SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amesema baada ya kupitia maelezo na ushauri wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, ameridhika na kuona ni busara kutoa muda zaidi kwa kamati kuendelea na kazi ya kuchambua muswada wa Marejeo ya Katiba.
Akitoa uamuzi wake kuhusu muswada huo bungeni jana, Makinda alisema kamati itaendelea kuchambua maoni ambayo tayari yametolewa na wadau na itakusanya mengine, kwa lengo la kuboresha zaidi muswada huo ili kuwa na manufaa zaidi.
“Naomba Watanzania kudumisha mila zetu za utulivu na amani, muswada kwa lugha ya kibunge ni mapendekezo tu, safari hii ni mapendekezo ya Serikali kuhusu namna ya kuanzisha zoezi la kuandika Katiba ya nchi,” alisema.
Alisema Bunge linawaomba wananchi, wasomi, wafanyakazi, wanawake, wanafunzi, wana vyuo, mashirika yasiyo ya kiserikali, walemavu, wakulima, madhehebu ya dini, vyama vya siasa na makundi mengine ya jamii, wajadili mapendekezo ya muswada.
“Tuache malumbano, kuzomeana na maandamano. Wanasiasa tuache kushindana majukwaani, tujadili muswada. Maoni, ushauri na mapendekezo ndiyo yatasababisha kutungwa kwa sheria nzuri,” alisema Makinda.
Spika aliwataka wananchi kuiamini Kamati ya Bunge, kwa sababu imejaa watu wenye uzoefu mkubwa na waliobobea kwenye taaluma mbalimbali ikiwamo sheria.Alisema muswada huo siyo mali ya chama chochote cha siasa na kwamba, busara zaidi zitumike na mtu anayebainisha lisilofaa awe tayari kutaja linalostahili kuwapo.
“Tunaitaka Serikali ilete muswada kwa Kiswahili na uandikwe kwenye magazeti mbalimbali, ili watu wote wasome wenyewe, waulize maswali, waondoe jazba ambazo hazina mantiki,” alisema Makinda na kuongeza:
“Uandikaji wa Katiba mpya iwe chanzo cha kutuunganisha Watanzania wote na kuimarisha utaifa wetu. Lengo letu ni kuwa na Tanzania moja yenye amani na utulivu.”
Makinda alisema wananchi wanatakiwa kupeleka maoni yao kwa Kamati ya Bunge kupitia ofisi za Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar, huku akiagiza kamati hiyo kumpelekea ratiba na utaratibu wa kukamilisha kazi ya muswada, ili uweze kusomwa mara ya pili mkutano ujao wa Bunge.
“Nasisitiza utulivu wakati wote wa kazi hii. Kila mwana kamati ajue kwamba shughuli hii inatawaliwa na Kanuni za Bunge na itaratibiwa na kusimamiwa na kamati husika na siyo vyama vya siasa,” alisema Makinda.
Akizungumzia hatua hiyo ya Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema Chadema kimesitisha maandamano yake ambayo yalikuwa yafanyike leo nchi nzima kupinga upitishaji wa muswada huo kuwa sheria.
“Chadema tunasema tumesitisha maandamano yetu, tunataka Watanzania watuelewe. Tunasubiri Serikali ili tuone hiyo nia njema inayotaka kuonyesha inakuja kwa njia gani,” alisema Mbowe.Mbowe alilaumu hatua ya Serikali kupeleka muswada huo kuwa umesababisha hofu, malumbano na migongano mikubwa kwa taifa.
“Ule muswada unaweza ukaandikwa na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa sheria, Serikali inaleta muswada kama ule na upungufu wote huo. Taarifa za uhakika ni kwamba wenzetu wa Zanzibar hawakushirikishwa wakati wao ni sehemu ya Serikali ya Muungano,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Vikao vya Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho kinachoongoza Serikali, vikao vya maamuzi ya kisera kama Nec (Halmashauri Kuu ya CCM), havikuwa na taarifa ya mabadiliko ya Katiba.
Ukweli ni kwamba kilikurupuka kikundi kidogo cha watu kikapata baraka za Rais, kikaleta muswada bungeni ambao ulikuwa haujapata hata baraka za chama chake.”Alisema mabadiliko ya Katiba ni makubwa kwenye taifa hivyo kitendo cha Serikali kupeleka mabadiliko hayo kwenye Bunge bila kushirikisha hata vikao vya chama ni aibu.
“Hii haikuwa sera ya CCM, ingekuwa Serikali inatekeleza sera ya chama chake ingekuwa haina tatizo. Hii haikuwa sera ya CCM, haikuwa sehemu ya vipaumbele vya chama hicho kwenye ilani ya uchaguzi uliopita, ilinyofoa kipengele hiki cha hoja ya mabadiliko ya Katiba baada ya shinikizo kubwa la kitaifa na pekee shinikizo kubwa la Chadema,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Mpaka tukaenda bungeni tukadai Serikali ifanye mabadiliko, lakini kwa utaratibu wa kawaida wa utawala bora, vyama vya siasa na vyombo vyake vya kufanya maamuzi ya kisera hasa yanapokuwa makubwa kama haya, vishirikishwe kama wadau.”
Mbowe alidai kuwa CCM wana tabia ya kubeba hoja bila kuangalia undani wake na kwamba hilo lilijidhihirisha jana wakati Spika akitoa uamuzi, wabunge wa CCM walishangilia ilhali Serikali yao ndiyo iliyopeleka hoja isiyo sahihi.
Akizungumzia hatua hiyo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema Singo Bensoni aliielezea hatua hiyo kuwa ni .“Ushindi wa nguvu ya umma dhidi ya mafisadi wa Katiba.”
Alisema maandamano ya chama hicho yalikuwa na malengo matatu ambayo kutokana na uamuzi wa Spika, mawili yameshapatiwa ufumbuzi ambayo ni kuondoa muswada bungeni pamoja na muswada huo kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
0 comments