ni jambo la kushangaza kwa ofisi hiyo kuwaalika wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya City na kukiacha chuo hicho bila ya kuwa na uwakilishi.

"Muswada huo umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza wamealika wanafunzi wa Shule ya Sekondari City ambao hawajui Kiingereza shule yenye matokeo mabovu kila mwaka, huku ni kuwachezea wananchi, alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Mmoja ya wanafunzi hao ambaye alijitambulisha kwa jina la moja la Denis, alisema iwapo wabunge watapitisha muswada huo wako radhi kuingia mtaani kupinga tume hiyo kwa kuwa haiwezekani kufanya majadiliano katika mikoa mitatu ya Zanzibar, Dar es Salaam na Dodoma, ilihali kuna mikoa mingi inatakiwa kuwasilisha maoni yake.

"Hawa wabunge wakipitisha mambo hayo tutashtaki kwa wananchi na kisha tunahamia mtaani tunafanya kama ilivyo Tunisia, Libya na Misri lazima kieleweke," alisema mmoja wa wanafunzi hao kwa kipaza sauti.Alisema kuwa muswada uliowasilishwa bungeni na serikali chini ya hati ya dharura haukidhi mahitaji ya Watanzania.

"Watanzania wa leo sio wa juzi au jana, hatutaki kijitabu chenye maandishi kinachoitwa katiba bali makubaliano ya utaratibu wa jinsi ya kuendesha maisha yetu katika nchi hii kwa kujadiliana kila kitu jambo linalohusu kwa manufaa ya wote, kwa haki na usawa ulioandikwa katika kitabu kitakachokuwa na kumbukumbu ya makubaliano. 

"Kwa matiki hii rasmu ya serikali inaonesha kuzidisha matatizo badala ya kuyapunguza kwa kuwa inaonesha kuwepo kwa kikundi cha watu wachache wanaotugilibu na kujitengenezea katiba ya kujilinda wao na mambo yao kwa manufaa yao. Tena wanaonesha kuwa wananufaika kwa sisi kupata shida, kwa kuwa ukisoma utagundua katika yale matatizo yetu makubwa hawataki tujadili kwa pamoja na kuyatatua," alisema.

Hata hivyo, hotuba hizo zilikatishwa baada ya kujitokeza kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. James Msekela ambaye alijikuta katika wakati mgumu kwa kuzomewa na wanafunzi hao.

"Mtoe huyo mtoe huyo mtoe huyo alitupiga mabomu, hatumtaki anaongea pumba, pumba, pumbaaaa pumbaaaa," walisikika wanafunzi hao wakisema kwa jaziba.

Dkt. Msekela alishindwa kutuliza fujo hizo hadi alipojitokeza  Mbunge wa Arusha mjini, Bw. Godbless Lema ambaye alipokewa kwa shangwe na vigelegele, 'jembee, jembee, jembee zilisikika sauti za wanafunzi hao.

Baada ya kuwashusha munkari, Bw. Lema aliwataka wanafunzi hao kuacha jazba, lakini aliulaumu utaratibu uliowekwa na bunge kwa kuwa haukuwatendea haki wananchi wanaoishi katika Mkoa wa Dodoma na migine kwa kutumia ukumbi mdogo wakati wakijua kuwa wananchi wana shauku ya kutoa maoni yao kwenye muswada huo.

"Nimewaita wanafunzi wa chuo kikuu ili kuja kujadili muswada huu kwa kuwa umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, hivi muuza mchicha, bagia anaweza kujadili muswada huu? Kuna watu wangapi wanapenda kuja hapa kujadili mustakabali nchi yao, hamuwezi kuita watu 300 ambao ni sawa na idadi ya wabunge wote," alisema Bw. Bw. Lema.

Alisema kuwa bora ofisi hiyo ikatafuta sehemu nyingine kubwa itakayoshirikisha watu wengi kujadili muswaada huo na kutoa maoni yao kwa uhuru kuliko kufanya katika chumba kidogo na kuwanyima haki watu wengine.

Mazungumzo hayo yalikatishwa na vurugu za wanafunzi hao waliotaka majadiliano hao yafanyike katika Uwanja wa Jamhuri, jambo lilopingwa na Dkt. Msekela ambaye alitaka kufanyika katika ukumbi wa Chimwaga.

Wanafunzi hao walipiga kelele kushinikiza kufanyika katika uwanja huo huku wakirusha mawe na kumzomea ndipo, Dkt. Msekela alipoamru Jeshi la Polisi kuwatanya, jambo lilozua kizazaaa katika mitaa mbalimbali ya mji wa Dodoma. 

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya vurugu hizo, Dkt. Msekela alisema kuwa ameamua kufanya hivyo kutokana na kushindwa kuelewana na wanafunzi hao, huku akimrushia lawama, Bw. Lema kuwa ndiye chanzo cha vurugu hizo.

"Ninatoa onyo kwa wanasiasa wanaojihusisha na siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma nimeambiwa kuwa jana kuna mwanasiasa mmoja alikwenda kule kuwahamasisha wanafunzi hawa," alisema Dkt Msekela.
 
Baada ya kusikia hivyo, Bw. Lema, alisema kuwa hakuna haja kuuma maneno, bali yeye ndiye aliyekwenda katika chuo hicho na kuzungumza na wanachama chama chake na atarudi tena Jumamosi.

"Mie ndiyo nilikwenda huko na kuzungumza na wanachama wangu na Jumamosi nitakwenda tena, njoo tutakutana tusitishane, si muda wa kutishana. Nimekwenda nikafanya siasa nje ya maeneo ya chuo sasa tatizo langu nini," alisema Bw. Lema. Baada ya kauli hiyo, Dkt. Msekela alionekana kunywea.

0 comments

Post a Comment