KAMATI ya Bunge ya Nishati na Madini, imetishia kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kama Serikali haitatekeleza ahadi ya kujenga mtambo wa umeme wa megawati 260, ifikapo Julai mwaka huu.Tishio hilo lilitolewa juzi na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Januari Makamba, alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu.
"Megawati 260 za umeme ni ahadi ya serikali. Iliahidi kuwa hadi kufikia Julai mwaka huu zitakuwa zimezalishwa. Hii ni ahadi kwa Watanzania. Kamati yangu inangoja ahadi hiyo itekelezwe na isipotimizwa, tutakwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka huu,"alisema Makamba.
Alisema bajeti ya wizara hiyo itapita kwa shida kama serikali itakuwa haijatekeleza ahadi hiyo kwa wananchi.Februari 11 mwaka huu katika mkutano wa pili wa Bunge la Kumi, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, katika swali lake la nyongeza, alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kutoa kauli kuhusu tatizo la umeme lakini.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliizima hoja hiyo kwa maelezo uwa lisingekuwa jambo rahisi kwa waziri kuzungumzia suala hilo muhimu katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.
"Suala la umeme ni janga la kitaifa ambalo halitakiwi kuchukuliwa kwa mzaha. Namuomba Waziri aliambie Bunge lako Tukufu pamoja na Watanzania wote ni lini hasa mgao wa umeme utakwisha. Atoe tamko la serikali kuhusu tatizo hilo," alisema Mbowe.
Hata hivyo, wakati Ngeleja akisimama kutaka kujieleza, Spika wa Bunge Anne Makinda alimtaka waziri huyo kutafuta muda muafaka wa kujibu swali hilo akisema kutokana na unyeti wake, swali hilo halipaswi kujibiwa kwa haraka.
Katika mkutano huo wa Bunge Ngeleja alilieleza Bunge kuwa, uwezo halisi wa mitambo yote ya kuzalisha umeme katika Gridi ya Taifa ni Megawati 1006.Katika mahojiano na gazeti hili Makamba alisema, wakati wa ahadi umekwisha na kwamba wananchi wanataka kuona utekelezaji.
Aliikumbusha serikali kuwa muda wa mwisho wa utekelezaji ahadi hiyo umekaribia."Tunataka kuwaambia, kuwa muda wa mwisho wa utekelezaji ahadi hii umepita na wakati wa ahadi bila utekelezaji umepita," alisema Makamba.
Alisema Mei mwaka huu , kamati yake itakutana na Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco na kuzitaka zitoe taarifa ya mapendekezo 30 kuhusu kumaliza matatizo ya umeme nchini.
Makamba alitumia fursa hiyo kuzungumzia uwezekano wa kujiuluzu nafasi yake kufuatia kuteuliwa kuwa Katibu wa Mambo ya Nje wa Sekretarieti ya CCM. "Sitajiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini," alisema.
Alisema hataachia nafasi hiyo kwa kuwa haina mgongano wa kimaslahi na nafasi yake ndani ya CCM na kwamba kwake kuiachia nafasi hiyo, ni sawa na kujimaliza kisiasa.Kwa mujibu wa Makamba, nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inamwezesha kufanya kazi yake vizuri zaidi.
"Nafasi hii ndani ya CCM haina mgongano na uenyekiti wangu wa kamati. Kamati ina vikao 40 kwa mwaka kazi ya kamati si uwaziri hata nikisema najivua uenyekiti bado nitakuwa mjumbe wa kamati. Sasa ni uamuzi ama nikae kama msikilizaji au nibaki kuwa mwenyekiti," alisema na kusisitiza;
"Ila nikiwepo katika kamati, nitapata nafasi zaidi ya kufanya kazi yangu vema. Kazi hii si kama ya kiserikali ya uwaziri au ukuu wa wilaya," alisema.
0 comments