Naibu waziri wa mambo ya nje nchini Libya, Khaled Kaim amesema kuwa vikosi vya jeshi la Libya vitaondoka kwenye mji uliozungukwa na majeshi hayo , unaodhibitiwa na waasi wa Misrata na badala yake watakuwepo wapiganaji wenye silaha wa kikabila.
Hakueleza ni lini wanajeshi hao watakapoondoka au kwa masharti gani. Kaim aliwaambia waandishi habari hapo jana jioni kuwa vikosi hivyo vitawaachia wapiganaji hao wa kikabila hali ilivyo katika eneo hilo la Misrata, na wakaazi wa eneo hilo. Wakati huo huo akiwa katika ziara ya mji wa Benghazi uliopo mashariki mwa nchi hiyo, Seneta wa Marekani John McCain alisema kuwa Marekani inapaswa kuchukuwa hatua zaidi.
McCain alisema pia Marekani inapaswa kutuma ndege za mashambuluzi ya ardhini dhidi ya vikosi vya Muammer Gaddafi na kuwatambua waasi nchini humo. Mjini Tripoli, ofisi ya habari ya serikali iliripoti kuwa vikosi vya shirika la kujihami la NATO,vililishambulia eneo la kati la mji huo mapema leo asubuhi. Waandishi habari wa shirika la habari la Reuters hatahivyo walisema kuwa hawakusikia miripuko yoyote ila walisikia ndege zikiruka juu ya anga ya mji huo.
0 comments