Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Dk Slaa kutaja orodha mpya ya mafisadi leo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijivua gamba kwa kuwataka wanaotuhumiwa kwa ufisadi wajiondoe wenyewe kwenye uongozi wa chama hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa leo anataja orodha mpya ya mafisadi ndani ya chama hicho tawala ili nao waunganishwe katika orodha hiyo.
Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Singo Bensoni aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Dk Slaa atataja majina hayo leo mkoani Tabora katika mkutano wa hadhara kama alivyofanya mwaka 2007, katika Viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam.
Alisema katika mkutano huo, Dk Slaa akiwa na viongozi wengine wa Chadema, atataja majina hayo ya mafisadi ili kuipa CCM wakati mzuri wa kuwatambua na kuwachukulia hatua kama kweli ina nia njema ya kujivua gamba.
Hii ni changamoto mpya kwa CCM ambayo tayari imenyooshea kidole genge la mafisadi lililoko ndani ya chama hicho na kuwapa siku 90 watuhumiwa hao kujiuzulu ili kukinusuru.

Bensoni aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa orodha hiyo mpya ya mafisadi inayotarajiwa kutajwa leo, ni kubwa kuliko ile ya mwaka 2007.“Ushahidi tunao ndiyo maana hata tuliowataja mwaka 2007 hadi leo hawajafungua kesi yoyote mahakamani. Wanasema kuwa wamejivua gamba. Gamba la CCM siyo uzee ni ufisadi,” alisema Bensoni na kuongeza: “Tutawakumbusha gamba wanalotakiwa kujivua ni lipi ili Watanzania watambue. Dk Slaa ataweka mambo hadharani katika mkutano huo akiwa pamoja Profesa Abdalah Safari na Mabere Malando.”

Alisema licha ya CCM kutoa siku 90 kwa watuhumiwa wa ufisadi wanaotajwatajwa, wapo ambao hawajatajwa kati ya waliotakiwa kujiuzulu kwa tuhuma za hizo.“Hapa sasa ndiyo watajua mafisadi ni kina nani. Tunataka kuwakumbusha gamba ni lipi.”

Alisema kuwa orodha hiyo ni mpya na ina tofauti na ile ya Mwembeyanga kwa kuwa tangu kipindi hicho mpaka leo kuna matukio mengi ya ufisadi yaliyoendelea nchini.“Ufisadi wa sasa ni mkubwa sana hivyo orodha itakuwa kubwa, ‘Ni ngoma nzito’ na tukimaliza kutaja orodha hiyo tutaendelea na mikutano yetu nchi nzima,” alisema Bensoni.
Akizungumzia hatua hiyo ya Chadema, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: "Chadema wamefilisika kisiasa, walidhani wataitisha CCM kwa hoja ya ufisadi lakini sasa CCM ni chama safi. Kwa mabadiliko tuliyoyafanya, Chadema inatakiwa kucheza ngoma yetu (CCM) na siyo sisi (CCM) kucheza ngoma yao."
Nape alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kukubali kurudisha muswada wa Katiba kwa wananchi na kuwapa fursa zaidi kujadili suala hilo.

0 comments

Post a Comment