Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Profesa Safari aibukia Chadema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MWANASHERIA maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari, amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).Akizungumza jana mara baada ya kukabidhiwa kadi hiyo katika Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es Salaam, Profesa Safari alisema angependa chama hicho kiyafanyie kazi mambo matatu katika harakati zake za kuchukua dola.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni nyumba za Serikali ambazo ziliuzwa kwa watumishi wake, udini na ukanda.
Alikitaka chama hicho kushughulikia kwa uzito wa kipekee suala la uuzwaji wa nyumba hizo uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu, akidai kuwa huo ulikuwa ufisadi mkubwa kuwahi kufanywa nchini.

Kwa mujibu wa Profesa Safari, kitendo hicho kilikiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 9 na kusema kwa vyovyote vile kinastahili kupingwa.

“Mambo yanayofanyika hivi sasa yalitabiriwa na Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah katika kitabu chake kwamba watatokea viongozi watakaoliuza bara hili kwa bei nafuu,”

Profesa Safari alipindekeza njia mbili za kushughulikia suala hilo. Kwanza alisema ni kwenda mahakamani au kutumia nguvu ya umma akisema hiyo ya pili ndiyo sahihi zaidi kwa mapendekezo yake.

“Suala la kwenda mahakamani kupinga uuzwaji wa nyumba za Serikali linaweza kuwa gumu kwa sababu walionunua nyumba hizo wapo na majaji. Njia ya iliyo bora ni ile ya nguvu ya umma," alisema.

Jambo jingine ambalo Profesa Safari alitaka Chadema ilifanyie kazi ni propaganda za udini na ukanda zinazoelekezwa kwa chama hicho ambazo alidai kuwa zimesukwa ili kukidhoofisha.“Wakoloni walitumia mbinu ya kutugawa katika misingi ya udini, ukabila na ukanda ili waweze kututawala na leo (CCM) wanatumia mbinu hizo,” alisema Safari na kuongeza:
“Walianza kwa kusema CUF ni chama cha Kiisilamu na watu wakaamini hata kufanikiwa kukidhoofisha na sasa wanasema Chadema ni chama cha Wakatoliki. Hizi ni propaganda."

Alitoa wito kwa wasomi na wanaharakati kuanza kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya propaganda hizo ili jamii ielewe ukweli.“Ninashukuru kwa sasa kuna vijana wengi hasa wasomi kutoka vyuo vikuu wameanza kutambua suala hilo. Wito wangu kwao ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu historia ya Taifa hili ili watu waelewe na kushiriki ukombozi wa nchi yao,” alisema.

Alisema ni suala linalotakiwa watu kukaa chini na kulifanyia kazi kwa kuwa linaweza kukidhoofisha Chadema.
“Tuliliona suala hilo wakati wa uchaguzi. Watu walitumia propaganda hiyo na wengi tulishuhudia kwani wapo waliopiga kura wakitumia sifa ya Uislamu na kuacha kiongozi mwadilifu aliyekuwa tayari kutetea tunu za Taifa,” alisema Safari.

Profesa Safari alitaka suala hilo lifanyiwe kazi na chama hicho ili kuelimisha Watanzania na kufuta dhana hiyo akidai hiyo itawezesha Taifa kuwapata viongozi wenye nia ya dhati ya kutetea rasilimali zake.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wote wa Chadema akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Profesa Safari alikumbuka adha aliyoipata na familia yake baada ya kufukuzwa kazi katika Chuo cha Diplomasia (CFR) kinachomilikiwa na Serikali kwa sababu za kisiasa.

“Niliumia mimi na familia yangu na hasa mke wangu ambaye alinishauri nisijiunge na siasa tena. Lakini, baada ya kushauriana na kushauriwa kwa muda wa miezi mitatu, nimeamua kujiunga na Chadema,” alisema Profesa Safari.
Awali, Mbowe akimkaribisha Profesa Safari, alisema Chadema imelenga kumtumia msomi huyo katika nafasi mbalimbali kadri zitakavyotokea.

“Sisi Chadema tunatambua uwezo na umakini wa Profesa Safari, tutamtumia katika vikao vyetu vyote  na katika kila nafasi zitakazojitokeza na  zaidi tutamtumia katika nafasi za uongozi kadiri itakavyowezekana”alisema Mbowe.
Akimzungumzia Profesa Safari, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema: “Nilifanya kazi naye Dodoma, ninafahamu uwezo wake na hiyo ndiyo sababu iliyonisukuma kumpigia simu usiku na kumshawishi kujiunga na Chadema.”

Profesa Safari alikuwa mwanachama wa CUF na pia mgombea uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi wake mkuu uliopita akichuana na Profesa Lipumba, alijitoa Januari 16, mwaka huu.

0 comments

Post a Comment