Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Mama wa Rais Kabila apata kikombe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mama Sifa Maanya Kabila
SASA ni dhahiri kwamba tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila, imesambaa na kuvuka mipaka ya nchi na kuanza kuzigusa familia za vigogo.Juzi, mama mzazi wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Joseph Kabila alifika katika Kijiji cha Samunge, Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro na kupata kikombe cha dawa.

Mama huyo, Sifa Maanya Kabila aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Wasso, Loliondo majira ya mchana kwa siri na kwenda moja kwa moja katika Kijiji cha Samunge ambako alipata dawa pamoja na ujumbe wake wa watu wasiozidi saba, wengi wakiwa ni kina mama.

Mwananchi lilishuhudia Mama Sifa akipanda ndege katika Uwanja za Wasso juzi jioni pamoja na ujumbe wake wakiondoka huku wakisindikizwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali na maofisa wa usalama.
 Hata hivyo, Lali alipohojiwa na Mwananchi kuhusu ujio wa Mama yake Rais Kabila alisema, hakuwa akiwafahamu waliokuwamo kwenye ndege hiyo na kudai kwamba alifika kumwombea msaada wa usafiri ndugu yakealiyekuwa akienda mjini Arusha.

Lakini, chanzo chetu cha habari kilithibitisha pasi na shaka kwamba ndege hiyo ilikuwa na ujumbe wa mama mzazi wa Rais Kabila. "Ni watu kutoka Kongo (DRC) na wameambatana na mama mzito kidogo ambaye ni mama mzazi wa Rais Kabila, wengine nadhani ni watu waliomsindikiza tu," kilisema chanzo chetu cha habari kilichokuwa katika msafara huo.Ujumbe wa Mama Sifa Kabila ulipanda ndege hiyo ya kukodi kuelekea mjini Arusha ambako ulitarajiwa kupanda ndege nyingine kuendelea na safari.

Waandishi wa habari walipofika katika Uwanja wa Ndege wa Wasso hawakuruhusiwa kuusogelea ujumbe huo kutokana na kile kilichodaiwa kuwa, watu hao walikuwa katika "safari binafsi".Sifa Maanya Kabila ambaye ni mmoja wa wake watatu wa aliyekuwa Rais wa DRC, Hayati Laurent Kabila amekuwa nadra kuonekana hadharani tangu mumewe alipofariki dunia na mtoto wake kuchukua madaraka hayo, hajawahi kuzungumza hadharani wala mbele ya vyombo vya habari.Taarifa za maofisa wa Uhamiaji waliopo Samunge zinabainisha kuwa zaidi ya wageni 500, wengi wao wakiwa raia wa Kenya, wameshafika kijijini hapo kunywa dawa.

Profesa na Dk Ishengoma nao kwa Babu
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Christine Ishengoma na mumewe, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Romanus Ishengoma walifika Loliondo kimyakimya na kwenda kijijini Samunge kunywa dawa kwa Mchungaji Mwasapila.
Profesa Ishengoma ambaye alikuwa Meya wa Manispaa ya Morogoro na Dk Ishengoma walifika Loliondo kwa ndege ya kukodi.

Habari ambazo Mwananchi lilizipata zinasema kuwa Profesa na Dk Ishengoma hawakutaka hata kukutana na maofisa usalama kwa maelezo kwamba safari yao ilikuwa ni ya kifamilia na si vinginevyo.
"Hawakutaka hata kutambulishwa kwa maofisa usalama waliokuwepo uwanja wa ndege," kilidokeza chanzo cha habari kilichowashuhudia wanandoa hao pamoja na wanafamilia wengine walipotua na kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Wasso, Loliondo.

Ujio wa Profesa Ishengoma na mkewe ni mwendelezo wa safari za vigogo katika Kijiji cha Samunge ambazo zilikuwa zimesitishwa kwa siku kadhaa kusubiri utaratibu mpya wa Serikali uliolenga kupunguza msongamano wa watu katika eneo la kutolea dawa.

Helikopta, ndege zapasua anga
Wakati ndege za kukodi zikipeana zamu za kutua katika uwanja wa Wasso, Loliondo katika Kijiji cha Samunge, helikopta za kukodi pia zimekuwa zikipasua anga la kijiji hicho ambacho hakikuwahi kuwa katika hekaheka za aina hiyo.

Timu ya waandishi wa habari wa Mwananchi iliyoweka kambi Mjini Loliondo na Samunge imeshuhudia helikopta zikitua kwa zamu katika kijiji hicho huku abiria wake wakiwa siyo vigogo wa Serikali kama ilivyokuwa awali, bali wafanyabiashara na watu wa kawaida.

Helikopta zinazotua Samunge zimekuwa zikitozwa ushuru wa Sh150,000 na abiria wake wamekuwa wakipata fursa ya kunywa dawa kwa utaratibu maalumu usio wa kupanga foleni, unaowawezesha kuondoka mapema.

Katika uwanja wa ndege wa Wasso, wastani wa ndege mbili hadi tatu zimekuwa zikitua kwa siku na abiria wake wamekuwa wakipanda magari na kusafiri umbali wa kilometa zipatazo 70 hadi nyumbani kwa Mchungaji Mwasapila.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, awali, Uwanja wa Wasso kwa wastani ulikuwa ukipokea si zaidi ya ndege mbili kwa wiki lakini sasa kazi imekuwa kubwa zaidi kutokana na wingi wa watu wanaokwenda kunywa dawa kijijini Samunge.

0 comments

Post a Comment