Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Slaa ataja mafisadi wapya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ametaja orodha mpya ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Vigogo hao ni Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, John Samwel Malecela, aliyekuwa Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Philip Mangula, kwa kuhusika na wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia Benki Kuu.
Dk. Slaa alitangaza majina hayo jana mjini Tabora alipokuwa akiwahutubia wanachama na wananchi waliofurika kwenye viwanja vya Chipukizi.
Alisema majina hayo ni muendelezo wa yale ya vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi aliyoyataja Septemba 15, 2007 katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam ambayo ni 11 akiwemo Rais Jakaya Kikwete.
Katika orodha ya mwaka 2007, Dk. Slaa aliwataja aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), ambaye sasa ni marehemu, Dk. Daudi Balali, Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM) na Basil Mramba aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Rombo (CCM).
Wengine ni Gray Mgonja aliyekuwa Katibu Mkuu mstaafu, Hazina, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, kada wa CCM, Nazir Karamagi, Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono (CCM), Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema katika orodha hiyo mpya Magufuli amehusika na kashfa ya uuzaji wa nyumba za serikali ambazo ziliuzwa kwa watu wasiostahili na nyingine hazikutakiwa kuwekwa sokoni.
Alibainisha kuwa katika kashfa hiyo, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa naye alihusika kwenye uamuzi huo mbovu uliosimamiwa na Magufuli, ambaye hivi sasa amepewa Wizara ya Ujenzi.
Mangula na Malecela, alisema wao walikuwa wakitoa ‘vimemo’ vilivyokuwa vikitoa maagizo ya kwenda kuchotwa fedha za EPA ambazo zilikisaidia Chama Cha Mapinduzi katika kampeni zilizomuwezesha Rais Kikwete kuingia madarakani.
Alisema Mangula alikuwa akitumia kofia yake ya ukatibu mkuu wa chama na Malecela alikuwa akitumia wadhifa wa umakamu mwenyekiti wa Bara kwa wakati huo.
Aliongeza kuwa Sumaye naye alihusika kwa kuwa alikuwa waziri mkuu na alikuwa akijua kila kilichokuwa kikiendelea lakini aliamua kunyamaza kimya na kushirikiana na wabadhirifu hao.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa ametoa siku 90 kwa Rais Kikwete, kuueleza umma zilipo sh bilioni 70 zilizorejeshwa na wezi wa EPA.
Alisema Rais Kikwete aliahidi kuwa fedha hizo zitapelekwa katika Benki ya TIB, ambako kumeanzishwa dirisha la kuwakopesha wakulima.
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), fedha hizo hazionekani zilipo kwa kuwa hakuna akaunti yoyote inayoonyesha zimewekwa.
Slaa, pia ametoa tuhuma kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba kuna upotevu wa sh bilioni 220 kwa mujibu wa taarifa ya CAG.
Alisema mfanyabiashara mwenye malori kadi za magari yake zimekuwa zikishikiliwa na TRA kwa muda wa miaka 10 sasa na ameishitaki serikali na imeamriwa kumlipa kiasi hicho cha fedha.
“Sioni sababu ya serikali kulipa kiasi hicho cha fedha wakati aliyesababisha hasara hiyo yupo na bado anaendelea kufanya kazi TRA,” alisema.
Slaa alitumia fursa hiyo kumtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, asitumie nafasi ya uspika kama jukwaa la kisiasa kwa sababu yeye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi.
Alisema Makinda anatumia nafasi hiyo kuwa mwanasiasa badala ya kufanya kazi za uspika zilizoingiliana na kazi za siasa.
Slaa, ameahidi kuwa CHADEMA itazirudisha hoja zote za ufisadi kwenye mjadala ili zijadiliwe upya kwa kuwa Kikwete ameshindwa kuchukua hatua.
Naye Mwasheria wa CHADEMA, Mabere Marando, aliwataja wafanyakazi wawili wa kampuni ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM) ya Caspian Ltd, ambao walighushi majina yao na nyaraka ili kufanikisha wizi wa sh bilioni 40.
Wafanyakazi hao ni John Kato, ambaye alijulikana kwa jina la Kamando William, na Bharaeti Goda, alijulikana kwa jina la Francis William, waliofanikiwa kuiba kiasi hicho cha fedha kupita Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd.
Alisema anao ushahidi wa jambo hilo na yuko tayari kuisaidia serikali kama ikiwapeleka mahakamani wahusika.
Naye Fred Mpendazoe, alisema kilichofanywa na CCM kujidai kujivua gamba ni usanii mtupu, kwani katika uchaguzi mkuu uliopita Kikwete mwenyewe aliwanadi watuhumiwa wa ufisadi huku akiwasifu kuwa ni viongozi bora na hakuna kama hao.
“Kama alivyo kuhani kanisani ndivyo walivyo waumini wake na kama alivyo sheikh msikitini ndivyo walivyo waumini wake…Kikwete hawezi kutenganishwa na hao waliovuliwa gamba”, alisema Mpendazoe.

0 comments

Post a Comment